Friday, 24 May 2013

Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Inguun Klepsvik amtembelea Makamo wa Pili wa  Rais Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Inguun Klepsvik Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar na kuiomba Norway kuangalia uwezekano wa kusaidia utaalamu wa Uvuvi wa Bahari Kuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwashukuru Madaktari Mabingwa wa China  kwa mchango wao mkubwa wa  huduma bora za afya ndani ya kipindi chao cha miaka Miwili ambao wanatarajiwa kumaliza muda wao ifikapo mwezi  ujao wa Juni mwaka huu.Hafla hiyo ya chakula cha usiku aliwaandalia hapo katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resor Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Madaktari Mabingwa wa China wanaotoa huduma za afya katika Hospitali mbali mbali za Zanzibar mara baada ya kula nao chakula cha usiku alichowaandalia ikiwa ni ishara ya kuwaaga rasmi baada ya kumaliza muda wao wa miaka miwili hapa Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa  -  OMPR – ZNZ.

  Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Timu ya Madaktari  Bingwa wa Jamuhuri ya Watu wa China kwa umakini wake wa kutoa huduma za Kiafya katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.
Pongezi hizo alizitoa wakati wa hafla maalum ya Chakula cha Usiku alichowaandalia Madaktari hao ambao wanatarajia kuondoka Nchini Mwezi ujao baada ya kumaliza muda wao wa kutoa huduma za afya wa miaka miwili hapa Zanzibar.
Hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji ilifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakifarajika kutokana na huduma nzuri wanazozipokea kutoka kwa madaktari Bingwa wa China wakati wanapofuata huduma za Afya katika Hospitali tofauti kubwa hapa Zanzibar.
Alifahamisha kwamba huduma za afya ndani ya Visiwa vya Zanzibar zimekuwa zikipanuka siku hadi siku kutokana na kuimarishwa kwa  mbiundo mbinu katika sekta ya  Afya kunakotekelezwa  kwa pamoja kati ya Wananchi na Serikali.
Balozi Seif alieleza kuwa mfumo huo wa miundo mbinu umekuwa ukipata nguvu za ziada za misaada ya vifaa, Utaalamu pamoja na uwezeshaji unaofanywa na mashirika, wahisani  na Mataifa rafiki miongoni mwao likiwemo la Jamuhuri ya Watu wa China.
“ Tumekuwa tukishuhudia kwa muda mrefu ndugu zetu wa China wanavyotuunga mkono katika masuala mbali mbali ya Maendeleo na Uchumi lakini Sekta ya Afya wameipa umuhimu zaidi Kivifaa na hata uwezeshaji “.  Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Watu China imekuwa ikiipatia Zanzibar  Madaktari Mabingwa wa fani tofauti katika mpango maalum iliyouweka Nchi hiyo kusaidia huduma za Afya mara tu baada ya   mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Alisema hatua hiyo imeendelea kujenga nguvu za Kihistoria kwa wananchi na Viongozi wa Pande hizi mbili zinazoimarisha  zaidi uhusiano uliopo wa kidugu wa mataifa haya rafiki.
Balozi Seif aliwahakikishia Madaktari Mabingwa hao wa Jamuhuri ya Watu wa China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kila msaada kwa Timu za Madaktari wa chi hiyo wanaopangiwa kuja kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa wa China Afisa wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Bwana Zhang Zhiqiang alisema juhudi zilizochukuliwa na  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea mazingira mazuri madaktari hao zimewawezesha kutekeleza vyema majukumu yao kwa  kiwango kikubwa.
Bwana Zhang alisema uungwana huo utabakia kuwa chachu ya upendo kati ya Madaktari hao na Zanzibar itakayoendelea kudumu ndani ya nyoyo zao katika uhai wote wa maisha yao.
Timu hiyo ya Madaktari Mabingwa 12 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China ikiongozwa na Dr.  Lu Jian Lian inatarajiwa kuondoka Nchini Tarehe 18 mwezi ujao wa Juni kurejea nyumbani  mara baada ya kuwasili Timu nyengine mpya katika ule mpango maalum wa Wataalamu wa afya wa China kuja kutoka huduma za afya Zanzibar.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa mazungumnzo na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik hapo ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliiomba Norway kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kitaaluma katika sekta ya Uvuvi wa Bahari Kuu kwa vile Nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika eneo hilo.
Alisema Zanzibar imezunguukwa na bahari pembe zote rasilmali ambayo ikitumika vyema inaweza kusaidia kutoka ajira katika kiwango kikubwa zaidi na kusaidia pia uchumi wa Taifa sambamba na kupunguza umaskini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania kwamba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika azma yake ya kuimarisha uchumi sekta ya Uvuvi imepewa msukumo na kinachoangaliwa zaidi wakati huu ni kuwashawishi washirika wa Maendeleo na Nchi hisani kuunga mkono sekta hiyo.
Aliipongeza Norway kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono harakati za maendeleo za Zanzibar kupitia Shirika lake la Maendeleo la Norad ambapo Zanzibar tayari inaendelea kufaidika  na sekta za nishati na mawasiliano ya bara bara kutokana na mchango wa Taifa hilo Hisani.
Naye kwa upande wa Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klepsvik alimuhakikishia Balozi Seif kwamba  Nchi yake itahakikisha kwamba sekta zilizopata msaada wa Nchini hiyo zitaendelea kuungwa mkono zaidi.
Balozi Ingunn alizitaja baadhi ya sekta  zilizoungwa mkono na Serikali yake hapa Zanzibar kuwa ni pamoja na Sekta ya mawasiliano ya Bara Bara Kisiwani pemba pamoja na Sekta ya Nishati Vijijini. 

