Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha salamu za pole kwa Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso kufuatia uwanja wa ndege wa Kimataifa wan chi hiyo kukum bwa na Moto.
Pembeni yao
kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh.
Mohammed Aboud Mohammed.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Balozi wa Kenya Nchini Tanzania anayemaliza muda wake wa utumishi wa miaka minne zawadi ya kasha kama kumbu kumbu ya kuwepo kwake Nchini.
Press release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imetoa pole kwa Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya kutokana na maafa ya moto
mkubwa uliokikumba Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyata Kiliopo
Mjini Nairobi Nchini humo na kusababisha hasara kubwa ambayo bado
haijajuilikana.
Moto huo umesabisha safari zote za
ndege zilizopangwa kuingia na kutoka kwenye uwanja huo kusitishwa na kupelekea
ndege hizo kutua katika viwanja vyengine vya ndege vya Eldoret, Mombasa na Nchi
jirani za Afrika Mashariki.
Pole hiyo imetolewa na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofanya mazungumao na Balozi
wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso aliyefika kumuaga hapo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kumaliza muda wa utumishi wake wa miaka
minne hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Wananchi wa kenya
wamekumbwa na maafa hayo yaliyosababisha kutishia kutetereka kwa uchumi wake
unaotegemea kwa kiasi kikubwa huduma zinazotolewa na Uwanja huo katika ukanda
mzima wa Bara la Afrika ukiunganisha ndegembali mbali za Kimataifa.
Alisema gharama za kuufanyia
matengenezo uwanja huo ni kubwa kufuatia moto huo uliotokea mapema alfajiri ya Jumatano katika eneo la kuwasili
abiria kabla ya kusambaa hadi maeneo mengine likiwemo lile la Idara ya
Uhamiaji.
Alifahamisha kwamba umefika wakati
kwa Waafrika kuwa makini na vitendo vya kuwatia hofu wananchi { Ugaidi }
ambavyo vinaweza kusababisha ukosefu wa utulivu na amani miongoni mwa Jamii.
Alimueleza Balozi Huyo wa Jamuhuri ya
Watu wa Kenya Nchini Tanzania kwamba Vitendo vya Kigaidi vinavyoonekana
kujitokeza katika Nchi mbali mbali Duniani vikilikumba pia Bara la Afrika
humfanya Mtu aishi katika maisha ya hofu na wasi wasi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alimpongeza Balozi huyo wa Kenya Nchini Tanzania kwa juhudi zake za utumishi
zilizochangia kuimarika zaidi kwa
uhusiano wa kudugu uliopo kati ya Kenya na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Balozi Seif alisema Wananchi wa
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hasa wale wanaoishi katika ukanda wa Pwani ya
Mwambao wa Afrika Mashariki wamekuwa na uhusiano wa karibu na kidugu na wenzao
wa Taifa la Kenya.
Alishauri uhusiano huo ukazidi
kuimarishwa kwa faida ya wananachi wa pande hizo mbili hasa kwa kuzingatia
zaidi muingiliano uliopo kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki iliyounganisha
harakati za kiuchumi za mataifa wanachama.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa
Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso alisema upo umuhimu wa wana Jumuiya
ya Afrika Mashariki kuendelea kuikuza na kuithamini Lugha ya Kiswahili kwa
lengo la kuipa heshima yake Kimataifa.
Balozi Mutiso alisema inasikitisha
kuona wenye Lugha ya Kiswahili wanaendelea kusua sua wakati lugha yenyewe
kimataifa inazungumzwa takriban na watu zaidi ya Milioni mia mbili na arubaini
duniani kote ikiwa lugha ya nne kwa ukubwa duniani hivi sasa.
“ Takwimu za watu wanaozungumza
Kiswahili Duniani ndizo zilizonishawishi mimi kufikia uwamuzi wa kutunga Kamusi
la Kingereza kwa Kiswahili kupitia mfumo wa Kidiplomasia ili kutoa mchango
wangu katika kukuza lugha yetu ya Afrika Mashariki. Mchango wangu huu pia
nimekusudia uwasaidie wanadiplomasia wenzangu “. Alifafanua Balozi Mutinda.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao hivi sasa unapita katika hatua ya
Rasimu ya Katiba hiyo Balozi Mutinda Mutiso ameipongeza Tanzania kwa hatua yake
hiyo yenye muelekeo wa kutandika Demokrasia zaidi.
Balozi Mutinda alisema Waafrika walio
wengi wanatarajia kukiona kipindi cha mpito cha kuelekea kwenye Katiba Mpya Nchini
Tanzania kinakuwa kigezo na mfano bora wa kuigwa na kuungwa mkono na Mataifa
mbali mbali ya Bara la Afrika.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iliyoamua kufuata mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambao umeleta utulivu, amani
na umoja miongoni mwa Wazanzibari walio wengi baada ya mgongano wa mrefu wa
kisiasa uliovikumba vyama vikuu viwili vya kisiasa.
Balozi Mutinda alisema inapendeza
kuona Zanzibar hivi sasa imetulia kisiasa kwa kuwa na mfumo huo wa Serikali ya
pamoja unaofaa kupongezwa na kuigwa na Mataifa mengine yanayotaka kuelekea
kwenye demokrasia zaidi ndani na nje ya Bara la Afrika.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
8/8/2013.
No comments:
Post a Comment