Sunday, 25 August 2013

Rais Dk.Shein afanya mabadiliko ya Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha  Salum Maulid Salum, kuwa Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora,katika hafla iliyofanyika Ukumbi
wa Ikulu Mjini Zanzibar.[Picha na Ramadhan
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha Joseph Abdalla Meza,kuwa Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ,katika hafla
iliyofanyika Ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha Mwinyiussi A.Hassan,kuwa Naibu Katibu
Mkuu (Tawala za Mikoa)  katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa ikulu
Mjini Zanzibar
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha CDR Julius Nalimy Maziku,kuwa  Naibu
Katibu Mkuu (Idara Maalum za SMZ) katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa
ikulu Mjini Zanzibar
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha  Yakout Hassan Yakout, kuwa  Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma,katika hafla
iliyofanyika Ukumbi wa ikulu Mjini Zanzibar
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akimuapisha ALI Khamis Juma,kuwa Naibu Katibu
Mkuu (Ustawi wa Jamii Vijana Wanawake na Watoto),katika hafla
iliyofanyika Ukumbi wa ikulu Mjini Zanzibar























Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraz la Mapinduzi
Dk.Ali Mohamed Shein,akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Naibu
katibu Wakuu wa Wizara mbali mbali baada ya kuwaapisha Ikulu Mjini
Zanzibar leo jioni.

Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Viongozi wa CCM wakati wa hafla ya Kulizindua rasmi Baraza la ushauri la Viongozi wakuu wa CCM Makao Makuu Mjini Dodoma.

 Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Viongozi wa CCM wakati wa hafla ya Kulizindua rasmi Baraza la ushauri la Viongozi wakuu wa CCM Makao Makuu Mjini Dodoma.
 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dr. Jakaya Mrisho Kiwete akibonyeza kitufe kuashiria kulizindua Baraza la ushauri la Viongozi wakuu wa CCM Makao Makuu Mjini Dodoma.

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dr. Jakaya Mrisho Kiwete akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la ushauri la Viongozi wakuu wa CCM mara baada ya kulizindua  rasmi Makao Makuu Mjini Dodoma.Kulia yake ni Mzee Ali Hassan mwinyi, Mzee John Malecela,Rais wa Zanzibar Dr. AIi  Mohammed Sheni  na Mh. Mizengo Pinda. Na Kushoto ya Dr. Kiwete ni Mh. Benjamin Mkapa, Dr. Amani Abeid Karume na Mh. Pius Msekwa.

 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dr. Jakaya Mrisho Kiwete akiingia katika viwanja  vya Makao Makuu wa Chama hicho Mjini Dodoma akiwa ni viongozi wa Baraza la ushauri la Viongozi wakuu wa CCM alilolizindua rasmi.

 Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi Mh. Benjamin William Mkapa akibadilishana mawazo na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume katika hafla ya uzinduzi ya Baraza la Ushauri la Viongozi  wakuu wa CCM Mjini Dodoma.
























Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mzee Ali Hassan Mwinyi akizungumza na Makamu mwenyekiti wa CCM na Rais nwa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni katika hafla ya uzinduzi ya Baraza la Ushauri la Viongozi  wakuu wa CCM Mjini Dodoma.

Press Release:-
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinzuzi Taifa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kuundwa kwa Baraza la ushauri la Viongozi Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi ni  fursa maalum na nzito itakayosaidia kuimarisha zaidi nguvu ya Chama hicho.
Dr. Kikwete alisema hayo katika hafla maalum ya uzinduzi wa Baraza hilo linalojumuisha Wenyeviti, Makamu wenyeviti na Makatibu wakuu wastaafu wa Chama hicho iliyofanyika katika viwanja vya Makamu Makuu ya Chama hicho yaliyopo katika Manispaa ya Dodoma.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alifahamisha kwamba Wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na uwezo kamili wa kushauri hata kuingia katika Vikao vya Juu vya CCM katika masuala mazito yatakayokijengea mustakabala mzuri wa baadae chama hicho.
Dr. Kikwete alieleza kuwa Uongozi wa CCM ulifikia uwamuzi wa kuundwa kwa Baraza hilo katika Mkutano wake Maalum wa nane Novemba Mwaka 2012 kupitia Ibara ya 127 ya chama hicho baada ya kutambua na kuheshimu mchango wa Viongozi hao.
Alisema Wana CCM  wanastahiki kujipongeza kutokana na ushauri huo ambao uliwahi kupingwa wakati wa nyuma kwa hofu ya Kikundi hicho kutengeneza fitina za kumuingilia Rais katika maamuzi mazito.
Dr. Kikwete alisema Tanzania imepata mafanikio makubwa kutokana na mabadiliko ya Kiuchumi na hata utulivu wa kisiasa kufuatia mchango wa Viongozi wastaafu ambao kwa sasa watakuwa wakitoa mawazo yao kwa chama kupitia Baraza hilo.
Dr. Kikwete alimtolea mfano  Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mzee Ali Hassan Mwinyi kuwa ni wa kwanza wa mabadiliko ya Uchumi na Siasa ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika miaka ya mwishoni mwa 80 na mwanzoni mwa 90.
“ Mzee Mwinyi ametuongoza katika mabadiliko  hayo ya kiuchumi sambamba nay ale ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa NchinibnTanzania licha ya yeye kutowahi kuufanyika kazi Mfumo huo “. Alifafanua Dr. Kiwete.
“ Ukweli tuseme mageuzi ya kiuchumi yaliyofanyika Tanzania chini ya uongozi wa Mzee Mwinyi wengine wakimwita Mzee Ruksa mimi ndie  niliyeanza kuyafaidi katika kazi zangu za Urais “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.
Aliongeza kwamba mfumo huo wa kuundwa kwa Baraza la Ushauri la Viongozi wa Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi litaondoa usumbufu wa kuwapa tabu wazee hao wa kuitwa mara kwa mara katika Vikao vya Chama kwa lengo la kupata ufumbuzi wa mambo.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za CCM Ibara ya 127 Baraza hilo litakuwa na uwezo kamili wa kushauri hata ndani ya Vikao vya juu vya Chama ama kwa kushiriki wajumbe wote wa baraza au hata uwakilishi wao.
Mapema Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Abdullrahman Kinana alisema Baraza hilo linalojumuisha Marais wastaafu wa Serikali ya Muungano na Wenyeviti wastaafu wa CCM Taifa Marais wastaafu wa Zanzibar kupitia  na Makamu Wenyeviti wastaafu CCM Zanzibar na Bara litafanya vikao vyake kwa mujibu wa utaratibu watakaojipangia wenyewe.
Katibu Mkuu wa CCM Kikana alisema wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na fursa ya kutoa ushauri kwa Serikali zinazoongozwa na Chama cha Mapinduzi Bara na Zanzibar.
Viongozi hao wanaounda Baraza hilo la Ushauri la Viongozi wakuu wa CCM waliopata fursa ya kuhudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa SMT awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi pamoja na aliyemfuatia Mh. Benjamin William Mkapa.
Wengine waliohudhuria ni Makamu mwenyekiti Msaafu na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Mh. Pius Msekwa.
Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dr. Salimin Amour hakuhudhuria hafla hiyo kutokana na sababu za kiafya wakati Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Phillip Mangula yeye alikuwa na udhuru wa msiba.
Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alibonyeza kitufe maalum kuashiria kuzindua  Baraza hilo hafla iliyoambatana na ngoma za vikundi vya utamaduni pamoja na muziki wa kizazi kipya.
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/8/2013.
 

