Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiingia kuatika mabanda ya maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya saba saba Jijini Dar es salaam akiambatana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed.
Balozi Seif akiangalia sabuni safi ya mapande ya kufulia iliyotengenezwa na Kiwanda cha Star Natural Product chini ya utaalamu wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo { SIDO }.
Mtaalamu wa dawa za asili za miti shamba kutoka Meli Nne Herbal Producti Zanzibar Bibi Salma Othman akimpatia maelezo Balozi Seif juu ya utengenezaji wa biadhaa zao kwa kutumia miti ya asili.
Nyuma ya Balozi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Waziri wa Viwanda na Biashara wa SMT Mh. Abdulla Kigoda.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiangalia viatu vya makubadhi vilivyotengenezwa na Saccos ya Nia Safi Women kutoka chake chake Kisiwani Pemba.
Msimamizi muandamizi wa mauzo katika banda la vifaa vya mawasiliano vya kampuni ya Sam Sung Bwana Dionis Ezekiel Mboya akimuonyesha balozi Seif teknolojia ya hali ya juu inayopatikana katika seti za Televisheni kwa kutumia ishara ya mkono au kidole bila ya kugusa.
Mwakilishi wa Kampuni ya Poly Machinery Co. LTD kutoka Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Even Mao akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya mashine zilizotengenezwa na kampuni hiyo jinsi zinavyofanya kazi.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo vidogo Nchini Tanzania { SIDO } limepongezwa kwa hatua yake iliyochukuwa ya kuwajengea mazingira bora ya miundo mbinu Wananchi katika upatikanaji wa vitendea kazi vyenye viwango vinavyowawezesha wakulima Nchini kumudu kuzalisha kitaalamu zaidi.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuyatembelea Mabanda mbali mbali yaliyopo kwenye maonyesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif alisema Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo vidogo { SIDO } limejikita zaidi katika kusaidia jamii hasa wananchi wanaojishughulisha na kilimo jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limeleta faraja na kuelekea kwenye njia ya kumkomboa mwananchi wa kipato cha chini.
Akionyesha furaha yake Balozi Seif alieleza kwamba yapo mambo ya kushangaza katika mabanda ya maonyesho ambayo yamefanywa na wananchi wenyewe wazalendo bila ya kushirikishwa wataalamu wa nje ya nchi kwa kutumia Teknolojia ya hapa hapa nchini.
“ Nimefurahishwa sana kutokana na vitu vingi nilivyovishuhudia katika mabanda haya ya maonyesho niliyoyatembelea. Ukweli halisi huwezi kufikiria kama bidhaa nilizoziona zimetengenezwa hapa nchini kutokana na ubora wake “. Alisistiza Balozi Seif.
Aliwaomba wajasiri amali mbali mbali wanaoshiriki katika maonyesho hayo kuhakikisha kwamba wanatumia fursawaliyoipata eneo hilo kutokanana na ushiriki wao kwenye maonyesho hayo kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye kiwango ili kujijengea soko la uhakika ndani na nje ya Nchi.
Mapema Meneja mauzo wa Shirika la kuhudumia Viwanda vidogo vidogo { SIDO } Henric Mdede alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Taasisi yake imekuwa ikitengeneza vifaa tofauti vya uzalishaji kulingana na mahitaji ya wananchi wa kipato cha kawaida.
Alisema utaratibu huo Umekusudiwa kutoa fursa kubwa zaidi kwa wazalishaji wadogo wadogo hasa wale walioamua kujiunga katika Muungano wa wazalishaji katika mfumo.
Naye mwakilishi wa Kampuni ya Poly Machinery co. LTD kutoka Jamuhuri ya Watu wa China ambayo imeshiriki katika maonyesho hayo ya saba saba Bwana Even Mao alisema Kampuni yao imefikia uwamuzi wa kuwekeza vitega uchumi vyao Nchini Tanzania kutokana na mazingira mazuri yaliyopo.
Bwana Even Mao alisema Tanzania nimebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ya ardhi ambayo ikitumiwa vyema inaweza kuchangia mapato ya Taifa pamoja na kuimarisha sekta ya kilimo ambayo ndio inayochukuwa asilimia kubwa ya wananchi wake kujishughulisha na Kilimo.
“ Ukweli sisi kampuni yetu tumelazimika kufungua tawi letu hapa kufuatia Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi ya kilimo “. Alisikika Bwana Even Mao akitamka maneno hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika ziara hiyo alifanikiwa kuyatembelea mabanda ya maonyesho ya shirika la kuhudumia Viwanda vidogo vidogo { SIDO }, wajasiri amali wa bidhaa mbali mbali za vyakula vikavu ,viungo, uchongaji pamoja na fani ya ufumaji vya Bara na Zanzibar.
Nyengine ni vifaa vya kisasa vya mawasiliano vinavyotengenezwa na kampuni ya Sam Sung pamoja na mashine tofauti za kuhudumia bidhaa za kilimo zikiwemo pia zile za kutotolea vifaranga vya kuku na kukobolea vyakula vya nafaka.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/7/2013.
No comments:
Post a Comment