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/5/2013.

Michezo:-
Wapenzi na Wanachama wote waanzilishi wa iliyokuwa Klabu Maarufu ya mchezo wa soka hapa Zanzibar Timu ya kandanda ya Small Simba wanatarajiwa kukutana kesho asubuhi katika azma ya kutaka kuifufua tena Timu hiyo.
Kikao cha kutafakari mustakabali wa timu hiyo kinatazamiwa kuwa wazi kikikaribisha pia  wadau wa klabu hiyo  ambacho kitafanyika katika jengo la CCM la Jimbo la Kikwajuni liliopo hapo mnazi Mmoja Mjini Zanzibar majira ya saa 3.00 za asubuhi.
Akikaririwa na vyombo vya  Habari Mmoja wa waanzilishi wa Klabu hiyo maarufu  katika miaka ya 1980 na  90 Dr. Juma Mambi kwa niaba ya Katibu mteulwe wa Klabu hiyo Kaasim Juma alisema mada tatu zitajadiliwa katika kikao hicho.
Dr. Mambi alizijada mada hizo kuwa ni pamoja na Kujua mustakabala wa Small Simba, kufufu ari na hamasa za wapenzi wa Klabu hiyo pamoja na mengineyo yatakayojichomoza katika kikao hicho.
Dr. Mambi aliwaomba pia wana habari kushiriki katika kikao hicho lengo la kutafuta mbinu na njia ya kutaka kurejesha ari na  hamasa ya mchezo wa soka ambao ulikuwa katika kiwango cha juu wakati timu hiyo ikiwa katika Nyanja za Kimichezo.
Timu ya Soka ya Small Simba iliwahi kushika ubingwa na soka wa daraja la kwanza hapa Zanzibar na kutoa upinzani mkali kwa timu za Yanga na Simba za Dar es salaam katika iliyokuwa mashindano ya klabu bingwa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

ATT:-  Habari Maelezo/ waandishi michezo:-
Waandishi wote wa Habari za michezo mnaalikwa katika mkutano huo muhimu ambao uitaanza saa 3.00 kamili za asubuhi katika Jengo la Ofisi ya Jimbo la Kikwajuni iliyopo Mnazi Mmoja Mkabala na lililokuwa Baraza la wawakilishi la zamani Mnazi Mmoja.

Othman Khamis Ame
OMPR - ZNZ
24/5/2013.