Wednesday, 21 August 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika ziara ya kuzitembelea Taasisi za SMZ zilizopo Dar.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima Zanzibar aliyepo kulia yake Dr. Hamed Rashid Hikman, ambapo  kushoto yake ni Mkuruigenzi Mtendaji wa Shirika hilo Abdulnaasir Abdulrahman kabla ya kuzungumza na watendaji wa shirika hilo tawi la Lumbumba Jijini Dar es salaam.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Bima Zanzibar Tawi la Lumbumba Jiijini Dar es salaa alipofanya ziara ya kuzitembelea Taasisi za SMZ zilizopo Dar.

 Meneja wa Benki ya watu wa Zanzibar { PBZ } Tawi la Kariakoo Jijijni Dar es salaam Badru Idd akitoa maelezo ya utendaji wa tawi hilo na Lile ya Benki ya Kiislamu liliopo Lumumba mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyekuwa katika ziara maalum ya kutembelea Taasisi za SMZ zilizopo Jijini Dar.
Pembeni yao kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Makao Makuu Zanzibar Juma Amour Mohammed.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Bima Zanzibar Tawi la Lumbumba Jiijini Dar es salaa alipofanya ziara ya kuzitembelea Taasisi za SMZ zilizopo Dar.























Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar wa Matawi ya Kariakoo na Lumbumba kwenye ukumbi wa Tawi la Benki hiyo inayotoa huduma za Kiislamu uliopo Lumumba Jijini Dar es salaam.
Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Uongozi pamoja na Wafanyakazi wa Shirika ya Bima la Zanzibar { ZIC } na ule wa Benki ya Watu wa Zanzibar          { PBZ } ndizo zilizopelekea  kuongezeka zaidi kwa idadi ya wananchi na wateja wanaohitaji kupata huduma katika Taasisi hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya kuzitembelea ofisi za Taasisi hizo zinazotoa huduma katika Jiji la Dar es salaam na kuelezea kuridhika kwake na utendaji bora wa kisasa uliofikiwa na mashirika hayo.
Balozi Seif alisema  licha ya kuvutiwa sana na utaratibu wao wa makusanyo ya mapato na matumizi ya wastani lakini bado watendaji wa taasisi hizo wanapaswa kujituma zaidi katika mbinu za kutafuta wateja kwa lengo la kwenda sambamba na ushindani uliopo wa kibiashara.
Alifahamisha kwamba mbinu za kumchunga mteja wakati wote zitafanikiwa endapo juhudi za ziada za utoaji huduma kwa mwendo wa kasi kupitia watendaji hao zitachukuliwa.
“ Tuna kila sababu ya kuyapongeza mashirika yetu haya kutokana na huduma zao zinazokwenda kwa kasi. Haya ni miongoni mwa mashirika yanayoinawisha uso Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tuna haki ya kujivunia “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Taasisi hizo za Bima na PBZ mbali ya kuendelea kujitangaza lakini pia kufikiria kuongeza matawi mengine zaidi katika maeneo yenye mkusanyiko wa wananchi wengi yakiwemo yale ya Vijijini ili huduma zao ziwe za uwiano katika maeneo yote ya hapa Nchini.
Alieleza katika kuzipa nguvu zaidi taasisi hizo Serikali Kuu itaangalia utaratibu wa kuzikatia Bima mali zake yakiwemo majengo mapya ya Ofisi za Serikali zinazoendelea kujengwa katika maeneo tofauti Nchini.
“ Hata nyumba zangu niko tayari kuzikatia bima, kinachohitajika kwa sasa ni nyinyi watendaji kunishawishi hadi nifikie kiwango cha kutekeleza wazo hilo muhimu “. Alieleza Balozi Seif.
“ Tumekuwa pia tukishuhudia mikopo mikubwa inayotolewa na Benki ya Watu wa Zanzibar na  ii ni vyema ikaenda samba mba na uwekaji wa bima ya maisha ili kunusuru kiwango kikubwa cha mikopo kinachotolewa endapo mkopaji mwenyezi Muungu atamuhitaji “. Aliendelea kufafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akitoa Taarifa ya Shirika la Bima Zanzibar na Utekelezaji wake  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Abdulnaasir Abdulrahman alisema hali ya soko inaendelea kuwa ya ushindani ambapo biashara kubwa ikitawaliwa na ile ya kinga za magari.
Alisema biashara hiyo inachangia zaidi ya asilimia 80% ya biashara yote hali inayopelekea uongozi wa shirika kufanya juhudi za kuandikisha biashara nyengine ambazo zina faida kubwa ikilinganisha na ya magari.
