Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima Zanzibar aliyepo kulia yake Dr. Hamed Rashid Hikman, ambapo kushoto yake ni Mkuruigenzi Mtendaji wa Shirika hilo Abdulnaasir Abdulrahman kabla ya kuzungumza na watendaji wa shirika hilo tawi la Lumbumba Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Bima Zanzibar Tawi la Lumbumba Jiijini Dar es salaa alipofanya ziara ya kuzitembelea Taasisi za SMZ zilizopo Dar.
Meneja wa Benki ya watu wa Zanzibar { PBZ } Tawi la Kariakoo Jijijni Dar es salaam Badru Idd akitoa maelezo ya utendaji wa tawi hilo na Lile ya Benki ya Kiislamu liliopo Lumumba mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyekuwa katika ziara maalum ya kutembelea Taasisi za SMZ zilizopo Jijini Dar.
Pembeni yao
kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Makao Makuu
Zanzibar Juma Amour Mohammed.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar wa Matawi ya Kariakoo na Lumbumba kwenye ukumbi wa Tawi la Benki hiyo inayotoa huduma za Kiislamu uliopo Lumumba Jijini Dar es salaam.
Picha na
Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Jitihada kubwa zinazoendelea
kuchukuliwa na Uongozi pamoja na Wafanyakazi wa Shirika ya Bima la Zanzibar {
ZIC } na ule wa Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } ndizo zilizopelekea kuongezeka zaidi kwa idadi ya wananchi na
wateja wanaohitaji kupata huduma katika Taasisi hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuzitembelea ofisi za Taasisi
hizo zinazotoa huduma katika Jiji la Dar es salaam na kuelezea kuridhika kwake
na utendaji bora wa kisasa uliofikiwa na mashirika hayo.
Balozi Seif alisema licha ya kuvutiwa sana na utaratibu wao wa
makusanyo ya mapato na matumizi ya wastani lakini bado watendaji wa taasisi
hizo wanapaswa kujituma zaidi katika mbinu za kutafuta wateja kwa lengo la
kwenda sambamba na ushindani uliopo wa kibiashara.
Alifahamisha kwamba mbinu za
kumchunga mteja wakati wote zitafanikiwa endapo juhudi za ziada za utoaji
huduma kwa mwendo wa kasi kupitia watendaji hao zitachukuliwa.
“ Tuna kila sababu ya kuyapongeza
mashirika yetu haya kutokana na huduma zao zinazokwenda kwa kasi. Haya ni
miongoni mwa mashirika yanayoinawisha uso Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Tuna haki ya kujivunia “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliziagiza Taasisi hizo za Bima na PBZ mbali ya kuendelea kujitangaza lakini
pia kufikiria kuongeza matawi mengine zaidi katika maeneo yenye mkusanyiko wa wananchi
wengi yakiwemo yale ya Vijijini ili huduma zao ziwe za uwiano katika maeneo
yote ya hapa Nchini.
Alieleza katika kuzipa nguvu zaidi
taasisi hizo Serikali Kuu itaangalia utaratibu wa kuzikatia Bima mali zake
yakiwemo majengo mapya ya Ofisi za Serikali zinazoendelea kujengwa katika
maeneo tofauti Nchini.
“ Hata nyumba zangu niko tayari
kuzikatia bima, kinachohitajika kwa sasa ni nyinyi watendaji kunishawishi hadi
nifikie kiwango cha kutekeleza wazo hilo muhimu “. Alieleza Balozi Seif.
“ Tumekuwa pia tukishuhudia mikopo
mikubwa inayotolewa na Benki ya Watu wa Zanzibar na ii ni vyema ikaenda samba mba na uwekaji wa
bima ya maisha ili kunusuru kiwango kikubwa cha mikopo kinachotolewa endapo
mkopaji mwenyezi Muungu atamuhitaji “. Aliendelea kufafanua Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar.
Akitoa Taarifa ya Shirika la Bima
Zanzibar na Utekelezaji wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika hilo Abdulnaasir Abdulrahman alisema hali ya soko
inaendelea kuwa ya ushindani ambapo biashara kubwa ikitawaliwa na ile ya kinga
za magari.
