Thursday, 2 May 2013

  UFUNGUZI WA WARSHA  YA  MAWASILIANO KUPITIA MFUMO WA TEKNOLOGIA YA KISASA.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifungua warsha ya siku tano kuhusu huduma za mawasiliano vijijini inayofanyika katika hoteli ya Kimataifa ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.



Katibu Mkuu  Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ya Serikali ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuifungua warsha ya Kimataifa ya siku tano ya mawasiliano Vijijini huko ukumbi wa Hoteli ya Melia Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kushoto ya Dr. Florens Martin Turuka ni Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi na Afisa Mkuu wa Mfuko wa wa huduma za Mawasiliano Mhandisi  Peter Ulanga.




Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku tano kuhusu huduma za mawasiliano wanaotoka mataifa 16 Barani Afrika wakiwemo pia Wawakilishi wa Mataifa ya India Malaysia na Marekani.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote kutoka Nchini Uholanzi na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi ya Teknolojia ya SMT mara baada ya kuifungua Warsha ya siku tano ya mawasiliano.
Picha na Hassan Issa wa  -(Vuga  newsroom )-  OMPR – ZNZ.



Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Maendeleo ya haraka yanaweza kupatikana kwa Mataifa Machanga iwapo suala la matumizi ya Mtandao wa kisasa wa Mawasiliano ya Kiteknolojia utapewa msukumo unaostahiki.
Alisema mfumo huo wa Teknolojia unaweza pia kutoa ajira hapo baadaye kwa kuangalia zaidi maeneo ya Vijijini ambayo huduma hizo za mawasiliano hazijafika na mwengine ziko katika kiango hafifu.
Balozi Seif alisema hayo wakati akiifungua warsha ya siku tano kuhusu mawasiliano Vijijini iliyoandaliwa na  Mfuko wa Mawasiliano kwa wote wenye makao makuu yake Nchini Uholanzi, warsha ambayo inafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Kilimo, Biashara na hata  Elimu ni sekta za msingi zinazoweza kuendelezwa kwa kutumia mfumo huo wa Teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serkali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeanza hatua za kufuata mfumo huu ili kutengeneza mazingira bora yatakayowezesha kukuza chumi wa Taifa katika kutumia Taaluma hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea hafaja yake kutokana na warsha hiyo kufanyika Nchini Tanzania, fursa  ambayo itasaidia kuunganisha nguvu za pamoja  katika kukabiliana na changamoto zilizomo kwenye mfumo huo wa mawasiliano.
“ Tumeshuhudia Mataifa kama vile Chile, Uturuki na Malaysia yalivyopiga hatua kubwa na ya haraka katika kuimarisha uchumi wao baada ya kuamua kutumia mfumo huo wa mawasiliano “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo ya mfuko wa mawasiliano kwa wote kufikiria njia zitakazowezesha mawasiliano ya teknolojia ya kisasa kuwafikia wananachi hasa wale walioko Vijijini wakati watakaporejea katika Mataifa yao.
Aliongeza kwamba licha ya Zanzibar kusifiwa kwa kupiga hatua kubwa ya mawasiliano lakini bado Serikali inaendelea na mikakati ya kusimamia upatikanaji wa huduma za mawasiliano ili ziwafikie wananchi wote mijini na Vijijini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka alisema  lengo la warsha hiyo ni kujenga nguvu zitakazosaidia kufikisha mawasiliano sehemu zisizo na huduma hizo.
Dr. Turuka alifahamisha kwamba mfumo huu mpya ambao unaanza kuelekezwa katika mataifa machanga unakusudiwa kuanzisha mpango maalum wa mafunzo ya maskuli kwa kutumia mtandao wa moja kwa moja wa mawasiliano kati ya sehemu moja hadi nyengine.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na huduma za mawailiano  ambazo zitawahusisha baadhi ya wasimamizi waliojiandaa kutoka huduma hizo kwa kupatiwa ruzuku katika maeneo ya vijijini.
  Tumefarajika kuona wataalamu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote wameamua kuifanya warsha hii hapa Zanzibar kufuatia Visiwa hivi kupiga hatua ya maendeleo katika matumizi ya mawasiliano ya simu za mkononi “ . Alisisitiza Dr. Turuka.
Warsha hii ya sita ya mawasiliano imeshirikisha  Mataifa  12 ya Bara la Afrika wakiwemo pia wawakilishi wa  mataifa ya India, Malaysia na Marekani   wakiwa chini ya udhamini wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote kutoka Nchini Uholanzi.

Othman Khamis Ame
( Vuga Newsroom )
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/5/2013.



No comments:

Post a Comment