Mkurugenzi huyo wa shirika la Bima alifahamisha kwamba shirika hilo limeweza kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 1.1 kutoka katika vianzio vyake mbali mbali sawa na asilimia 86% ya lengo lake ambalo ni kukusanya shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka 2013.
Abdulnaasir alisema Kanda ya Pwani Dar es salaam ni tegemeo kubwa la shirika kwa makusanyo yake ambapo katika kipindi cha  Januari hadi Juni mwaka huu Ofisi hiyo tayari imeshakusanya shilingi Bilioni 2.1 ikiwa ni sawa na asilimia 87% ya makadirio ya mwaka.
Alisema katika kukabiliana na ushindani wa kibiashara shirika lake licha ya kufanya kazi zake Zanzibar lakini pia  limeweza kujitanua kwa kufungua ofisi zaidi katika kanda za Pwani- Dar es salaam, Arusha, Mwanza, mbeya, Dodoma na Mtwara.
Naye akitoa Taarifa ya maendeleo ya Matawi ya Benki ya Watu wa Zanzibar yaliyopo Kariakoo na Lumumba Mjini  Dar es salaam Meneja wa Tawi la Kariakoo Badru Idd  alisema PBZ ilipanga kuwafuata wateja wake waliopo na wanaokwenda Tanzania Bara kikazi, kibiashara, kimasomo na wanaopita ambao wanahitaji huduma za Kibenki.
Meneja Badru alisema pamoja na kuwepo kwa ushindani mkubwa wa kibiashara lakini matawi hayo yameweza kufungua hesabu za wateja mbali mbali na kufikia elfu 8,360 kutoka 3,209 ikiwa ni ongezeko la asilimia 160% .
Alifahamisha kwamba amana za wateja zimekuwa kwa kiwango kizuri na kufikia Shilingi Bilioni 24.58  mwezi agosti mwaka 2013 wakati disemba 31 mwaka 2011 zilikuwa Shilingi Bilioni 3.99 ikiwa ni ongezeko la asilimi 516%.
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikutana na Uongozi wa shirika la Meli na Uwakala Zanzibar Tawi la Dar es salaam na kuwaasa kwamba wana kazi kubwa ya kulihudumia shirika hilo katika mazingira ya uwajibikaji.
Balozi Seif alisema shirika hilo linaweza kupoteza imani ya wateja kwa kufikia hatua ya kukata tamaa endapo uendeshaji wa taasisi hiyo hautakuwa wa kiwango na uhakika.
Shirika la Meli na uwakala limeasisiwa mwaka 1978 likiwa na Meli sita zikiwemo mbili zilizorithiwa kutoka ukoloni ambazo zilikuwa zikitoa huduma katika mwambao wa Afrika ya mashariki kuanzia Mtwara Tanzania, Zanzibar, Tanga hadi Mombasa Nchini Kenya.
Mapema mchana Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } ambapo aliushauri uongozi wa shirika hilo kuanzisha utaratibu wa kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuwapatia bidhaa zinazozalishwa Tanzania Bara kwa bei nafuu.
Balozi Seif alisema utaratibu huo unaweza kutoa fursa zaidi ya kuongeza kipato cha wafanyabiashara hao ambao wengi hawana uwezo wa kufuatilia bidhaa hizo katika maeneo mbali mbali ya mIkoa ya Tanzania Bara.
Akitoa Taarifa fupi Naibu Mkurugenzi muendeshaji wa shirika la Taifa la Biashara Zanzibar { ZSTC } Suleiman Juma Jongo alisema lisha ya shirika hilo lililoasisiwa katika miaka ya 70 kuendesha shughuli za ununuzi na uuzaji wa karafuu lakini bado lina fursa ya  kuendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
 
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/8/2013.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika ziara yake katika Taasisi za SMZ zilizopo Mjini Dar es salaam.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Mkurugenzi wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dar es salaam Shumbana Taufiq kabla ya kuanza ziara yake katika Taasisi za SMZ zilizopo Mjini Dar es salaam.
 Kulia yao ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Issa Mlingoti.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisaini kitabu cha wageni mara alipowasili katika jengo la Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar liliopo Mjini Dar es salaam akikaribishwa na Mkurugenzi wa Ofisi hiyo  Shumbana Taifiq.

 Balozi Seif akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha ZBC Dar Msangu Said Mohammed alipotembelea chumbna cha Habari cha Kitengo hicho.
Kulia yake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Issa Mlingoti na Kushoto yake ni Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Hassan Mitawi.
 





















Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Zanzibar Juma Ameir akimuelezea Balozi Seif namna Wizara hiyo inavyojaribu kutatua baadhi ya changa moto wanazopambana nazo  watendaji wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali waliopo Dar es salaam.

Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona changamoto zinazowakabili watendaji wa Ofisi ya Uratibu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliopo Dar es salaam zinashughulikiwa vyema kwa kupatiwa ufumbuzi ili kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara maalum ya kuangalia shughuli za kazi za watendaji wa Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizopo Dar es salaam akianzia na Ofisi ya Uratibu wa shughuli za Serikali.
Ofisi hiyo  iliyopewa mamlaka ya kuratibu uwajibikaji wa Taasisi zote za SMZ zilizopo Mjini Dar es salaam  itakuwa  chini ya Ofisi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Sheni katika baadhi ya Taasisi za Serikali siku moja iliyopita.
Balozi Seif alisema  Serikali iliamua kwa makusudi kuanzisha Ofisi hiyo mnamo mwaka 1986 kwa lengo la kuwa kiunganishi cha upatikanaji wa huduma za kiuchumi kiurahisi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara sambamba na mashirika pamoja na Taasisi za Kimataifa.
Katika  mbinu za kujaribu  kupunguza  matumizi  ya uendeshaji wa Ofisi Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ina nia ya kulipata jengo hilo kwa kuwasiliana na Serikali ya Muungano hata kwa njia ya kubadilishana { Butter system } jambo ambalo gharama zinazotumika hivi sasa zinaweza kusaidia masuala mengine.
Akizungumzia Kitengo cha Habari kilichojumuisha Magazeti ya Serika { Zanzibar Leo }, shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } na Habari Maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wana Habari hao kwa umahiri wao wa kufanya kazi licha ya kuzunguukwa na mazingira magumu ya kikazi likiwemo tatizo la usafiri .
Aliuagiza Uongozi wa Taasisi hizo kufanya utaratibu wa kuandika mapendekezo  ya vile vifaa muhimu zaidi  vya mwanzo na kuyawasilisha Serikalini ili kuangalia namna ya kusaidia uwezeshaji.
Balozi Seif alisema kutokana na mabadiliko ya haraka na ya kila wakati katika sekta ya Habari, watendaji wake wanalazimika nao muda wote waende na wakati.
“ Kwa vile Serikali Kuu tumeshaamua Sekta zetu za Habari zijiendeshe kibiashara. Sasa Baraza letu la Wawakilishi kuanzia mwezi Oktoba katika vikao vijavyo litalazimika kulipa matangazo ya moja kwa moja ya vituo vya Habari vya  ZBC Redio na Tv “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliuagiza Uongozi wa Sekta ya Habari kufanya utafiti utakaofahamu tatizo linalosababisha matangazo ya ZBC Redio na Televisheni kutopatikana katika maeneo ya Tanzania Bara.
“Mimi nilikuwa msikilizaji mkubwa wa Vipindi vya Redio hasa kile cha kutoka magazetini hakinipiti ninapokuwa Dar pamoja na matangazo ya ZBC TV. Hata nikiwa Dodoma Matangazo ya Redio nilikuwa nikiyapa lakini sasa yote yamekatika siju kwa nini? “ Aliuliza Balozi Seif.
Mapema Mkurugenzi wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dar es salaam Shumbana Taufiq alisema Taasisi hiyo ambayo ni kiunganishi muhimu cha mawasiliano kati ya Zanzibar na Mashirika na Taasisi za Kimataifa imekuwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yake kutokana na tatizo la kutoingiziwa fedha kwa wakati.
Mkurugenzi Shumbana alisema gharama za kupanda kwa maisha hasa katika Jiji la Dar es salaam kumewafanya watendaji hao kuishi katika maisha ya kubahatisha suala ambalo hupunguza ari na moyo wa uwajibikaji.
“ Wakati mwengine sisi wasimamizi tunakuwa katika hali ya unyonge wakati hata zile fedha za pencheni kwa wafanyakazi wastaafu zinachelewakutufikia na matokeo yake kuleta malalamiko kwa wazee wetu hao waliopo hapa Dar “. Alifafanua Mkurugenzi Shumbana.
Nao baadhi ya watendaji wa taasisi hizo wakiwemo viongozi wao wa Wizara na Idara wamezitaja baadhi ya changa moto zinazokwaza utekelezaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kazi, usafiri pamoja na kuomba kuongezewa posho ili kukidhi mahitaji.
Awali  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizitembelea Ofisi ya Idara ya Uratibu, Kitengo cha Utawala na Rasilmali Watu, uratibu wa misaada na Mipango pamoja na ile ya wana Habari.
 
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/8/2013.

Monday, 19 August 2013

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi,pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein katika Kikao cha siku moja cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu CCM Taifa

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapiunduzi,pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein,akisalimiana na Viongozi wa Chama alipowasili katika viwanja vya
Ofisi ya CCM Kisiwandui, kushiriki katika Kikao cha siku moja cha
Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu CCM Taifa,kilichofanyika leo Mjini
Zanzibar.{Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapiunduzi,pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein,akiendesha Mkutano wa Siku Moja wa Kamati Maalum ya Halmashauri
Kuu ya Taifa CCM,katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya CCM Kisiwandui
Mjini Zanzibar.{Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
 Baadhi ya wajumbe wa Kikao cha siku moja cha Kamati
Maalum ya Halmashauri Kuu CCM Taifa,kilichofanyika leo Mjini
Zanzibar,wakifuatilia kwa makini mada wakati kikao hicho kikiendelea
chini Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapiunduzi,pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed
Shein,(hayupo pichani)
























Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya
Halamashauri Kuu ya CCM Taifa NEC,wakiwa tayari kuweka kumbu kumbu ya
michango mbali mbali itakayotolea kufuatia mada zitakazotolewa katika
Kikao cha siku moja chini ya mwenyekiti wake  Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi,pia Makamo Mwenyekiti wa CCM
Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein

Sunday, 18 August 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Chen Qiiman Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar Chen Qiiman Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Chen anakaribia kumaliza muda wa utumishi wake wa Ubalozi wa miaka miwili na nusu hapa Zanzibar.





























Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar  akipokea zawadi wa mlango kutyoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kama ishara ya kufunguliwa mlango wa kuingia Zanzibar wakati wowote licha ya kwamba anamaliza muda wake wa utumishi hapa Nchini.


