Thursday, 2 May 2013

  UFUNGUZI WA WARSHA  YA  MAWASILIANO KUPITIA MFUMO WA TEKNOLOGIA YA KISASA.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifungua warsha ya siku tano kuhusu huduma za mawasiliano vijijini inayofanyika katika hoteli ya Kimataifa ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.



Katibu Mkuu  Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ya Serikali ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka akijiandaa kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuifungua warsha ya Kimataifa ya siku tano ya mawasiliano Vijijini huko ukumbi wa Hoteli ya Melia Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kushoto ya Dr. Florens Martin Turuka ni Makamu wa  Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi na Afisa Mkuu wa Mfuko wa wa huduma za Mawasiliano Mhandisi  Peter Ulanga.




Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku tano kuhusu huduma za mawasiliano wanaotoka mataifa 16 Barani Afrika wakiwemo pia Wawakilishi wa Mataifa ya India Malaysia na Marekani.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote kutoka Nchini Uholanzi na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi ya Teknolojia ya SMT mara baada ya kuifungua Warsha ya siku tano ya mawasiliano.
Picha na Hassan Issa wa  -(Vuga  newsroom )-  OMPR – ZNZ.



Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Maendeleo ya haraka yanaweza kupatikana kwa Mataifa Machanga iwapo suala la matumizi ya Mtandao wa kisasa wa Mawasiliano ya Kiteknolojia utapewa msukumo unaostahiki.
Alisema mfumo huo wa Teknolojia unaweza pia kutoa ajira hapo baadaye kwa kuangalia zaidi maeneo ya Vijijini ambayo huduma hizo za mawasiliano hazijafika na mwengine ziko katika kiango hafifu.
Balozi Seif alisema hayo wakati akiifungua warsha ya siku tano kuhusu mawasiliano Vijijini iliyoandaliwa na  Mfuko wa Mawasiliano kwa wote wenye makao makuu yake Nchini Uholanzi, warsha ambayo inafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya Melia iliyopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Kilimo, Biashara na hata  Elimu ni sekta za msingi zinazoweza kuendelezwa kwa kutumia mfumo huo wa Teknolojia ya kisasa ya mawasiliano.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serkali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeanza hatua za kufuata mfumo huu ili kutengeneza mazingira bora yatakayowezesha kukuza chumi wa Taifa katika kutumia Taaluma hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea hafaja yake kutokana na warsha hiyo kufanyika Nchini Tanzania, fursa  ambayo itasaidia kuunganisha nguvu za pamoja  katika kukabiliana na changamoto zilizomo kwenye mfumo huo wa mawasiliano.
“ Tumeshuhudia Mataifa kama vile Chile, Uturuki na Malaysia yalivyopiga hatua kubwa na ya haraka katika kuimarisha uchumi wao baada ya kuamua kutumia mfumo huo wa mawasiliano “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwataka washiriki wa warsha hiyo ya mfuko wa mawasiliano kwa wote kufikiria njia zitakazowezesha mawasiliano ya teknolojia ya kisasa kuwafikia wananachi hasa wale walioko Vijijini wakati watakaporejea katika Mataifa yao.
Aliongeza kwamba licha ya Zanzibar kusifiwa kwa kupiga hatua kubwa ya mawasiliano lakini bado Serikali inaendelea na mikakati ya kusimamia upatikanaji wa huduma za mawasiliano ili ziwafikie wananchi wote mijini na Vijijini.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano,Sayansi na Teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Florens Martin Turuka alisema  lengo la warsha hiyo ni kujenga nguvu zitakazosaidia kufikisha mawasiliano sehemu zisizo na huduma hizo.
Dr. Turuka alifahamisha kwamba mfumo huu mpya ambao unaanza kuelekezwa katika mataifa machanga unakusudiwa kuanzisha mpango maalum wa mafunzo ya maskuli kwa kutumia mtandao wa moja kwa moja wa mawasiliano kati ya sehemu moja hadi nyengine.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na huduma za mawailiano  ambazo zitawahusisha baadhi ya wasimamizi waliojiandaa kutoka huduma hizo kwa kupatiwa ruzuku katika maeneo ya vijijini.
  Tumefarajika kuona wataalamu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote wameamua kuifanya warsha hii hapa Zanzibar kufuatia Visiwa hivi kupiga hatua ya maendeleo katika matumizi ya mawasiliano ya simu za mkononi “ . Alisisitiza Dr. Turuka.
Warsha hii ya sita ya mawasiliano imeshirikisha  Mataifa  12 ya Bara la Afrika wakiwemo pia wawakilishi wa  mataifa ya India, Malaysia na Marekani   wakiwa chini ya udhamini wa Mfuko wa mawasiliano kwa wote kutoka Nchini Uholanzi.

