HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA MOJA WA BARAZA LA
WAWAKILISHI- TAREHE 19 APRILI, 2013
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye wingi wa rehema na neema, kwa kutujaalia uzima na afya njema tukaweza kuhudhuria Mkutano huu wa kumi na moja wa Baraza lako Tukufu. Nakushukuru wewe Mheshimiwa Spika na wasaidizi wako wote. Kama kawaida yako umeliendesha vyema Baraza hili na kwa umahiri mkubwa, hekima na busara ambazo zimefanikisha mkutano huu. Mafanikio ya mkutano huu pia yanatokana na umakini wa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa michango yao mbali mbali waliyoitoa wakati wote wa majadiliano.
Mheshimiwa Spika, mchango wa waandishi wa habari pia ni mkubwa katika kufanikisha mkutano huu. Kwa kipindi chote cha mkutano wetu vyombo vya habari vya Serikali na watu binafsi vimekuwa vikifuatilia kwa karibu majadiliano yetu na hatimaye kuwafikishia wananchi wetu. Hongereni sana kwa kazi yenu nzuri.
Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa dhati Rais wetu mpendwa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa busara, hekima na ujasiri mkubwa alionao katika kuliongoza Taifa letu na kutuletea maendeleo. Ni dhahiri kwamba, wananchi wa Zanzibar wamekuwa na imani na matumaini makubwa kwa Rais wao kutokana na mabadiliko yanayoonekana katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Aidha, namshukuru na kumpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad kwa jitihada kubwa anayochukua kumshauri vizuri Rais wetu katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Sina budi pia kuwashukuru Viongozi wote wa Serikali, Vyama vya Siasa na wananchi kwa ujumla kwa namna wanavyoendelea kudumisha amani na utulivu na kutekeleza majukumu yao katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Ni matumaini yangu kwamba watauendeleza mwenendo huu ili amani na utulivu viendelee kutawala katika nchi yetu, kwani bila ya amani na utulivu maendeleo tunayotafuta yatakuwa taabu kupatikana.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI:
Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Machi, 2013 nchi yetu ya Tanzania ilipokea ugeni wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping ambapo lengo kubwa la ziara hiyo ni kukuza uwekezaji wa biashara baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Aidha, Rais wa China alipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Viongozi Waandamizi wa SMZ. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imenufaika kwa kiwango kikubwa na ziara ya Rais Xi Jinping ambapo jumla ya miradi saba (7) imo kwenye mpango wa kunufaika na ufadhili wa Serikali ya China. Kati ya miradi hiyo saba (7), miradi mitatu (3) imekubaliwa kupewa fedha ikiwemo mradi wa kazi za miundombinu, ukarabati wa matengenezo ya Hospitali ya Abdalla Mzee na kupatiwa msaada wa vifaa vya kukagua mizigo iliyomo ndani ya kontena bandarini. Namshukuru sana Mheshimiwa Omar Yussuf Mzee, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kwa kuliarifu Baraza lako Tukufu kwa ukamilifu kuhusu ugeni huu.
Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa kuwa hivi sasa tuko katika kipindi cha msimu wa mvua za masika. Mwishoni mwa mwezi wa Februari 2013, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania Kanda ya Zanzibar ilitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za masika kwa mwaka huu ambayo ilielezea kuwa mvua hizo zilitarajiwa kuanza mapema kuliko kawaida na zingekuwa za wastani na juu ya wastani kwa mwezi wa Machi na kutarajiwa kuwa chini ya wastani kwa miezi ya Aprili na Mei. Baada ya kupokea taarifa hiyo, Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa ilijadili na kuweka mikakati na hatua madhubuti za kuchukuliwa ili mvua hizo pindipo zikinyesha, zisiweze kuleta madhara makubwa. Kamati iliziagiza sekta zote zinazohusika na kukabiliana na maafa ziendelee kuchukua hatua za tahadhari na kujiandaa kukabiliana na majanga pindipo yakitokezea. Mpaka sasa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kuwa hali ya wananchi wetu bado iko salama na hakuna madhara makubwa yaliyokwisha tokea. Aidha, mvua za mwaka huu zimekuwa zikinyesha vizuri, kwani zimekuwa zikitupa muda wa kujitafutia riziki.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imo katika harakati za kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume iliyoundwa ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Mabadiliko ya Katiba kutoka kwa wananchi tayari imekamilisha kukusanya maoni hayo kupitia Shehia zao, Taasisi za Serikali na zisizokuwa za Serikali pamoja na makundi maalum. Hii ilikuwa ni hatua ya kwanza. Hivi sasa kazi ya uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, ikiwa ni hatua ya pili inaendelea ambapo Mabaraza hayo yataanza kazi zake za kupitia Rasimu ya awali ya Katiba Mpya hivi karibuni. Ni imani yangu kwamba, Mabaraza hayo yatatekeleza majukumu yao kwa umakini na ufanisi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa. Nitumie nafasi hii kuwasihi Wajumbe wa Mabaraza hayo kuitumia fursa hiyo muhimu na ya kipekee kutoa michango yenye maslahi ya nchi yetu na wananchi wake bila kuweka mbele itikadi zao za Vyama vya Siasa, dini na maeneo wanayotoka. Naamini kuwa kama ilivyomalizika hatua ya kwanza, na hatua hii ya pili itamalizika salama.
Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 10 Aprili, 2013 Wazanzibari sote tulijumuika katika sherehe za Uzinduzi wa kukamilika mradi wa njia mpya ya kusafirishia umeme yenye uwezo wa kuchukua Megawati 100 za umeme kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. Kwa hakika nchi yetu imefungua ukurasa mwengine wa maendeleo katika nyanja hii muhimu kwa mustakbali wa maendeleo yetu ya kiuchumi na kijamii. Hatua hii ni muendelezo wa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme hapa Zanzibar kama ilivyoelezwa katika Dira yetu ya Maendeleo ya 2020, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA II) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 – 2015. Tunatoa pongezi na shukurani za dhati kwa Serikali na Watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) kwa kutuunga mkono katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo hasa katika mradi huu na ule wa ujenzi wa barabara za Kaskazini, Pemba. Napenda kutoa wito kwa wananchi kuthamini jitihada hizi za Serikali kwa kuilinda na kuitunza miundombinu yote ya umeme huu na ile ya awali kwa kuhifadhi mazingira ya maeneo ambayo miundombinu hiyo imepita. Kwa kuupata umeme huu, tunatumai kauli ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuwa mgao wa umeme sasa basi itakuwa ya kweli. Pamoja na kuupata mradi huu muhimu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuwakaribisha wawekezaji wenye nia ya kuja kuwekeza katika miradi ya nishati mbadala ili kuongeza uwezo wa Zanzibar kuwa na umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, taarifa za kitaalamu juu ya ugonjwa wa malaria hapa nchini inaonesha kwamba kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu umedhibitiwa kupitia Programu ya Kupambana na Malaria inayofadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Marekani. Hata hivyo, bado kuna matukio machache ya kupatikana wagonjwa katika Wilaya tisa (9) za Unguja na Pemba. Ni Wilaya ya Mjini pekee ambayo hadi sasa haijaripotiwa kupatikana mgonjwa wa malaria. Serikali imeendelea na kazi ya upigaji dawa katika maeneo yaliyobainika kuwepo wagonjwa wa malaria. Jumla ya nyumba 26,900 zimepigwa dawa kati ya nyumba 28,463 sawa na asilimia 94.5 ya nyumba zote zilizotakiwa kupigwa dawa. Aidha, jumla ya wagonjwa wanne (4) wa malaria Unguja na Pemba wameripotiwa kufariki katika kipindi cha Julai, 2012 hadi Machi, 2013. Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa pamoja na kutoa mashirikiano kwa watendaji wanaosimamia zoezi la upigaji dawa majumbani ili kushinda vita dhidi ya malaria, kwani Zanzibar bila malaria inawezekana. Pamoja na juhudi hizo za Serikali, bado kuna baadhi ya wananchi wakiwemo na baadhi ya Viongozi kukataa nyumba zao kupigwa dawa. Ningewasihi sana wananchi na hasa viongozi kuacha tabia hiyo ili wawe mfano kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi karibuni nchi yetu imeshuhudia matukio mbali mbali ya majanga hasa kuungua kwa majengo ya makaazi na biashara, matukio ambayo yanarudisha nyuma ustawi na maendeleo ya wananchi na Taifa kwa jumla. Uzoefu unaonesha kwamba, wananchi wanaofikwa na matatizo hayo mara nyingi hushindwa kurudi katika hali zao za kawaida kwa haraka na hivyo hupelekea kukata tamaa na shughuli zao za kiuchumi na kupata makaazi bora. Ni vyema basi wananchi na wafanya biashara wetu kuwa na utamaduni wa kukata bima ili kulinda mali zao majumbani na sehemu za biashara. Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako kutumia nafasi zao kushajiisha jamii katika maeneo yao juu ya umuhimu wa kukata bima. Ni jambo la kustaajabisha kuona mwananchi anaikatia bima gari yake yenye thamani ya Shilingi Milioni 5 au 10, lakini anaacha kukatia bima nyumba yake au sehemu yake ya biashara yenye thamani kubwa zaidi ya hapo. Nawaomba wananchi waitumie fursa zinazotolewa na Mashirika ya Bima ili kulinda mali zao.
Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya nchi na wananchi wake kiuchumi na kijamii. Kwa mujibu wa sheria, rasilimali hii bado itaendelea kuwa mali ya Serikali. Hivyo, wananchi na Taasisi zitapewa ardhi kwa matumizi yao tu na haitoruhusiwa kuuzwa. Hata hivyo, kumejitokeza tabia ya wananchi na baadhi ya Viongozi kuuza ardhi kiholela bila kufuata sheria na taratibu ziliopo hali ambayo inasababisha migogoro. Serikali haitomvumilia mtu yeyote atakaekwenda kinyume na sheria na taratibu hizo. Kama kila mara Mheshimiwa Rais anavyotukumbusha kuwa ardhi ni mali ya Serikali na haipaswi kuuzwa. Mtu anaeuza ardhi anauza mali ambayo siyo yake. Hivyo, muuzaji na mnunuzi wote kwa pamoja ni wakosaji na wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Naielekeza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kuisimamia vyema sheria za ardhi bila ya kumuonea haya mtu yeyote. Naipongeza Kamati ya Mawasiliano na Uchukuzi kwa kutukumbusha kuwa ardhi ambayo imetengwa kwa ajili ya maendeleo ya jamii iachwe itumike kwa shughuli hiyo. Lakini pia na wale wananchi waliopewa maeneo makubwa yapunguzwe ili wananchi wengine nao wafaidike na rasilimali yao hii. Namuagiza Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ayatekeleze maelekezo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala la migogoro ya ardhi, Serikali imeona njia pekee na nzuri ni kusajili ardhi kwa utaratibu uliowekwa na Sheria Namba 10 ya mwaka 1990. Katika utaratibu huo, kutakuwa na mfumo maalum wa kuwatambua watumiaji wa ardhi kama vile; waliopewa eka tatu tatu, mashamba binafsi, mashamba ya Serikali na maeneo ya wazi. Hivyo, nachukua nafasi hii kuwataka wananchi wote kusajili ardhi wanazozitumia katika muda uliopangwa kupitia Ofisi ya Mrajisi wa Ardhi ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ya mwaka 2012 kwa lengo la kuhakikisha kuwa inapeleka maendeleo na huduma mbali mbali za jamii karibu na wananchi wa visiwa vyetu vya Unguja na Pemba. Fedha hizo tayari zimeshakabidhiwa kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wanaostahiki kwa mwaka 2012 ambazo zilikuwa ni Shilingi Milioni Kumi (Shs:10,000,000/=) kwa kila mmoja. Ni mategemeo ya Serikali kwamba fedha hizo zimetumika kwa mujibu wa matakwa ya sheria husika. Kwa mwaka huu 2013 Serikali imeamua kuongeza kima hicho cha Shilingi Milion 10 hadi kufikia Milioni 15 ili kuwawezesha Waheshimiwa Wawakilishi kuwaunga mkono wananchi wao katika miradi midogo midogo wanayoianzisha kwa mujibu wa vipaumbele wanavyoviweka.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena, napenda niwakumbushe Waheshimiwa Wawakilishi kuwasilisha marejesho ya fedha walizopokea kwa mwaka 2012 kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwani hayo ni matakwa ya Sheria ambayo tumeijadili na kuipitisha kwa pamoja ndani ya Baraza letu hili. Haitokuwa jambo la busara kuja kuoneshana vidole humu ndani kwani sisi ni Viongozi na tunatakiwa tuwe mfano mzuri kwa jamii. Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ya mwaka 2013, Mheshimiwa Mwakilishi hatopatiwa fedha nyengine hadi atakapowasilisha marejesho kamili na sahihi.