Press Release:-
Zanzibar itaendelea kuwa mshirika mkubwa na Jamuhuri ya Watu wa China katika kuungwa mkono kwake kwenye harakati za kujiletea maendeleo ya Kiuchumi, kibiashara  sambamba na ustawi wa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisi kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Chen Qiiman anayekaribia kumaliza muda wake wa utumishi hapa Nchini.
Balozi Seif ameipongeza Serikali ya China kupitia Balozi wake mdogo hapa Zanzibar kwa juhudi zake za kuunga mkono na kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar.
Alisema Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa mfano katika jitihada za kuunga mkono nchi changa duniani asilimia kubwa ikiwa nchi zilizomo ndani ya Bara la Afrika katika kusaidia taaluma kwenye masuala ya utawala, Uchumi na Maendeleo.
Balozi Seif alitolea mfano wa jitihada hizo za china hasa hapa Zanzibar kuwa  ni ule wingi wa miradi ya maendeleo pamoja na majengo tofauti ya Ofisi za umma yanayoendelea kujengwa na wahandisi mbali mbali wa Makampuni ya China.
“ Miradi ya elimu iliyofadhiliwa na China hapa Zanzibar katika ujenzi wa skuli za sekondari mbili na nyengine moja ikiwa katika hatua za kukamilika Unguja na Pemba samba mba na zile Yuan Milioni 1,000,000 za China zilizonunuliwa madeski 400 ni ushahidi wa wazi wa jinsi nchi hiyo ilivyoamua kwa dhati kuunga mkono nchi rafiki “. Alifafanua Balozi Seif.
“ Msaada huu wa wenzetu wa China umetuwezesha kupunguza tatizo la madeski ambapo bado Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa vikalio maskulini vipatavyo 25,000 Unguja na Pemba “. Alisisitiza Balozi Seif.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba China kuangalia uwezekano wa Makampuni ya Nchi hiyo  kufikiria kuwekeza tena katika sekta ya viwanda hapa Zanzibar.
Alisema China ilikuwa nchi ya mwanzo kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa kuwekeza viwanda mbali mbali vilivyosaidia uchumi wa Zanzibar.
Balozi Seif alifahamisha kwamba viwanda hivyo mbali ya mapato ya serikali lakini pia vilichangia kutoa ajira kwa kundi kubwa la wananachi wa Zanzibar hasa Vijana.
“ Vijana wetu wengi walikuwa na ajira za kuendesha maisha yao kupitia miradi kadhaa ya viwanda vilivyoanzishwa na marafiki zetu wa china kama vile kiwanda cha sukari, mahonda, ngozi na viatu Mtoni na kile cha sigareti Maruhubi lakini vyote hivi sasa vimekufa na kuongeza wimbi kubwa la watu wasio na ajira “. Alifafanua Balozi Seif.
Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Chen Qiiman alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Nchi yake itaendelea kutoa fursa za masomo katika fani mbali mbali sambamba na kusaidia miradi ya maendeleo hapa Nchini.
Alifahamisha kuwa Wazanzibar wapatao 700 tayari wameshapata mafunzo ya muda mfupi, muda mrefu na semina mbali mbali ndani ya kipindi cha miaka miwili Nchini China kitendo ambacho kitazidisha kasi ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Balozi Chen Qiiman alisema licha ya kumaliza muda wake wa utumishi lakini Nchi hiyo kupitia uongozi mwengine utakaosimamia shughuli za Diplomasia hapa nchini bado unafikiria njia zaidi za kusaidia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar.
Alieleza kwamba ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Shein Nchini China katika miezi ya hivi karibuni imechangia kuamsha ari ya makampuni mengi nchini humo kutaka kuwekeza vitega uchumi vyao Zanzibar.
Balozi Chen alisisitiza kwamba ujumbe wa Viongozi na wataalamu 20 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China unatarajiwa kuwasili Zanzibar mwishoni mwa mwezi huu kuangalia uwezekano wa kutaka kuwekeza katika sekta za Uvuvi na Utalii hapa Zanzibar.
Balozi huyo mdogo wa China aliyepo hapa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na  kwamba miradi ya Zanzibar  iliyopata msaada na ufadhili wa Jamuhuri ya Watuy wa China na kuisimamia yeye na watendaji wake mingi imemalizika kwa wakati na ufanisi mkubwa.
Hata hivyo Balozi Chen Qiiman alisema ana matumaini makubwa kwa balozi mwenzake mpya atakayekuja kushika wadhifa huana muelekeo wa kusimamia vyema na kufikia hatua ya kukamilika kwa miradi hiyo.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/8/2013.

Tuesday, 13 August 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa 31 wa siku Tano wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika { AEAA } unaofanyika katika Ukumbi wa Victoria wa Hoteli ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.

 Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano huo iliyotolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa 31 ya Kimataifa wa Tathmini ya Elimu ya Afrika unaofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto Mkoani Arusha.


 Balozi Seif akiangalia maonyesho na kupata maelezo ya mfumo wa utayarishaji wa mitihani na vyeti kutoka kwa wataalamu wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika mara baada ya kuufungua mkutano wa Jumuiya hiyo Mkoani Arusha.



























Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiagana na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika Dr. Joyce Ndalichako mara baada ya kuufungua Mkutano wa Jumuiya hiyo.