Othman Khamis Ame
( Vuga Newsroom )
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/5/2013.



Tuesday, 30 April 2013


           NMB  YAKABIDHI MSAADA WA MADESKI   SKULI YA  BUMBWINI


Meneja Biashara  kutoka Makao Makuu ya Benki ya Biashara Jijini Dar es salaam Bibi Shilla Sennoro akimkabidhi Mgeni Rasmi Mama Asha Suleiman Iddi Madeski 100 na Viti 100 kwa ajili ya Skuli za Msingi za Bumbwini na Mangapwani hapo skuli ya Msingi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B.



Mama Asha Suleiman Iddi akikabidhi rasmi madeski 100 na Viti 100 kwa uongozi wa Skuli za Bumbwini na Mangapwani ambavyo vimetolewa msaada na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } hapo Skuli ya Msingi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B.







Baadhi ya Wanafunzi wa Skuli ya Msingi ya Bumbwini na Mangapwani wakifurahia Vikalio vipya vilivyotolewa msaada na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } hapo Skuli ya Msingi Bumbwini.

Picha  na Hassan Issa  (Vuga Newsroom )



 

 Press Release:-

Taasisi za Umma,Mashirika pamoja na Sekta Binafsi zina wajibu wa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali Kuu katika kuwajengea mazingira bora Wananachi wake hasa katika Sekta muhimu ya Elimu yenye dhamana ya kufinyanga   wataalamu na Viongozi wa Baadae.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati wa hafla maalum ya kukabidhi Meza na Viti mia Moja kwa Skuli za Msingi za Bumbwini na Mangapwani iliyofanyika katika Skuli ya Msingi Bumbwini iliyopo Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Msaada huo wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Milioni kumi                           { 10,000,000/- } umetolewa na Benki ya Biashara Tanzania { NMB } ambapo kila Skuli imebahatika kupata Meza Hamsini na Viti Hamsini.
Mama Asha Suleiman Iddi alisema  nguvu za Serikali pekee kwa sasa haziwezi kukidhi mahitaji ya Wananachi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji miongoni mwa Wananchi na maeneo tofauti hapa Nchini.
Aliipongeza Benki ya Biashara Tanzania { NMB } kwa uamuzi wake wa kusaidia Sekta ya Elimu ambayo ndio muhimili mkubwa wa Maendeleo katika Taifa lolote Ulimwenguni.
Alisisitiza kwamba utekelezaji wa Sera ya Elimu Zanzibar katika kuhakikisha kila mtoto wa Taifa hili anapata Elimu ya lazima umo ndani ya Sera ya Chama cha Mapinduzi iliyopata ridhaa ya Wananchi walio wengi ilipokuwa  ikinadiwa wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkuu uliopita wa Mwaka 2010.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwaomba Wazaliwa na Vijiji hivyo  vya Bumbwini na Mangapwani kusaidia Maendeleo ya Vijiji vyao ili kuunganisha nguvu zao  pamoja na viongozi wao Mbunge na Mwakilishi.
Alishauri kufanywa kwa tathmini ili kujua  mahitaji halisi ya huduma za umeme ili kupata mbinu za  kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo  linalowakabili wananchi wa Mangapwani la ukosefu wa Huduma ya Umeme.
Mapema akitoa Taarifa fupi Meneja wa Biashara kutoka Makao Makuu ya Benki ya NMB Mjini Dar es salaam Bibi  Shilla Sennoro alisema anza ya Benki hiyo hivi sasa ni kuhakikisha inaimarisha huduma zake ili kwenda sambamba na jitihada za Serikali za kuwapatia huduma za kifedha wananchi walio wengi.
Bibi Shilla alieleza kuwa katika kutekeleza jitihada hizo Benki hiyo licha ya kuwa na matawi zaidi ya 145 Nchini kote lakini pia imelenga kuongeza mengine katika Wilaya mpya na maeneo mengine yanayohitaji huduma za kifedha.
Meneja huyo wa Biashara kutoka Makao Makuu ya NMB Jijini Dar es salaam alifahamisha kwamba hatua hiyo imelenga kusaidia wananchi kuokoa muda wao na kuutumia zaidi katika shughuli za kiuchumi.
Bibi Shilla Sennoro  alisema Taasisi yake kwa kutambua umuhimu wa Jamii na jitihada za Serikali Benki hiyo itaendelea kutoa misaada  kwa jamii katika sekta mbali mbali kadri hali itakavyoruhusu.
Katika Risala yao Wananchi, Walimu na Wanafunzi hao wa Vijiji vya Bumbwini na Mangapwani wameishukuru Benki ya Biashara ya NMB kwa uwamuzi wake wa kusaidia Samani skuli hizo ambazo zipapunguza kero linalowakabili wanafunzi la baadhi yao kukaa chini.
Hata hivyo wananchi, walimu na Wanafunzi hao walisema  bado skuli hizo zinaendelea kukabiliwa na changa moto kadhaa ikiwemo huduma za maji safi, Umeme kwa kijiji cha mangapwani pamoja na uchakavu wa baadhi ya Majengo ya Skuli zao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/4/2013.