MAMBO MUHIMU YALIYOJITOKEZA BARAZANI:
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu wa kumi na moja wa Baraza lako Tukufu, Serikali imewasilisha jumla ya Miswada mitano (5) ya Sheria ambayo inalenga kulinda ustawi na maslahi ya nchi yetu. Aidha, Baraza lako Tukufu lilipokea Ripoti za Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza kwa Wizara kwa mwaka 2011/2012 zilizowasilishwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara husika. Pia, Baraza lilipokea Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza kwa mwaka 2012/2013 zilizowasilishwa na Wenyeviti wa Kamati hizo. Ripoti hizo zilijadiliwa na kuchangiwa kikamilifu na Waheshimiwa Wawakilishi.
Mheshimiwa Spika, vile vile, katika mkutano huu jumla ya maswali 82 ya msingi na maswali 167 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi na kujibiwa kwa ukamilifu na Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara husika.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza uliowasilishwa ulikuwa ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo (ZURA). Madhumuni ya Mswada huu ni kuanzisha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati ambayo itasimamia ubora wa huduma inayotolewa kulingana na viwango pamoja na kudhibiti bei kwenye huduma za maji na nishati.
Katika kujadili Mswada huu, Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi na Waheshimiwa Wajumbe kwa ujumla wao walisisitiza zaidi juu ya usimamizi na utoaji wa huduma bora za maji na nishati pamoja na kusimamia utolewaji wa leseni kwa wauzaji wa mafuta kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa katika sheria hii. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wajumbe na wananchi kwa jumla kuwa Serikali imejidhatiti kuhakikisha kwamba huduma ya maji safi na salama na nishati itatolewa kwa kufuata misingi ya sheria hii ambayo itazingatia upatikanaji wa huduma bora, yenye viwango vinavyokubalika na itakayokidhi mahitaji ya watumiaji. Aidha, Mamlaka itasimamia viwango vya bei za maji na nishati ili kudhibiti upandaji wa bei hizo kiholela.
Mheshimiwa Spika, Mswada mwengine uliowasilishwa na kujadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Shirika la Bandari na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Mswada huu una madhumuni ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Kuanzishwa kwa Shirika la Bandari Namba 1 ya Mwaka 1997 yenye lengo la kuweka mazingira bora ya uendeshaji na udhibiti wa Bandari pamoja na kukuza uwiano na mashirikiano mazuri kati ya Shirika na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini.
Wakati wa kuujadili Mswada huo, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu walishauri kuwepo na udhibiti na usimamizi mzuri wa uuzaji wa tiketi za kusafiria ili kudhibiti upakiaji wa idadi kubwa ya abiria kuliko uwezo wa vyombo hivyo. Aidha, suala la ujenzi wa gati lilichukua nafasi kubwa katika michango ya Waheshimiwa Wajumbe na walishauri kuwa Serikali ijenge bandari itakayokidhi mahitaji ya hivi sasa na baadae. Niwahakikishie Waheshimiwa Wajumbe kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuzungumza na Washirika wa Maendeleo ili kupata fedha kwa ajili ya kuliendeleza eneo la Mpiga Duri kwa kujenga bandari ya kisasa. Aidha, nachukua fursa hii kuzitaka Taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa uuzwaji wa tiketi kuhakikisha kwamba suala la uuzwaji wa tiketi kiholela linadhibitiwa na kwamba yeyote atakaekwenda kinyume na sheria zilizopo achukuliwe hatua zinazofaa. Pia, niwaombe Waheshimiwa Wajumbe tushirikiane kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kununua tiketi katika maeneo yaliyoruhusiwa ikiwa ni pamoja na kukataa kununua tiketi zinazouzwa kiholela mikononi mwa walanguzi kwa ajili ya kulinda usalama wao.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa tatu uliowasilishwa na kujadiliwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako ni Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Kuweka Utekelezaji wa Majukumu na Uwezo na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Wadhifa wa Mwanasheria Mkuu umeanzishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 55. Katika kifungu cha 56 cha Katiba hiyo, kinaeleza kazi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa ndiye atakayekuwa Mshauri Mkuu wa kisheria kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na atatekeleza shughuli nyengine zozote za kisheria zitazopelekwa kwake au atakazoagizwa na Rais au kwa mujibu wa Katiba hii au Sheria nyenginezo zozote. Kutokana na mapungufu ya kimsingi ambayo yanaathiri ufanisi wa utendaji kazi, Serikali imeona haja ya kuanzishwa kwa Sheria hii itakayoiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakijadili mswada huu, Waheshimiwa Wajumbe waliishauri Serikali kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ishirikishwe kikamilifu katika kuandaa na kufunga mikataba mbali mbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuepuka watendaji kufunga mikataba mibovu. Serikali itaendelea kuitumia ipasavyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa masuala yote yanayohusu sheria, ufungaji wa mikataba ambapo kitengo maalum cha kusimamia Mikataba kitaundwa ili kudhibiti mikataba na nyaraka za Serikali.
