Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amekemea tabia ya baadhi ya Viongozi
wa Chama hicho kuwa na hulka ya kuwatenga Vijana ambao ndio muhimili na wenye
nguvu katika kukipigania Chama hicho.
Kauli hiyo aliitoa katika Ukumbi wa
Jamuhuri Wete Pemba wakati akizungumza na vijana wa Chama cha Mapinduzi wa
kikundi cha Hatudanganyiki mara baada ya kupokea malalamiko yao dhidi ya baadhi
ya Viongozi wa Chama hicho Wilaya ya Wete na Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alisema zipo kasoro ndogo ndogo zinazotofautiana za
mawazo zilizopo baina ya Viongozi na Wanachama lakini haziwezi kuachwa zinaendelea kudhoofisha nguvu
za Chama hicho.
Aliwaasa wana CCM hao kujiepusha na
mgawanyiko ndani ya chama ambao unaweza kuleta balaa na kitu kinachowakabili
hivi sasa mbele yao ni kuhakikisha
wanapanga mikakati katika kuimarisha nguvu ya chama chao kwa ajili ya ushindi
wa mwaka 2015.
Alitahadharisha kwamba hitilafu
zinazojichomoza baina ya Viongozi na Wanachama wa chama hicho ni vyema
zikatatuliwa na kuishia katika Vikao vya halali na kujiepusha na tabia ya
kuitana majina ya ajabu ambayo hutoa mwanya wa kudhoofisha chama.
Balozi Seif alielezea kuunga mkono vijana hao wa CCM wa kundi la hatudanganyiki
Kaskazini Pemba kwa ushujaa wao wa kutetea na kuimarisha Chama cha Mapinduzi na
Kuuagiza Uongozi wa CCM Wilaya ya Wete pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba
kufuatilia matatizo yanayowakabili Vijana hao na hatimae kuyatatua nay ale
wasio na uwezo nayo kuyawasilisha kwa Uongozi wa Juu wa Chama.
“ Mimi kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambae pia nasimamia shughuli za Serikali ya
Chama Tawala nitahakikisha baadhi ya matatizo yenu Vijana nayawasilisha kwa
Makamu Mwenyekiti wetu wa CCM Zanzibar ili itafutwe mbinu ya kuyatatua “.
Alisisitiza Balozi Seif.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwapongeza wana CCM Kisiwani Pemba kwa
msimamo wao wa kuendelea kukiunga mkono chama hicho.
Alisema Wanachama wa chama hicho
Kisiwani humo ni madhubuti kutokana na kutoyumba kwao licha ya mikiki mikiki
wanayopambana nayo kutoka kwa kambi ya upinzani hasa katika nyakati za
uchaguzi.
“ Ushindi wa Chama cha Mapinduzi
katika uchaguzi Mkuu unategemea sana wana CCM wa upande wa Kisiwa cha Pemba
ambao hawatetereki wala kuyumba kutokana na vitisho vya upinzani “. Alisisitiza
Balozi Seif.
Balozi Seif aliendelea kufahamisha
kwamba nguvu na uhai wa Chama cha Mapinduzi mara zote unategemea jumuiya zake
za Wazazi, Vijana na UWT, hivyo Vijana
hao wanapaswa kuelewa kwamba wao ni tegemeo la Chama wakati wote.
Mapema Vijana hao wa CCM wa kikundi
cha hatudanganyiki wakiongozwa na Mwenyekiti wao Omar Rashid walielezea
changamoto wanazokabiliana nazo kila siku katika harakati zao za kuimarisha
Chama Cha Mapinduzi.
Walisema asilimia kubwa ya changa
moto hizo ambazo zimo ndani ya uwezo wa Viongozi wenyewe zimekuwa zikiwapa
wakati mgumu kutokana na udhaifu binafsi uliopo kwa baadhi ya Viongozi wa CCM
Wilaya na Mkoa.
Walieleza kwamba upo ushahidi wa wazi
unaoonyesha baadhi ya Viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa kufuja mali za Chama kwa
maslahi yao binafsi pamoja na kujishirirkisha katika vitendo vya rushwa wakati
zinapotokea fursa za ajira kwa ajili ya Vijana hao.
Baadaye Balozi Seif alifika katika
Kijiji cha Michakaeni Chake Chake Pemba kuipa pole Familia ya Mwanaharakati wa
Chama cha Mapinduzi Marehemu Bibi Fatma Omar Khatib ambae aliyefariki dunia hivi
karibuni baada ya kupata ajali ya kugongwa na Gari.
Akiifariji Familia hiyo Balozi Seif aliwataka
ndugu na jamaa wa marehemu Bibi Fatma Omar Khatib kuwa na moyo wa subra katika
kipindi hichi kigumu cha maombolezo.
Alisema msiba huo wa Bibi Fatma ambao
utaendelea kukumbukwa katika kipindi kirefu mbali ya kuiathiri familia hiyo
lakini pia umewagusa takriban wana chama wa chama cha mapinduzi wote waliopata
taarifa ya msiba huo Zanzibar na bara kwa ujumla.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pia alimtembelea Mzee mwanaharakati wa CCM wa miaka mingi Kisiwani
Pemba Bibi Habiba Ali Hamadi hapo nyumbani kwake Mtaa wa Michakaeni.
Bibi Habiba mwenye umri wa Miaka 70
aliwahi kupata ajali ya gari wakati wa kampeni za mwanzo za uchaguzi wa vyama
vingi vya siasa ambapo CCM iliibuka na ushindi kwa kumuwezesha Dr. Salmin Amour
kuiongoza Zanzibar mnamo mwaka 1995.
Balozi Seif alimuahidi Bibi Habiba
ambae hadi sasa ni Balozi wa CCM wa nyumba kumbi kwamba Uongozi wa chama cha
Mapinduzi utakuwa pamoja na yeye kwa
kumpatia misaada kadri hali itakavyoruhusu kutokana na mchango wake mkubwa aliyoitoa
ndani ya chama hicho.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar
28/7/2013.