Thursday, 23 May 2013


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amtembelea Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kumfariji Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu }




Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } akielezea mkasa uliompata wa kumwagiwa Tindi kali { Acid } mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kumfariji.
Picha na Haasn Issa wa –OMPR – ZNZ.
Press Release:
Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Bwana Mohd Omar Said        { Maarufu Kidevu } anaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindi kali { Acid }  na mtu asiyejuilikana.
Mkasa huo umempata jana usiku mara baada ya kurejea ibada ya sala ya Isha wakati akiendelea na harakati za kutafuta huduma za maji na kumwagiwa tindi kali hiyo iliyoathiri eneo la kifua chek, Bega pamoja na sehemu za jicho la kulia.
Hili ni tukio la tatu kutokea ndani ya mkoa wa mjini Magharibi likiwahusisha aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma pamoja na Katibu wa Fufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.
Sheha huyo wa Tomondo Bwana Mohd Omar Kidevu akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali hapo kumfariji pamoja na kumpa pole alisema alijikuta akimwagiwa tindi kali majira ya saa 2.00 za usiku na mtu asiyemfahamu.
Bwana Mohd Kidevu alisema Mtu huyo alianza kutimua mbio baada ya kufanikiwa kufanya dhambi hiyo kitendo ambacho akalazimika kuomba msaada kwa wasamaria wema lakini hatimae ilishindikana kutokana na kuzidiwa kwa maumivu makali yenye kuchoma kama moto.
Sheha huyo wa Shehia ya Tomondo aliendelea kumfahamisha Balozi Seif kwamba hali yake hivi sasa inaendelea vyema na ameshaanza kupata matumaini kufuatia jicho lake kuanza kuona ingawa bado anakabiliwa na maumivu katika sehemu yake ya usoni. 
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alimuomba Sheha huyo wa Tomondo kuwa na moyo wa subra wakati wa kipindi hichi kigumu cha huduma za matibabu.
Balozi Seif alimuhakikishia Bwana Mohd Kidevu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufuatilia ushauri utakaotolewa na Madaktari kuhusu   tiba ya afya yake na kutoa msaada wowote utakaohitajika ili kuendeleza nguvu za huduma ya tiba yake.
“ Tutafuatilia ushauri watakaotupa Madaktari kuhusu afya yao. Na kama kuna wazo la kukusafirisha iwe Hospitali ya Rufaa Muhimbili au Nje ya Nchi basi sisi kama Serikali tuko tayari  kulitekeleza hilo “. Balozi Seif alimuhakikishia Sheha  Mohd Kidevu.
Akizungumza na vyombo vya Habari nje ya Wodi ya Mapinduzi Kongwe katika Hospitali Kuu ya Mmnazi Mmoja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali  Iddi alisema Serikali Kuu imesikitishwa na vitendo hivi viovu vinavyoleta athari kwa Binaadamu.
Balozi Seif alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuanza kuchipua hapa Nchini ikibeba ufinyu wa imani inaanza kuleta hofu miongoni mwa wananchi katika kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.
Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea na uchunguzi wa kufuatilia matukio hayo na haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwafikisha katika mkondo wa sheria.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/5/2013.




Tuesday, 14 May 2013

UZINDUZI WA KIWANDA  KIPYA  CHA MAJI   ZANZIBAR


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda kipya cha maji ya kunywa hapo maeneo huru amani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifungua pazia kuashiria kukifungua rasmi Kiwanda cjha maji ya Kunywa cha Super Shine Kinachomilikiwa na Kampuni ya Safari yenye Makao Makuu yake Nchini India.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayesimamia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar Mh. Omar Yussuf Mzee akiwa na akiambatana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kukagua baadhi ya sehemu ya KiwandaKipya  cha Maji ya kunywa kiliopo maeneo ya Viwanda Amani Mjini Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiangalia baadhi ya mashine za Kiwanda cha maji ya kunywa kiliopo maeneo huru ya Viwanda yaliopo Amani Mjini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiangalia moja ya sampuli ya chupa ya maji yenye ujazo wa nusu lita ambayo tayari imeshakamilika utayarishaji wake katika kiwanda kipya cha maji ya kunywa kiliopo Maeneo huru Amani.