Mheshimiwa Spika, Mswada wa nne uliowasilishwa ni Mswada wa Sheria ya Mahkama ya Biashara Zanzibar na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo. Madhumuni ya mswada huu ni kuanzisha mfumo madhubuti wa kufanya mageuzi na kuimarisha mfumo wa kisheria, kitaasisi na utendaji wa shughuli zake hapa Zanzibar. Pia mswada huu umezingatia changamoto zinazokabili utatuzi wa migogoro ya kibiashara hapa Zanzibar chini ya mfumo wa sheria uliopo sasa ambao unazingatia migogoro ya kibiashara kama migogoro mingine yeyote. Wakati wakichangia mswada huu Waheshimiwa Wajumbe walieleza kuwa kuna tatizo la kesi kukaa muda mrefu bila kusikilizwa na hivyo kuongeza malalamiko ya wadai na wadaiwa wa kesi hizo. Pia imeonekana kuwa kuna tatizo katika uwekaji wa kumbukumbu wa kesi zote zinazowasilishwa na zilizokamilika.
Mheshimiwa Spika, kupitia sheria hii Mahkama itaweka utaratibu mzuri kuhakikisha kuwa kesi zote zinazowasilishwa zinasikilizwa kwa muda mfupi zaidi. Aidha, suala la uwekaji wa kumbukumbu za kesi zote na utekelezaji wake litapatiwa ufumbuzi kwa kuanzishwa Daftari maalum la kumbukumbu ambalo litahifadhi kesi zote na maamuzi yanayotolewa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali kwamba Baraza hili pia lilipokea na kujadili Ripoti za Utekelezaji wa Maagizo ya Kamati za Kudumu za Baraza kwa Wizara kwa mwaka 2011/2012 pamoja na Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza kwa mwaka 2012/2013. Waheshimiwa Mawaziri walitoa ufafanuzi wa kina na kwa ufasaha hoja zote zilizojitokeza. Nachukua nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe wao kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuishauri Serikali katika kutekeleza Majukumu yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa ufafanuzi wa hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wawakilishi, naamini hoja na ufafanuzi uliotolewa ni kwa lengo la kuimarisha utendaji wetu katika sekta mbali mbali za Serikali, ili Serikali yetu iendelee kuaminika mbele ya macho ya wananchi inaowatumikia.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza kwa dhati Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa namna walivyoichangia ripoti ya PAC kwa hisia kali zilizoonyesha utendaji dhaifu wa Watendaji wetu kwa matumzi yasiyoridhisha ya pesa za Serikali katika Mawizara na Taasisi mbali mbali za Serikali. Nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati hii, Mheshimiwa Omar Ali Shehe pamoja na Wanakamati wake wote kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufanya uchunguzi wa kina kwenye Mawizara na Taasisi mbali mbali za Serikali mpaka wakaiwasilisha ripoti nzuri kama hii.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wakiwa wasimamizi wakuu wa watendaji wao wamezisikia hisia hizo na watafanya kila linalowezekana kuzirekebisha kasoro zilizoonekana. Ninaamini kuwa kasoro hizo zitarekebishwa na hazitorejewa tena.