Saturday, 27 April 2013




 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Ujumbe wa Viongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme               { Botjheng Water na Megtron } ya Afrika Kusini pamoja Uongozi wa Wizara ya Ardhi , Makazi, Maji na Nishati aliokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.







Mwakilishi wa Makampuni ya Botjheng Water na Megatron ya Afrika Kusini Bwana Dean Hiran  akiwa  pamoja na Viongozi wa Makampuni hayo wakizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na Uongozi wa Makampuni ya Maji na Umeme { Botjheng Water na Megatron } ya Afrika Kusini mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Picha nan Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.




Wednesday, 24 April 2013


Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wakisikiliza Taarifa fupi iliyosomwa na Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Vuga Mkadini Nd. Hamad Mwinyi Ramadhan katika uzinduzi wa Mradi wa maji safi na salama wa Kijiji cha Vuga Mkadini.



Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizindua mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Vuga Mkadini ndani ya Jimbo la Kitope.
Nyuma ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi pamoja na baadhi ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo.

Picha na Hassan Issa wa  - OMPR – ZNZ.

 Press Release:-
Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kujitahidi katika kuhakikisha huduma za Maji safi na salama ndani ya Jimbo hilo zinapatikana ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma hiyo Wananchi wake.
Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif alieleza hayo wakati akizindua mradi wa huduma za maji safi na salama katika kijiji cha Vuga Mkadini kilichomo ndani ya jimbo la Kitope.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Maji ni miongoni mwa huduma muhimu inayopaswa kutumiwa na kila mwanaadamu, hivyo Uongozi huo utachukuwa juhudi ya ziada katika kuona kero za upatikanaji wa huduma hiyo inakuwa ndoto ndani ya jimbo hilo.
Aliwaeleza Wananchi hao wa Kijiji cha Vuga Mkadini kwamba utaratibu mwengine utaangaliwa katika mpango wa kujenga Tangi jengine katika eneo hilo ili lisaidie kukidhi mahitaji ya maji ambayo kwa hivi sasa yanaendelea kuwa ya mgao.
Balozi Seif aliwakumbusha Wananchi hao kuzingatia maagizo ya Wahandisi katika matumizi ya mashine zinazotumika katika Tangi la Kisima kilichopo Kijijini hapo ili zidumu kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.