 Wasanii wa Kikundi cha sanaa Zanzibar wakitoa burdani safi katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda kipya cha maji ya kunywa kiliopo amani maeneo huru ya viwanda.


Balozi Seif akiwa pamoja na baadhi ya viongozi  wakishangiria moja ya nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na kikundi cha sanaa kwenye hafla ya uzinduzi wa kiwanda kipya cha maji ya kunywa kiliopo maeneo huru ya Viwanda Amani

Mkurugenzi na Mmiliki wa Kampuni ya Safari inayomiliki Kiwanda cha maji ya kunywa kiliopo amani maeneo huru Bibi Mala Kalwan akielezea faraja yake kutokana na ukarimu alioushuhudia Zanzibar wakati akijiandaa kuwekeza Vitega uchumi vyake hapa Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Serikali na wale wa Kampuni ya Safari inayomiliki Kiwanda cha maji ya kunywa  hapo amani eneo huru la Viwanda.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri anayesimamia Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Mh. Omar Yussuf Mzee, Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA Nd Salum Khamis na Mmmoja wa Viongozi wa Kiwanda hicho.Kushoto yake ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Safari inayomiliki Kiwadna hicho Bibi Mala Kalwan na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Mh. Nassor Ahmed Mazrui.
Habari na Picha Kutoka  HAssan Issa  na  Othman Khamis Vuga  NewsroomAfisi ya  Makamu wa  Pili wa  Rais-Zanzibar



Tuesday, 7 May 2013

MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDI ATEMBELEA MAJERUHI WA MRIPUKO KATIKA KANISA KATOLIKI ARUSHA





Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia baadhi ya majeruhi wa mripuko wa linalodhaniwa kuwa bomu uliotokea Jumapili iliyopita katika Kanisa Katoliki Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbali mbali Nchini mara baada ya kuwakagua na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha baada ya kujeruhiwa katika mripuko unaodhaniwa kuwa Bomu katika Kanisa Katpoliki la Arumeru Mkoani Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na baadhi ya Viongozi wa Kanisa Katoliki Mkoani Arusha alipofika kuwafariji kufuatia mripuko wa unaodhaniwa bomu wakati Viongozi hao pamoja na waumini wao walipokuwa katika ibada ya Juma pili iliyopita.


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nd. nYerembe Munasa Sabi akitoa Taarifa ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la Mripuko wa unaodhaniwa kuwa Bomu mbele ya Viongozi wa Kanisa Katoliki na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kuwatembelea majeruhi wa mripuko huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Balozi wa Papa Nchini Askofu Mkuu Francisck Pdilla Mjini Arusha.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Askofu Josephat Lebulu alipowatembelea kuwapa pole baada yam ripuko wa Bomu Jumapili iliyopita.
Balozi Seif akisalimiana na Viongozi wa Dini ya Kikristo Mkoani Arusha wakati alipokwenda kuwapa pole kufuatia ajali ya bomu lililotokea Jumapili iliyopita katika Kanisa Katoliki la Arumeru Mkoani Arusha

Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Watanzania kuacha dhana ya kulihusisha tukio la mripuko unaodhaniwa kuwa ni bomu uliotokea katika Kanisa la Kikatoliki Wilayani Arumeru Mkaoni Arusha kuwa lisihushishwe na masuala ya Kidini wala Kisiasa.Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara fupi ya kuangalia mareruhi wa mripuko huo waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha pamoja na kuwapa pole Viongozi pamoja na waumini wa Kanisa lililopata maafa hayo.Balozi Seif alisema Tukio hilo ambalo linadalili zote za Kigaidi limeshitua Taifa na kuwakera Wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar na linafaa kulaniiwa na wapenda amani wote popote walipo.Alifahamisha kwamba hiyo ni fitna inayojengwa katika kuleta chuki baina ya Serikali na Wananchi hasa waumini. Hivyo aliwanasihi Watanzania kuendelea kutulia na wala hakuna haja ya kuanza kutuhumiana ndani ya kipindi hichi kigumu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea fahaja yake kufuatia vyombo vya ulinzi kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wahusika wa mripuko huo wapatao 10 hadi hivi sasa ambao kati yao wane ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja Raia wa Kenya.
Balozi Seif aliwahakikishia wananchi wote pamoja na waumini walioathirika na tukio hilo kwamba Serikali itahakikisha inawashikilia wale wote waliohusika na njama hizo na kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na udhalimu wao huo.

