Mwenyekiti
wa Bodi ya kuchunguza ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro II Khamis
Ramadhan Abdallah (kushoto) akikabidhi Ripoti ya Bodi hiyo baada ya
kukamilika kwa Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif
Suleiman Ofisini kwake Kisauni nje kidogo ya mji wa Zanzibar
Bodi ya kuchunguza ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro II leo imekabidhi rasmi Ripoti ya ajali hiyo baada ya kumaliza kazi hiyo kwa Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Rashid Seif Suleiman Ofisini kwake Kisauni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akikabidhi Ripoti hiyo Mwenyekiti wa Bodi
hiyo Khamis Ramadhan Abdallah amesema kazi hiyo waliyopewa wameweza
kuimaliza kwa mujibu wa siku walizopewa na walikuwa huru bila ya
kuingiliwa na mkono wa Serikali wala Taasisi yoyote.
Aidha alisema Bodi ilifanya kazi katika
mazingira magumu lakini walichukulia kazi hiyo niyanyumbani na niwajibu
wao kufanya kwa Maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo alisema hapo awali kazi hiyo
walipangiwa kuifanya kwa kipindi cha mwezi mmoja lakini kutokana na
uzito wa kazi hiyo na majukumu mengine walilazimika kuomba mwezi mmoja
ambapo kazi hiyo walitakiwa kuikabidhi kesho na badala yake wameweza
kuikabidhi leo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya kuchunguza ajali ya Meli ya MV. Kilimanjaro II, Khamis
Ramadhan Abdallah (katikati) akisoma baadhi ya vipengele vya Ripoti hiyo
wakati wa kumkabidhi Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano Zanzibar
Rashid Seif Suleiman (mwenye kanzu) Ofisini kwake Kisauni nje kidogo ya
mji wa Zanzibar. Picha – Nafisa M. Ali
Aidha Mwenyekiti huyo alitoa shukran zake
za dhati kwa niaba ya bodi hiyo kwa mamlaka ya Usafiri Baharini kwa
ushirikiano mzuri waliouonesha kwa bodi hiyo kwa kipindi chote cha kazi
hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu na
Mawasiliano Rashid Seif Suleiman ameipongeza Bodi hiyo kwa kufanya kazi
bila ya upendeleo na zaidi walizingatia uhalisia wa kazi yao na siyo
kubabaishwa na Mtu.
Aidha alisema chombo hicho hakikuundwa
kwa kutafutwa nani mbaya wala mkosa wa ajali hiyo bali kimeundwa kwa
ajili ya kuangalia mapungufu yaliyopo na kuweza kurekebishwa ili
Wazanzibari wasizidi kuumia.
Hata hivyo alisema dalili nzuri ipo
katika Ripoti hiyo na kazi iliyobaki ni kuisoma kwa kina na kisha
kukabidhi katika Mikono ya Serikali kuu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Aidha aliishukuru sana bodi hiyo kwa vile ilikuwa huru na kuweza kufanya kazi kwa kina bila kizuizi cha mtu wala Serikali.
Naye Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya
Miundombinu na Mawasiliano Tahir A.K Abdullah amesema Wananchi hivi sasa
wanasubiri kuona Serikali imefanya nini tokea ajali hiyo imetokea
ambapo aliwatoa wasiwasi kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa uchunguzi
uliofanyika.
Bodi hiyo ya Wajumbe watano ambayo
iliyoundwa chini ya Sheria ya Usafiri wa Baharini kifungu no. 4552 na
4551 ya mwaka 2006 imeundwa kufuatia ajali ya Meli ya MV.
Kilimanjaro II iliyotokea miezi miwili iliyopita katika mkondo wa Nungwi ilipokuwa ikitokea Pemba kuja Unguja.
No comments:
Post a Comment