Akitoa Taarifa ya uzinduzi wa Mradi wa maji safi na salama wa katika Kijiji hicho cha Vuga Mkadini Katibu wa Kamati ya  maendeleo ya Kijiji hicho Ndugu  Hamad Mwinyi Ramadhan alisema huduma za maji safi ilikuwa ni kilio cha muda mrefu katika kijiji chao.
Nd. Hamadi alisema juhudi za Viongozi wa Jimbo hilo kupitia Mbunge huyo katika harakati za ziada za kujituma zimesaidia kuleta maendeleo ya haraka ndani ya Jimbo  hilo.
“ Ukweli juhudi unazoendelea nazo siku hadi siku, hasa kilio chetu cha ukosefu wa Pump ya kupandisha maji na Switch Control Box zimeleta faraja na kwa kweli tunajisikia raha isiyo kifani “. Alisema Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Vuga Mkadini Nd. Hamad.
Akitoa Shukrani kwa niaba ya Wananachi wa Kijiji hicho Diwani wa Wadi ya Fujoni Nd. Hamad Khamis Hamad amempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif kupitia uratibu wa Mke wake Mama Asha Suleiman Iddi kwa kusimamia vyema maendeleo ya Wananachi wa Jimbo hilo.

Diwani Hamad alisema Wananchi wa Jimbo hilo wamekuwa wakishuhudia usimamizi wa Mbunge Kimawazo na hata uwezeshaji unaoendelea kuleta faraja na neema kwa wananchi hao.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif tayari ameshauzindua mradi wa Maji safi na Salama wa Kijiji cha Kipandoni uliogharimu shilingi Milioni 2,300,000/-, Kisima cha Maji Mgambo kiligharimu shilingi Milioni 4,000,000/- na mradi wa Vuga Mkadini umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 6,900,000/-.
Miradi yote mitatu imegharimu zaidi ya shilingi Milioni Kumi na Tatu na Laki Mbili { 13,200,000/- }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/4/2013.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na watendaji wa shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } alipofanya ziara ya ghafla Kituoni hapo Karume House


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na ule wa ZBC wakisikiliza changamoto za watendaji wa ZBC wakati alipofanya ziara fupi kituoni hapo


 Baadhi ya watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } wakisikiliza hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hayupo pichani alipofanya ziara fupi Kituoni hapo.


 Mhandisi wa ZBC Saadat Haji akielezea kero wanazopambana nazo Kituoni hapo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefanya ziara ya ghafla Kituoni hapo.



 Mtayarishaji wa Vipindi shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } Nasra Nassor akishauri umuhimu wa kuwa na bajeti maalum katika utengenezaji wa vipindi.




Press Release:-
Matumaini ya Wananachi katika kupokea na hatimae kuangalia matangazo ya Televisheni kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } yatarejea endapo watendaji wa Shirika hilo kwa kushirikiana na Viongozi wao watajipanga vyema katika kutekeleza majukumu yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo alipofanya ziara ya ghafla katika Kituo cha Televisheni cha Shirika hilo kilichopo Karume House kuangalia matatizo yaliyopelekea kukosekana kwa matangazo ya Habari Kituoni hapo.

Akizungumza na Uongozi wa Shirika hilo na baadae Watendaji wake Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuunda Shirika hilo lengo likiwa ni kuimarisha zaidi matangazo yake pamoja na kwenda sambamba na mabadiliko ya mfumo wa utendaji katika sekta ya Habari Duniani.
Balozi Seif alisisitiza kwamba wakati umefika hivi sasa   kwa Shirika hilo kuendeshwa kibiashara, na hilo litafikiwa iwapo Taasisi zinazoendelea na zile zinazotumia na kuhitaji huduma za matangazo za Shirika hilo zitalipa.
“ Sisi Serikalini tumeshaliagiza Baraza la Wawakilishi ambalo liko chini ya Wizara yangu lianze kulipa fedha wakati linapoendelea na vikao vya Baraza katika matangazo yake ya moja kwa moja. Dodoma Shirika la Utangazaji Tanzania TBC wanalipwa na Bunge wakati wanaporusha matangazo yao utaratibu ambao hata sisi wabunge tunachangia suala hilo “. Alifafanua Balozi Seif.
“ Katika kujenga mahusiano mema baina ya Taasisi hizo inaweza kuruhusiwa kutangazwa  bure wakati wa kipindi cha maswali na majibu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia suala la uwajibikaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwaonya watendaji hao kuwepuka tabia ya fitna baina yao na Viongozi jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa kazi zao.
Alikemea kwamba Kiongozi ye yote ambae atapenda kutanguliza fitna na majungu mbele aelewe kwamba anajiingiza katika mfumo mbaya wa kazi unaosababisha kuyeyusha haki za wafanyakazi wake.