“ Tungeliomba jambo hili baya lisitokezee tena katika Nchi yetu kwani linaonyesha kuleta fitna kati ya Serikali na Wananchi wake “ Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.

Akizungumzia suala la Kidini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali zote mbili zimetoa uhuru wa kuabudu ambao umo ndani ya katiba na kamwe haitavumilia kuona uhuru huo unaingiliwa na watu wachache. Alisema matukio ya hujuma ndani ya majengo ya ibada yamekuwa yakiwapa hofu na wakati mgumu waumini kuendelea na ibada zao za kila siku.“ Hofu hii iliyojengeka miongoni mwa waumini kutokana na hujuma wanazofanyiwa inawapa wakati mgumu wa kuabudu waumini hao “. Alifafanua Balozi Seif. Akitoa shukrani kwa niaba yake na waumini wenzake Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Askofu Josephat Leburu alisema waumini wa jimbo hilo wamepata fafaja kubwa kufuatia ujio wa Viongozi mbali mbali wa Kitaifa waliofika kuwapa pole.

Askofu Josephat alisema moyo huu ulioonyeshwa na Vionmgozi wa Kitaifa umetoa sura sahihi uliyoonyesha ushirikiano wa karibu yao yao na WEananchi wanaowaongoza.Hata hivyo Viongozi hao wa Kidini waliiomba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi kuendelea kutoa Taarifa kadri hatua zinavyochukuliwa za kukabiliana na tukio hilo waliloliita la kigaidi.Walisema hatua hiyo itasaidia sana kupunguza joto la waumini wao ambalo wakati mwengine hufiki maamuzi ya kutaka kuchukuwa hatua mikononi mwao wakati wanapokabiliwa na matukio ya hujuma dhidi yao.Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Nd. Nyerembe Munasa Sabi akitoa ufafanuzi wa baadhi ya changamoto za waumini hao alisema Serikali Kuu kupitia, Mkoa na Wilaya hiyo inaendelea na juhudi za kuwasaka wale wote waliohusika la mripuko huo.Nd. Nyerembe alifahamisha kwamba hadi sasa watuhumiwa kumi wameshatiwa mbaroni kwa msaada wa wananchi wema ambapo kati yao wane ni raia wa Saudi Arabia na Mmoja Raia wa Kenya.Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kwamba tukio hilo la mripuko ni ishara ya ugaidi unaojenga chuki ambao umeandaliwa katika mazingira ya kitaalamu zaidi.

Aliwanasihi Viongozi na Waumini wa Kikristo Mkoani humo kuendelea kuwa wastahamilivu wakati Serikali kuu inajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kuepusha mgawanyiko miongoni mwa Wananchi.Ndugu Nyerembe Munasa Sabi pia alikemea tabia ya baadhi ya wana siasa kuanza propaganda ya kulinasbisha tukio hilo kuwa na uhusiano na Chama cha siasa.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Arumeru alieleza kuwa hadi sasa Mripuko huo ulisababisha vifo vya watu watatu, na wengine 66 kujeruhiwa ambapo mkapa muda huu watu 24 wamesharuhusiwa kurejea nyumbani na wengine 34 wanaendelea kupata huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Arusha.

Othman Khamis Ame
Vuga Newsroom
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar7/5/2013.


            SHEREHE ZA KUKABIDHI MCHANGO WA  VIKUNDI  VYA USHIRIKA  WA  WAWANAWAKE 



 WANAUSHIRI wa Vikundi  vya Ushirika vya Wanawake Wilaya ya Chake Chake Pemba wakimsikiliza Mkle wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Balozi Seif, akiwahutubia katika sherehe za kukabidhi mchango uliotolewa na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein, Mama Asha Balozi na Wake wa Wawakilishi na Wabunge wa CCM, makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Makumbusho Chakechake




MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Balozi Seif, akiwahutubia Wanaushirika wa Vikundi vya Wanawake Wilaya ya Chakechake, baada ya kukabidhi misaada iliotolewa na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein, Mama Asha Balozi na Wake wa Wawakilishi na Wabunge kwa ajili ya kuegeze mtaji wa Ushirika wao.