Press Relese:-
Mataifa ya Bara la Afrika yana wajibu wa kuhakikisha kwamba Elimu inayotolewa na kufundishwa katika Taasisi zote za Elimu Barani humu inakuwa bora na kumnufaisha vilivyo Mtoto wa Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiufungua Mkutano wa 31 wa siku Tano wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika { AEAA } unaofanyika katika Ukumbi wa Victoria wa Hoteli ya Ngurdoto iliyopo Mkoani Arusha Tanzania.
Balozi Seif aliwaambia washiriki wa Mkutano huo kutoka Nchi 28 Barani Afrika sambamba na wadau wa Elimu wa Nchi washirika Duniani kwamba Serikali za mataifa hayo wanachama ziangalie njia muwafaka katika kuona hadhi na ubora wa elimu inaendelea kupatikana kwenye mataifa yao.
Alisema mara nyingi wananchi na hasa wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakilalamikia kushuka kwa kiwango cha elimu suala ambalo linafaa kuchukuliwa hatua za ziada katika kupatikana kwa vifaa ambavyo ndivyo vinavyochangia kupunguza ubora wa elimu.
Alisema hivi sasa kiwango cha elimu kinaonekana kuchuka kinachochangiwa na ukosefu wa vifaa vya sayansi jambo ambalo linahitaji mazingatio makubwa katika mabadiliko ya viwango bora vya elimu.
Balozi Seif alieleza kuwa Mkutano huo wa Tathmini ya Elimu ya Afrika umekuja muda muwafaka kwa wanachama hao katika kubadilisha uzoefu wa tathmini ya elimu ambapo utasaidia kujenga nguvu za pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Barani Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba elimu ndio uti wa mgongo wa maendeleo popote pale duniani, hivyo jitihada za ziada zinapaswa kuchukuliwa katika kuona eneo hilo linajengewa mazingira mazuri na ya uhakika.
“ Na matumaini makubwa kwenu washiriki wa Mkutano huu wa Tathmini ya Elimu ya Afrika kwamba mtatumia fursa na nafasi ya mkutano huu kuondoka na wazo litakalosaidia kuimarika kwa ubora wa elimu Barani Afrika ”. Alifafanua Balozi Seif.
Aliwakumbusha wajumbe wa Mkutano huo kuelewa kwamba Mataifa ya Afrika yamejikubalisha kuimarisha Mpango wa Elimu kwa wote na Malengo ya Milenia hadi ifikapo mwaka 2015 ikiwa ni hatua inaozitaka nchi hizo kufikia.
Hata hivyo Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa kukabiliana na tatizo la kuvuja kwa mitihani ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangia kushuka kwa kiwango cha elimu katika mataifa mengi dunia likiwemo Bara la Afrika.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano wa mpango wa uimarishaji wa elimu unaofuatwa Zanzibar unaofuatwa kuanzia Maandalizi,Msingi, Sekondari hadi chuo Vyuo Vikuu unaweza kusaidia katika baadhi ya Mataifa ya Afrika endapo utafanyiwa utafiti na Jumuiya hiyo ya Tathmini ya Elimu ya Afrika.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika     { AEAA } Dr. Joyce Lazaro Ndalichako alisema lengo la Mkutano huo ni kuangalia njia bora za kuimarisha hadhi ya Elimu katika Mataifa wanachama wa { AEAA }.
Dr. Joyce alisema kwamba Jumuiya yake imekuwa ikitumia njia kadhaa ikiwemo kuwashirikisha wataalamu sambamba na Kamati za Utafiti ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa vyema.
Alisema upo utaratibu wa kubadilishana vipindi na uzoefu katika utunzi wa mitihani kwa hatua ya kujenga nguvu za pamoja za kuimarisha kiwango cha elimu Barani Afrika.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano huo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Phillip Mulugo alisema wakati umefika kwa Taasisi za elimu kuhakikisha ongezeko la Maskuli popote pale linakwenda sambamba na ubora wa elimu.
Mh. Mulugo alifahamisha kwamba mfumo huo ukitekelezwa kwa pamoja unaweza kusaidia kupata wataalamu wenye kiwango kinachokubalika vyema kitaifa na Kimataifa.
Mkutano huo wa 31 wa Kimataifa wa Jumuiya ya Tathmini ya Elimu ya Afrika uliojumuisha washiriki wa Mataifa 28 ya Bara la Afrika umehudhuriwa pia na wadau wa Elimu kutoka mataifa zaidi ya kumi Duniani zikiwemo Uingereza,Marekani, India, China na Ujerumani.



Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
12/8/2013.


Sunday, 11 August 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akielezea jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyosikitishwa na Kitendo cha raia wawili wa Uingereza Katie Gee na Kisty Trup cha kumwagiwa tindikali { Acid } na watu wasiojuilikana katika maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

 Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, Kulia yake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed wakiambatana na Bamalozi wa heshima wa Uingereza, Ujerumani an Marekani waliopo hapa Zanzibar























Kikao hicho cha dharura kilifanyika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar na kushuhudia pia na baadhi ya Viongozi wa Jumuia za utembezaji watalii za hapa Zanzibar ZATO na ZATI.


Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kitendo kibaya na kiovu walichofanyiwa raia wawili wa kike wa Uingereza Katie Gee na Kisty Trup cha kumwagiwa Tindi kali  { Acid } mapema jana usiku katika maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Raia hao wawili wa Uingereza ambao wamekuja Nchini Tanzania kwa kazi za kujitolea wakiwa hapa Zanzibar kwa matembezi ya wiki wamejeruhiwa katika sehemu zao za uso na vifua na watu ambao mpaka sasa bado hawajajuilikana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Mabalozi wadogo wa Heshima wa Uingereza, Ujerumani na Marekani waliopo hapa Zanzibar walioambatana na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Utalii na Michezo pamoja na Jumuia zinazojihusisha na utembezaji watalii za ZATO NA ZATI.
Balozi Seif alisema kwa kuwa hilo sio tukio la bahati mbaya kufanya hivyo amewaomba wananchi popote pale walipo kujaribu kusaidia kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi mara tuu watakapoona dalili za watu waliohusika na vitendo hivyo.
Alifahamisha kwamba Zanzibar ni moja ya Nchi inayosemwa vizuri katika Nyanja za Kimataifa, lakini kwa mfumo huu uliojichomoza unaofanywa na baadhi ya watu wachache wasioeleweka malengo yao unaweza kukatisha tamaa kwa wale wageni waliojipangia kutaka kutemebelea Zanzibar.
“ Ipo kumbu kumbu hapo nyuma na nyengine si ya muda mrefu ya matukio ya baadhi ya watu kumwagiwa tindi kali { Acid } lakini hichi cha wageni hawa waliokuwa kujitolea hapa Nchini kimewafanya kupewa adhabu wasiyostahiki “. Alielezea Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewahakikishia Mabalozi hao wadogo wa Heshima hapa Zanzibar wa Uingereza, Ujerumani na Marekani kwamba Serikali kwa kushirikiana na Vyombo vya ulinzi kwa msaada wa Wananchi itafanya uchunguzi na kuhakikisha wahusika wa kitendo hicho wanatiwa nguvuni ili kupelekwa katika vyombo vya sheria.
Mapema Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema Vijana hao wa kujitolea kutoka Uingereza Katie Gee na Kisty Trup walipatia huduma ya kwanza katika Hoteli ya Tembo iliyopo Forodhani chini ya usimamizi wa Dr. Saleh Mohammed Jidawi Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
Alisema tukio hilo la tindikali linaloonekana kutumiwa na baadhi ya wakorofi kama sialaha kwa kuwaathiri watu wasio na hatia limeleta athari kubwa na kutia doa katika sekta ya Uchumi.
Waziri Mbarouk alimpongeza Balozi wa Heshima wa Uingereza hapa Zanzibar  Balozi Carll Salisbury kwa hatua zake za kutoa usafiri wa Ndege ili kusafirishwa kwa vijana hao ili kuendelea kupatiwa  matibabu zaidi Mjini Dar es salaam na baadae Nchini mwao.
Wakichangia katika kikao hicho  Ofisa wa Ubalozi wa Marekani hapa Zanzibar  Jefferson Smith na Balozi wa Heshima wa Uingereza hapa Zanzibar Carll Salisburg walisema Serikali ni vyema ikawa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wakati yanapotokea matukio yasio ya kawaida ndani ya Jamii.
Nao wawakilishi wa jumuiya za watembezaji watalii hapa Zanzibar wameiomba Serikali kutenga fungu maalum kwa ajili ya kuviunga mkono vyombo vya ulinzi katika kukabiliana na matukio yanayoashiria kutaka kuvunja amani na kuhatarisha maisha ya Jamii.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed ameiasa jamii kujenga tabia ya kuchukia jambo lolote baya lionaloonekana kujichomoza miongoni mwao katika maeneo wanayoishi.
Waziri Aboud alieleza kwamba mazingira yaliyopo mitaani hivi sasa yamejidhihirisha wazi kuwa wapo baadhi ya watu wanaoshabikia matendo maovu yanayofanyika katika sehemu zao ambayo wanaelewa wazi kuwa hatma ya matendo hayo hufikia hatua ya kuwaathiri hata wao wenyewe.
 
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/8/2013.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasilisha salamu za pole kwa Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso kufuatia uwanja wa ndege wa Kimataifa wan chi hiyo kukum bwa na Moto.


Pembeni yao kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed.

 Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mutinda Mutiso akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kamusi ya Kiingereza kwa Kiswahili aliyoitunga kwa ajili ya kukuza lugha hiyo pamoja na kusaidia wana diplomasia.























Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Balozi wa Kenya Nchini Tanzania anayemaliza muda wake wa utumishi wa miaka minne zawadi ya kasha kama kumbu kumbu ya kuwepo kwake Nchini.