Hata hivyo Balozi Seif aliwapongeza Watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } kwa utendaji wao wa kizalengo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yao waliyopangiwa.
Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alisema Vituo vya Matangazo ya Televisheni haviwezi kufanya kazi zake kwa mpangilio wa bajeti kama zinavyofanya Idara nyengine.
Alisema Uongozi wa Shirika hilo umekuwa akitoa Taarifa za maandishi wakati yanapotokea matatizo hasa suala kubwa la vifaa na uharibikaji wa mashine lakini ufumbuzi wake huchukuwa muda mrefu kutokana na mfumo wa matumizi uliopo.
“ Tumekuwa tukiiandikia Wizara kuijuilisha matatizo yetu yanapotokea lakini hatua zinazochukuliwa za kusubiri fedha hupelekea hata vile vifaa vya dharura vikaharibika baada ya kukosa usaidizi wa ziada “. Alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa ZBC Nd. Chande.

Hata hivyo Ndugu Chande alimueleza Balozi Seif kwamba Uongozi wa Shirika hilo tayari umeshachukuwa hatua za dharura kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwasiliana na makampuni yanayotengeneza vifaa vinavyohitajika kituoni hapo kwa wakati huu wa dharura.
Alisema lengo la Shirika hilo katika mpango wake wa kuingia katika matangazo ya Kisasa ya Digital ni kuwa na mashine 10 za kurikodia vipindi zitakazotosheleza kabisa mahitaji ya vitengo vya Habari, Vipindi pamoja na Matangazo.
Kwa upande wao watendaji wa shirika hilo la Utangazaji Zanzibar wameelezea changamoto wanazopambana nazo kituoni hapo ambazo zimekuwa zikirejesha nyuma hamu na utendaji wao wa kazi za kila siku.

Walizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu usafiri wa uhakika wa kufuatilia Vipindi, Habari na hata kurejeshwa majumbani wakati wa usiku, ukosefu wa Bajeti za Vipindi, uchakavu wa Mashine za Matangazo, Haki za Wafanyakazi kama maposho na fedha za likizo pamoja na majungu na fitina baina ya Viongozi na Wafanyakazi.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/4/2013.






Press release

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imemuagiza mwekezaji aliyepewa eneo la Magofu ya Kihistoria liliopo Bweleo Wilaya ya Magharibi kuhakikisha kwamba ameshakamilisha shughuli zake za uwekezaji na kuanza kutoka huduma kama alivyoahidi katika mkataba wake ndani ya kipindi cha Mwaka mmoja kuanzia leo.
Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Mwekezaji huyo Bwana Chandra, Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya watu wa Bweleo, Sheha wa Shehia ya Bweleo, Mkurugenzi Zipa pamoja na  Mkurugenzi Mazingira hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema ameridhika na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Maalum aliyoiteua kuchunguza mgogoro wa eneo hilo Tarahere 28 Oktoba mwaka 20112 kati ya Mwekezaji huyo na wananachi wa Bweleo waliyoiomba Serikali Kuu kumnyang’anya eneo hilo Mwekezaji huyo baada ya kukaa nalo kwa miaka mingi bila ya faida ya Wananchi hao.
Akifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo Maalum ya kuchunguza mgogoro wa eneo hilo  ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Mh. Abdulla Mwinyi, Balozi Seif alimtaka Mwekezaji huyo kuhakikisha kwamba mradi wake unafaidisha kimapato Wananchi wa maeneo hayo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema njia pekee ya kuepuka migogoro ndani ya sekta ya uwekezaji ni kwa wananchi wenyewe kuiachia Serikali kuu kutimiza waji wake kwa kutiliana saini ya mikataba na wawekezaji ili kuwepuka ujanja unaopelekea kuleta mzozo hapo baadaye.
“ Moja kati ya suala nililolishuhudia wakati wa ziara yangu mwaja jana katika eneo hilo ni lile lalamiko la wananchi hao la kuzibiwa njia wanayoitumia wakati wanapotoka katika shughuli zao za uvuvi. Hili unapaswa kulichukulia hatua mara moja kwa kushirikiana na Uongozi wa Shehia, Zipa na Mazingira “. Balozi Seif alimuagiza Mwekezaji huyo.
Hata Hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwekezaji huyo Bwana Chandra kwa hatua yake ya kusaidia maendeleo ya Wananachi wa Vijiji vinavyouzunguuka mradi huo na kumuomba asichoke kuendelea kufanya hivyo ili kujenga uhusiano mwema na Wananchi hao.

