Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi ameitahadharisha Jamii nchini kujiepusha na tabia za
baadhi ya watu wanaotumia dini katika ushawishi wa kuhatarisha amani ya Nchi.
Alisema uchezewaji wa amani hiyo
endapo utavurugika watakaoumia na kupata shida na taabu ni wananchi waliowengi na
kamwe hazitowagusa wale waliochangia ushawishi wa kuivuruga amani hiyo.
Balozi Seif alitoa kauli hiyo nzito
mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Afisi
Kuu Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Umoja huo uliopo hapo Jimkana Mjini
Zanzibar.
Alisema wananchi walio wengi wamekuwa
wakishuhudia hotuba za uchochezi zilizokuwa zikitolewa katika baadhi ya
misikiti na mmoja wa sheikh kutoka nje ya Zanzibar ambazo zinahatarisha amani
ya Nchi.
Aliwatahadharisha wananchi hasa
Vijana kuacha kununua au kutumia kanda zilizorekodiwa hivi karibuni na mhadhiri
huyo na kusambazwa katika maeneo mbali mbali nchini.
“ Amekaanga mbuyu yeye na hivi sasa
hayupo. Lakini hata Mama watoto wake hayupo, watoto wake hawapo na mama yake
pia hayupo. Sasa kapanda chuki jamii inapaswa kujihadhari nayo chuki hiyo.
Likitokea vurugu lolote lile tutakaoumia ni sisi na wala sio yeye aliyekaanga
mbuyu hizo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Taifa limekuwa
katika hali ya amani kwa kipindi kirefu sasa hali ambayo ni muhimu katika
kustawisha ustawi wa wananchi wote Mjini
na Vijijini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alikumbusha
kwamba bila ya amani wananchi wasingepata fursa ya kuendelea na shughuli zao za
kimaisha za kila siku.
Alisisitiza kwamba wananchi wakati
wote wana wajibu wa kukataa maovu sio
katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani bali hata katika miezi
mengine ya kawaida ili waendelee kuishi
kwa amani na upendo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Umoja wa
Vijana wa CCM Afisi Kuu Zanzibar Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali
Vuai alisema Zanzibar ina hazina kubwa
ya Uislamu.
Alisema hazina hiyo ambayo nadra
kupatikana katika baadhi ya Nchi haipaswi miongoni mwa waumini wakaichezea kwa
kuwaalika mahadhiri wa nje ya Zanzibar kuja kufitinisha waumini.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM
Zanzibar alimpongeza Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr.
Ali Mohammed Sheni na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
kwa kauli zao za kila wakati za kusisitiza umuhimu wa kuitunza amani wakati wote.
Vuai Ali Vuai alishauri na kuomba
suala hili muhimu kwa ustawi wa Taifa hili lazima likaungwa mkono na vyombo vya
Dola hapa Nchini.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
4/8/2013.
No comments:
Post a Comment