Press release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa pole kwa Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya kutokana na maafa ya moto mkubwa uliokikumba Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyata Kiliopo Mjini Nairobi Nchini humo na kusababisha hasara kubwa ambayo bado haijajuilikana.
Moto huo umesabisha safari zote za ndege zilizopangwa kuingia na kutoka kwenye uwanja huo kusitishwa na kupelekea ndege hizo kutua katika viwanja vyengine vya ndege vya Eldoret, Mombasa na Nchi jirani za Afrika Mashariki.
Pole hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipofanya mazungumao na Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso aliyefika kumuaga hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kumaliza muda wa utumishi wake wa miaka minne hapa Nchini.
Balozi Seif alisema Wananchi wa kenya wamekumbwa na maafa hayo yaliyosababisha kutishia kutetereka kwa uchumi wake unaotegemea kwa kiasi kikubwa huduma zinazotolewa na Uwanja huo katika ukanda mzima wa Bara la Afrika ukiunganisha ndegembali mbali  za Kimataifa.
Alisema gharama za kuufanyia matengenezo uwanja huo ni kubwa kufuatia moto huo uliotokea mapema  alfajiri ya Jumatano katika eneo la kuwasili abiria kabla ya kusambaa hadi maeneo mengine likiwemo lile la Idara ya Uhamiaji.
Alifahamisha kwamba umefika wakati kwa Waafrika kuwa makini na vitendo vya kuwatia hofu wananchi { Ugaidi } ambavyo vinaweza kusababisha ukosefu wa utulivu na amani miongoni mwa Jamii.
Alimueleza Balozi Huyo wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania kwamba Vitendo vya Kigaidi vinavyoonekana kujitokeza katika Nchi mbali mbali Duniani vikilikumba pia Bara la Afrika humfanya Mtu aishi katika maisha ya hofu na wasi wasi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi huyo wa Kenya Nchini Tanzania kwa juhudi zake za utumishi zilizochangia kuimarika  zaidi kwa uhusiano wa kudugu uliopo kati ya Kenya na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Balozi Seif alisema Wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hasa wale wanaoishi katika ukanda wa Pwani ya Mwambao wa Afrika Mashariki wamekuwa na uhusiano wa karibu na kidugu na wenzao wa Taifa la Kenya.
Alishauri uhusiano huo ukazidi kuimarishwa kwa faida ya wananachi wa pande hizo mbili hasa kwa kuzingatia zaidi muingiliano uliopo kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki iliyounganisha harakati za kiuchumi za mataifa wanachama.
Mapema Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi Mutinda Mutiso alisema upo umuhimu wa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuikuza na kuithamini Lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuipa heshima yake Kimataifa.
Balozi Mutiso alisema inasikitisha kuona wenye Lugha ya Kiswahili wanaendelea kusua sua wakati lugha yenyewe kimataifa inazungumzwa takriban na watu zaidi ya Milioni mia mbili na arubaini duniani kote ikiwa lugha ya nne kwa ukubwa duniani hivi sasa.
“ Takwimu za watu wanaozungumza Kiswahili Duniani ndizo zilizonishawishi mimi kufikia uwamuzi wa kutunga Kamusi la Kingereza kwa Kiswahili kupitia mfumo wa Kidiplomasia ili kutoa mchango wangu katika kukuza lugha yetu ya Afrika Mashariki. Mchango wangu huu pia nimekusudia uwasaidie wanadiplomasia wenzangu “. Alifafanua Balozi Mutinda.
Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao hivi sasa unapita katika hatua ya Rasimu ya Katiba hiyo Balozi Mutinda Mutiso ameipongeza Tanzania kwa hatua yake hiyo yenye muelekeo wa kutandika Demokrasia zaidi.
Balozi Mutinda alisema Waafrika walio wengi wanatarajia kukiona kipindi cha mpito  cha kuelekea kwenye Katiba Mpya Nchini Tanzania kinakuwa kigezo na mfano bora wa kuigwa na kuungwa mkono na Mataifa mbali mbali ya Bara la Afrika.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyoamua kufuata mfumo wa Umoja wa Kitaifa ambao umeleta utulivu, amani na umoja miongoni mwa Wazanzibari walio wengi baada ya mgongano wa mrefu wa kisiasa uliovikumba vyama vikuu viwili vya kisiasa.
Balozi Mutinda alisema inapendeza kuona Zanzibar hivi sasa imetulia kisiasa kwa kuwa na mfumo huo wa Serikali ya pamoja unaofaa kupongezwa na kuigwa na Mataifa mengine yanayotaka kuelekea kwenye demokrasia zaidi ndani na nje ya Bara la Afrika.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/8/2013.


Mabunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na baadhi ya Viongozi na Wananchi wa Jimbo la Kitope mara baada ya kula chakula cha mchana baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.


 Baadhi ya Viongozi na Wananchi wa Jimbo la Kitope wakimsikiliza Mbunge wao Balozi Seif hayupo pichani baada ya kula chakula cha pamoja mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
























  Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe isingependa kuona usalama na amani   ya Nchi inapotea kwa kuachwa kuchezewa na baadhi ya watu kwa maslahi yao wakishindwa kuelewa kuwa  ni hazina kubwa kwa Taifa zima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope alitoa kauli hiyo mara baada ya kujumuika katika chakula cha pamoja kati yake Familia yake na baadhi ya Wananchi na Viongozi wa Jimbo la Kitope.
Hafla hiyo iliyoshirikisha pia baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wa Wilaya ya Kaskazini “ B “ ilifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbno la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kasakazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif alisema zipo nchi nyingi duniani akazitolea mfano Misri na Syriya ambazo ndani ya siku kuu hii ya Iddi el fitri iliyokuja baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa zimezunguukwa na mitutu ya bunduki  iliyotanda kuimeza amani waliyokuwa nayo kabla.
“ Ukiipoteza amani ya nchi  sharti uelewe kwamba ni tabu na kuirejesha kwake tena inataka kazi kubwa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliitahadharisha Jamii kuwa macho na baadhi ya watu wanaojaribu kuwashawishi wananchi  hasa vijana kupitia misingi ya Dini kuchochea uvunjifu wa amani na utulivu uliopo Nchini.
Balozi Seif amewashukuru wananchi waliojaribu kushawishiwa kujiingiza ndani ya shari katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa msimamo wao usiyoyumba wa kukataa shari hiyo.
Amewaomba wananchi na hasa waumini wa Dini tofauti nchini kutokubali maeneo yao kuchezewa kwa kuoteshwa mbegu mbovu za chuki, uhasama pamoja na shari.
Balolzi Seif aliwakumbusha Vijana kuwa makini katika kujiepusha kutumiwa katika kufanya fujo na maovu kwani kila siku mwanaadamu anapenda kuwa katika mambo mema ikiwemo suala la amani ambalo ndilo la msingi mkuu kuliko yote.
Naye Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwaasa wazazi kuwa na  hadhari na watoto wao ndani kipindi hichi wakati  watoto hao wanapoelekea kwenye viwanja vya siku kuu.
Kwa upande wake Katibu Mpya wa Chama cha Mapinduzi  Wilaya ya Kaskazini  “ B” Subira Mohd Ameir alikipongeza kitendo cha Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif cha kuwa karibu na wananchi wake kwani huleta faraja.
Mapema Balozi Seif akitoa nasaha kwa waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kitope amehimiza suala la kuendelezwa kwa  ushirikiano ili kuleta upendo miongoni mwa waumini hao.
Balozi Seif alifahamisha kwamba ushirikiano  umekuwa ukisisitizwa kila wakati na kuelezwa ndani ya vitabu vya dini, hivyo waumini hao wanastahiki kuuheshimu na kuufuata.
Siku Kuu ya Iddi El Fitri imekuja kufuatia kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao ni  wa Nne katika nguzo tano za Kiislamu ikifuatiwa na Ile ya Hijja kwa muumini mwenye uwezo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/8/2013.