Balozi Seif aliusisitiza Uongozi wa mradi huo kuwasiliana na Taasisi ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA }, Mipango Miji pamoja na Idara ya Mazingira ili kuhakikisha kwamba mradi huo unaendeshwa katika misingi iliyokubalika kutekelezwa Kisheria.
Eneo la Magufu ya Kihistoria la Bweleo limekuwa na mzozo wa muda mrefu kati ya Mwekezaji wake Bwana Chandra na Wananchi wa Vijiji vilivyolizunguuka eneo hilo wakidai Mwekezaji huyo kushindwa kuliendeleza kama ilivyokubalika.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar
23/4/2013..

Monday, 22 April 2013


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizindua wiki ya usalama bara barani hapo katika ukumbi wa salama hoteli ya bwawani Mjini Zanzibar.

Amina Mkombe na Mwanajuma Mkombe wakisoma utenzi kusherehesha kwenye usinduzi wa wiki ya usalama bara barani zilizofanyika katika ukumbi wa salama katika hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.


Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa akitoa takwimu za ajali na vifo kwa mwaka 2012 na 2012 kwenye uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani zilizofanyika katika ukumbi wa salama  bwawani hoteli.





Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi akitoa takwimu za vifo na majeruhi waliopokelewa katika vituo mbali mbali vya afya hapa Zanzibar kwenye uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani hapo bwawani hoteli.




Mwakilishi wa Wizara ya elimi Zanzibar Bwana  Ahmed Abdull majid akielezea madhara wanayoyapata wanafunzi waendapo maskulini wakati wanapotumia bara bara kwenye uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani hapo bwawani Hoteli.




Katibu Mkuu Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano Dr. Juma  Malik akielezea juhudi zinazochukuliwa na Wizara yake katika kuendeleza miundo mbinu ya bara bara ili kupunguza ajali.




Waziri wa MKiundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Rashid Seif akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani hapo Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.




Baadhi ya washiriki walioshuhudia uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani zilizofanyika katika ukumbi wa salama hoteli ya bwawani Mjini Zanzibar.



Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kudumu ya usalama bara barani Mh. Abdulla Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi akitoa shukrani mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa wiki ya usalama wa bara barani hapo bwawani Hoteli Mjini Zanzibar.

 Picha Hassan Issa wa  - OMPR – ZNZ.


  Press Release:-

Wananchi wanaotumia  usafiri wa dala dala na magari yaendayo vijijini wametakiwa kuchukua hatua za kuripoti katika vituo vya Polisi au Idara ya Usafiri na leseni mara moja dhidi ya Madereva au Matingo  wanaowafanyia  vitendo vinavyokiuka sheria za bara barani.
Hatua ya kukomesha vitendo hivyo kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria  wahusika hao zitafanikiwa vyema endapo Wananchi watakubali kutoa ushirikiano unaofaa kwa Taasisi hizo katika kukabiliana na usumbufu huo.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua rasmi Wiki ya Usalama Bara barani hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Salama uliopo Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif aliliamuru Jeshi la Polisi, Kikosi cha usalama bara barani kusimamia sheria za usalama bara barani na kuondoa muhali kwa wote wanaokiuka sheria hizo kwa kuwachukuliwa hatua kali za kisheria kwani hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria.
Alisema kwa kuwa suala la usalama wa bara barani linahitaji nguvu za pamoja  madereva wana wajibu wa kuwajali watumiaji wengine wa bara bara ikiwa ni pamoja na watembeao kwa miguu, wapanda baskeli wakiwemo pia watu wenye mahitaji maalum.

