Tuesday, 30 April 2013


           NMB  YAKABIDHI MSAADA WA MADESKI   SKULI YA  BUMBWINI


Meneja Biashara  kutoka Makao Makuu ya Benki ya Biashara Jijini Dar es salaam Bibi Shilla Sennoro akimkabidhi Mgeni Rasmi Mama Asha Suleiman Iddi Madeski 100 na Viti 100 kwa ajili ya Skuli za Msingi za Bumbwini na Mangapwani hapo skuli ya Msingi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B.



Mama Asha Suleiman Iddi akikabidhi rasmi madeski 100 na Viti 100 kwa uongozi wa Skuli za Bumbwini na Mangapwani ambavyo vimetolewa msaada na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } hapo Skuli ya Msingi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B.







Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Bumbwini na Mangapwani wakifurahia Vikalio vipya vilivyotolewa msaada na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } hapo Skuli ya Msingi Bumbwini.

Picha  na Hassan Issa  (Vuga Newsroom )



 

 Press Release:-

Taasisi za Umma,Mashirika pamoja na Sekta Binafsi zina wajibu wa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali Kuu katika kuwajengea mazingira bora Wananachi wake hasa katika Sekta muhimu ya Elimu yenye dhamana ya kufinyanga   wataalamu na Viongozi wa Baadae.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati wa hafla maalum ya kukabidhi Meza na Viti mia Moja kwa Skuli za Msingi za Bumbwini na Mangapwani iliyofanyika katika Skuli ya Msingi Bumbwini iliyopo Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Msaada huo wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni kumi                           { 10,000,000/- } umetolewa na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } ambapo kila Skuli imebahatika kupata Meza Hamsini na Viti Hamsini.
Mama Asha Suleiman Iddi alisema  nguvu za Serikali pekee kwa sasa haziwezi kukidhi mahitaji ya Wananachi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji miongoni mwa Wananchi na maeneo tofauti hapa Nchini.
Aliipongeza Benki ya Biashara Tanzania { NMB } kwa uamuzi wake wa kusaidia Sekta ya Elimu ambayo ndio muhimili mkubwa wa Maendeleo katika Taifa lolote Ulimwenguni.
Alisisitiza kwamba utekelezaji wa Sera ya Elimu Zanzibar katika kuhakikisha kila mtoto wa Taifa hili anapata Elimu ya lazima umo ndani ya Sera ya Chama cha Mapinduzi iliyopata ridhaa ya Wananchi walio wengi ilipokuwa  ikinadiwa wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkuu uliopita wa Mwaka 2010.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwaomba Wazaliwa na Vijiji hivyo  vya Bumbwini na Mangapwani kusaidia Maendeleo ya Vijiji vyao ili kuunganisha nguvu zao  pamoja na viongozi wao Mbunge na Mwakilishi.
Alishauri kufanywa kwa tathmini ili kujua  mahitaji halisi ya huduma za umeme ili kupata mbinu za  kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo  linalowakabili wananchi wa Mangapwani la ukosefu wa Huduma ya Umeme.
Mapema akitoa Taarifa fupi Meneja wa Biashara kutoka Makao Makuu ya Benki ya NMB Mjini Dar es salaam Bibi  Shilla Sennoro alisema anza ya Benki hiyo hivi sasa ni kuhakikisha inaimarisha huduma zake ili kwenda sambamba na jitihada za Serikali za kuwapatia huduma za kifedha wananchi walio wengi.
Bibi Shilla alieleza kuwa katika kutekeleza jitihada hizo Benki hiyo licha ya kuwa na matawi zaidi ya 145 Nchini kote lakini pia imelenga kuongeza mengine katika Wilaya mpya na maeneo mengine yanayohitaji huduma za kifedha.
Meneja huyo wa Biashara kutoka Makao Makuu ya NMB Jijini Dar es salaam alifahamisha kwamba hatua hiyo imelenga kusaidia wananchi kuokoa muda wao na kuutumia zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Bibi Shilla Sennoro  alisema Taasisi yake kwa kutambua umuhimu wa Jamii na jitihada za Serikali Benki hiyo itaendelea kutoa misaada  kwa jamii katika sekta mbali mbali kadri hali itakavyoruhusu.
Katika Risala yao Wananchi, Walimu na Wanafunzi hao wa Vijiji vya Bumbwini na Mangapwani wameishukuru Benki ya Biashara ya NMB kwa uwamuzi wake wa kusaidia Samani skuli hizo ambazo zipapunguza kero linalowakabili wanafunzi la baadhi yao kukaa chini.
Hata hivyo wananchi, walimu na Wanafunzi hao walisema  bado skuli hizo zinaendelea kukabiliwa na changa moto kadhaa ikiwemo huduma za maji safi, Umeme kwa kijiji cha mangapwani pamoja na uchakavu wa baadhi ya Majengo ya Skuli zao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/4/2013.



No comments:

Post a Comment