Mheshimiwa Spika, katika michango iliyohusiana na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, liligusiwa suala la mafuta na gesi asilia kutolewa kutoka kwenye orodha ya Muungano, na wapi suala hili lilipofikia.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inayoongozwa na Wanasheria Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inalifanyia kazi suala hili. Ninategemea tutapata taarifa ya awali ya namna suala hili linavyoendelea tutakapofanya kikao chetu cha pamoja kati ya SMT na SMZ chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuzungumzia kero (changamoto) za Muungano, kitakachofanyika tarehe 28 Aprili, 2013. Lakini niseme tu Mheshimiwa Spika, kuwa suala hili si rahisi kama tulivyofikiria lina mambo mengi ya kiufundi ambayo ndiyo yanayofanyiwa kazi na Wanasheria Wakuu wa Serikali wa pande mbili. Hata hivyo, nina matumaini makubwa kwamba Wanasheria wetu wakuu hawa, wa SMT na SMZ, watalifikisha jambo hili mahala pazuri katika muda mfupi utakaowezekana.
Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili ripoti ya Wizara ya Katiba na Sheria, baadhi ya Waheshimiwa Wajumbe waliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itoe kauli yake kama Serikali ya kutoa mwongozo kuhusu suala la hatma ya Zanzibar katika suala zima la mjadala wa Katiba.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishaeleza hapo awali, mchakato wa Katiba sasa unaingia katika hatua yake ya pili baada ya hapo zitabaki hatua za kufanyika kwa Bunge la Katiba kujadili rasimu ya Katiba hiyo na hatimae hatua ya kura ya maoni.
Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa Katiba linaendeshwa kwa kufuata sheria iliyotungwa kwa pamoja baina ya pande mbili za Muungano na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia Baraza lako Tukufu. Kwa hivyo, Mheshimiwa Spika, kutokana na mchakato kuendeshwa kwa kufuata sheria ambayo imeweka utaratibu mzima wa kuliendesha zoezi hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kama Serikali haina kauli ya kutoa mwongozo juu ya jambo hilo. Tunaiachia Tume ya Katiba ifanye kazi yake.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya ufungaji wa kikao cha Baraza cha mwezi wa Januari, 2013 nililieleza Baraza lako Tukufu kuwa maandalizi ya ununuzi wa meli ya abiria yameshakamilika, kilichosalia ni utiaji wa saini. Tumechelewa kukamilisha uwekaji wa saini mkataba wa kutengeneza meli hiyo, kutokana na kwamba tulitaka tujenga meli itakayokidhi haja yetu. Meli hiyo itabeba abiria 1,200 pamoja na mizigo isiyopungua tani 200. Aidha, meli hiyo itaweza kuhimili bahari yetu hasa mkondo wa Nungwi.
Mheshimiwa Spika, sasa napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kuwa maandalizi yote juu ya ujenzi wa meli mpya ya abiria pamoja na mchoro wa meli yenyewe yamekamilika na fedha tulizozikusanya zitatumika kulipia sehemu ya gharama ya ujenzi wa meli hiyo na ni matarajio yangu kuwa utiwaji wa saini utakamilika ndani ya mwezi wa Mei, 2013. Kadhalika, ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kuchukua miezi kumi na nane baada ya utiwaji wa saini.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Spika, nachukua tena nafasi hii kukushukuru tena wewe binafsi kwa kuliendesha Baraza hili vizuri na kwa ufanisi wa hali ya juu. Pia nawashukuru Waheshimiwa Wawakilishi kwa kutekeleza Majukumu yao ya kuishauri Serikali na mwisho nawashukuru wananchi wote kufuatilia mwenendo wa Baraza letu hili. Nawashukuru tena Waheshimiwa Wawakilishi wetu wa wananchi kwa michango yao ya uwazi ambayo ilikuwa na nia ya kuimarisha utendaji wa Serikali. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu na tumepokea ushauri wao kwa mikono miwili. Pamoja na kupokea mawazo, ushauri na mapendekezo yao na kuahidi kuyatekeleza, niseme tu pale ambapo Serikali imefanya vizuri basi nayo ipongezwe na kusifiwa ili kuitia moyo ifanye vizuri zaidi.
Mwisho, Mheshimiwa Spika, ninawatakia Waheshimiwa Wawakilishi kila la kheri na mafanikio mema katika kuwatumikia wananchi katika Majimbo yao na kuwatakia safari njema na salama ya kurejea Majimboni mwao.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 12 Juni, 2013 saa 3.00 barabara za asubuhi.
Naomba kutoa hoja.