Balozi Seif alielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya madereva na Matingo wao  kuwanyanyasa wananchi ambao ndio abiria wao kwa kutowafikisha  mwisho wa safari kama walivyoomba ruhusa ya usafirishaji pamoja na kuwatolea lugha chafu.
Akizungumzia suala la matumizi mabaya ya bara bara Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema bara bara nyingi zinaharibiwa  kwa kuwekwa matuta na wananchi baaba ya kukosa imani ya uendeshaji mbovu unaofanywa na baadhi ya madereva.
Balozi Seif alionya kwamba wakati umefika kwa Taasisi inayosimamia masuala ya Leseni kuweka utaratibu wa  kuwanyang’anya Leseni Madereva wanaosababisha  ajali  za mara kwa mara kwa makusudi na  uzembe.

Aliitaja sababu moja kubwa inayochangia ajali za mara kwa mara kwenye bara bara  nyingi hapa nchini kuwa ni matumizi ya simu za mkononi hali inayomfanya Dereva kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja.
“ Haiwezekani kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja. Na hili tumekuwa tukilishuhudia pia ndani ya majengo ya ibada ambapo muumini anashindwa kuzima simu yake wakati tayari mlangoni pameshawekwa tangazo la kukumbusha jambo hilo “. Alifafanua Balozi Seif.

“ Ukweli usiofichika ni kwamba Jamii kubwa ya Wazanzibari imekuwa kaidi katika kutii sheria ambazo zimetungwa maalum kwa lengo la kufuatwa uadilifu utakaotoa haki kwa kila Mtu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akigusia tukio la uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani ikiwa ni sehemu ya kutathmini utekelezaji wa mpango wa miaka kumi ya usalama bara barani ulioanzishwa na Rais wa Zanzibar Dr. Sheni Disemba mwaka 2011 Balozi Seif alisema  ajali za bara barani zimefikia kushika nafasi ya Pili kwa kusababisha vifo vingi baada ya ugonjwa wa ukimwi.
Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba uelewa wa hali ya usalama bara barani duniani umeongezeka baada ya shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } kueleza kuwa watu wapatao Milioni 1.3 hufa na wengine wapatao Milioni 50 hujeruhiwa ulimwenguni kila mwaka.
Alieleza kwamba ajali ya bara barani zina athari kiuchumi kwa kupunguza nguvu kazi ya Taifa sambamba na kuwaacha watu wenye ulemavu ambao kwa kiasi kikubwa  hupunguza uwezo wao wa uzalishaji mali katika kujipatia kipato kinachowawezesha katika maisha yao ya kila siku.

Balozi Seif alisema katika kukabiliana na changa moto hiyo ya ajali za bara barani Serikali itahakikisha inasimamia vilivyo bara bara zinazojengwa  ili zikidhi viwango ikiwa ni pamoja na uimara wa bara bara zenyewe, upana, pamoja na kuwekwa kwa alama za bara barani.
Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar Bwana Mussa Ali Mussa alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu wa magari pamoja na madereva wazembe.

Kamishna Mussa alisema ajali za bara barani kwa mwaka 2012 zilifikia 855 ikilinganishwa na ajali 849 kwa mwaka 2011 ikiwa na ongezeko la ajali sita wakati ambapo ajali hizo zimesababisha vifo vya watu 138 kwa mwaka 2012 kukiwa na ongezeko la vifo vya watu 47 ikilinganishwa na vile vya mwaka 2011 vya watu 117.
Bwana Mussa alizishauri Taasisi zinazohusika kuweka viwango maalum vya uingizaji wa magari nchini  kupunguza vyombo vilivyochakaa ambavyo ndivyo vinavyochangia kuongezeka kwa msongamano wa ajali zinazotokea Nchini.
Kamishna Mussa alisisitiza umuhimu wa kutumiwa kwa utatu ambao ni mawasiliano, mashirikiano pamoja na Uratibu katika kufanikisha malengo ya matumizi bora ya sheria ikiwemo  suala la matumizi sahihi ya bara bara.

Wakitoa mawazo yao baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya wiki ya usalama bara barani walisema ajali zinaweza kupungua au kuondoka kabisa iwapo alama za bara barani zitatumiwa kama zilivyokusudiwa.
Walisema wakati busara inaweza  kuokoa ajali kwa suala hili kuwekwa katika vichwa vya madereva wakati umefika kwa Wizara ya Maiundo mbinu na mawasiliano kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kulijadili tatizo la matumizi ya simu unaofanywa na madereva wakati wanapoendesha gari bara barani.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/4/2013.