Alisema biashara hiyo inachangia
zaidi ya asilimia 80% ya biashara yote hali inayopelekea uongozi wa shirika
kufanya juhudi za kuandikisha biashara nyengine ambazo zina faida kubwa
ikilinganisha na ya magari.
Mkurugenzi huyo wa shirika la Bima
alifahamisha kwamba shirika hilo limeweza kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni
1.1 kutoka katika vianzio vyake mbali mbali sawa na asilimia 86% ya lengo lake
ambalo ni kukusanya shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka 2013.
Abdulnaasir alisema Kanda ya Pwani
Dar es salaam ni tegemeo kubwa la shirika kwa makusanyo yake ambapo katika
kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu
Ofisi hiyo tayari imeshakusanya shilingi Bilioni 2.1 ikiwa ni sawa na asilimia
87% ya makadirio ya mwaka.
Alisema katika kukabiliana na
ushindani wa kibiashara shirika lake licha ya kufanya kazi zake Zanzibar lakini
pia limeweza kujitanua kwa kufungua
ofisi zaidi katika kanda za Pwani- Dar es salaam, Arusha, Mwanza, mbeya, Dodoma
na Mtwara.
Naye akitoa Taarifa ya maendeleo ya
Matawi ya Benki ya Watu wa Zanzibar yaliyopo Kariakoo na Lumumba Mjini Dar es salaam Meneja wa Tawi la Kariakoo
Badru Idd alisema PBZ ilipanga kuwafuata
wateja wake waliopo na wanaokwenda Tanzania Bara kikazi, kibiashara, kimasomo
na wanaopita ambao wanahitaji huduma za Kibenki.
Meneja Badru alisema pamoja na kuwepo
kwa ushindani mkubwa wa kibiashara lakini matawi hayo yameweza kufungua hesabu
za wateja mbali mbali na kufikia elfu 8,360 kutoka 3,209 ikiwa ni ongezeko la
asilimia 160% .
Alifahamisha kwamba amana za wateja
zimekuwa kwa kiwango kizuri na kufikia Shilingi Bilioni 24.58 mwezi agosti mwaka 2013 wakati disemba 31
mwaka 2011 zilikuwa Shilingi Bilioni 3.99 ikiwa ni ongezeko la asilimi 516%.
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alikutana na Uongozi wa shirika la Meli na Uwakala Zanzibar Tawi la
Dar es salaam na kuwaasa kwamba wana kazi kubwa ya kulihudumia shirika hilo
katika mazingira ya uwajibikaji.
Balozi Seif alisema shirika hilo
linaweza kupoteza imani ya wateja kwa kufikia hatua ya kukata tamaa endapo
uendeshaji wa taasisi hiyo hautakuwa wa kiwango na uhakika.
Shirika la Meli na uwakala
limeasisiwa mwaka 1978 likiwa na Meli sita zikiwemo mbili zilizorithiwa kutoka
ukoloni ambazo zilikuwa zikitoa huduma katika mwambao wa Afrika ya mashariki
kuanzia Mtwara Tanzania, Zanzibar, Tanga hadi Mombasa Nchini Kenya.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar alifanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Taifa la Biashara
Zanzibar { ZSTC } ambapo aliushauri uongozi wa shirika hilo kuanzisha utaratibu
wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuwapatia bidhaa zinazozalishwa
Tanzania Bara kwa bei nafuu.
Balozi Seif alisema utaratibu huo
unaweza kutoa fursa zaidi ya kuongeza kipato cha wafanyabiashara hao ambao
wengi hawana uwezo wa kufuatilia bidhaa hizo katika maeneo mbali mbali ya mIkoa
ya Tanzania Bara.
Akitoa Taarifa fupi Naibu Mkurugenzi
muendeshaji wa shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } Suleiman Juma
Jongo alisema lisha ya shirika hilo lililoasisiwa katika miaka ya 70 kuendesha
shughuli za ununuzi na uuzaji wa karafuu lakini bado lina fursa ya kuendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake
kiuchumi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
22/8/2013.
No comments:
Post a Comment