MKE wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Balozi Seif, kushoto akimkabidhi fedha kiongozi wa Kikundi cha Ushirika  cha Wanawake wa Tujiendeleze kwa Maisha Bora Hadia Omar, shiliki laki nne kwa kikundi chao.



WANACHAMA vikundi vya Ushirika vya Wanawake wakishangilia kwa kubeba zawadi zao kumpelekea Mama Asha Balozi .

Picha  na Habari kutoka  
Hassan Issa   na  Othman Khamis
Vuga newsroom
OMPR  - ZANZIBAR

Sunday, 5 May 2013

   KUTOKA  VUGA  NEWSROOM


Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners ya Mjini Salala Nchini Oman Bwana li Omar Al-Sheikh akizunguza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi watano wa Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners ya Mjini Salala Nchini Oman uliofika ofisini kwake mapema asubuhi.





Balozi Seif akiiomba Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners ya Mjini Salala Nchini Oman kupitia Mwakilishi wake Bwana Ali Omar Al-Sheikh kutumia fursa zilizopo za rasilmali Zanzibar kuwekeza vitega uchumi vyao Nchini.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Viongozi watano wa Kampuni ya Kimataifa ya Kibiashara ya Shanfar & Patners ya Mjini Salala Nchini Oman baada ya mazungumzo yao yaliyohusu suala la uwekezaji hapa Nchini.

Picha na Hassan Issa na Mwandishi  Othman Khamis  - 
Vuga  Newsroom– OMPR – ZNZ.

ZIARA YA CHAMA YA MAKAMO MWENYEKITI WA CCM AMBAE PIA NI RAIS WA ZANZIBAR - MKOA WA KASKAZINI UNGUJA


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif akizungumza na Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Bibi Catherine Peter Nao wakati wa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Shein Mkoa Kaskazini Unguja.Kulia yao ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Ndugu Haji Juma Haji.




Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Tifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Makamu Mwenyekiti wa Chama hIcho Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheinn wakati wa ziara yake ya Kichama Mkoa wa Kaskazini Unguja.




Dr. Ali Mohammed Shein na Viongozi wengine wa Chama cha Mapinduzi wakikagua baadhi ya sehemu za Tawi la CCM Kwa Gube Mfenesini akiwa katika ziara ya Kichama ya siku mbili Mkoa wa Kaskazini Unguja.



Mkamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akitoa kadi kwa wanachama wapya wa CCM hapo tawi la CCM Kwa Gube Mfenesini akiwa katika ziara ya siku mbili ya Kichama Mkoa Kaskazini Unguja.






Wanachama wapya wa CCM Tawi la Kwa Gube wakila kiapo mara baada ya kukabidhiwa kadi zao na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein.




Dr. Shein, Balozi Seif pamoja na Viongozi wengine wakuu wakishangiria hamasa ya Viongozi wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja kwenye Mkutano wa Majumuisho wa ziara ya Dr. Shein Mkoani humo.




Baadhi ya Viongozi wa CCM Mkoa Kaskazini Unguja wakiwa katika Kikao cha Kutathmini ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Hicho Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein hapo ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini B.






Mzee wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kaskazini Unguja Ali Ameir Mohd akitoa neon la shukrani baada ya kumalizika kwa mkutano wa majumuisho kufuatia ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Sheni Mkoani humo.




Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai wakibadilisjhana mawazo wakati wa ziara ya siku mbili ya Kichama ya Dr. Shein Mkoa Kaskazini Unguja



Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akiweka jiwe la msingi la Tawi la CCM Zingwe zingwe wakati wa ziara yake ya Kichama Mkoa wa Kaskazini Unguja.



Picha na Hassan Issa wa
Mwandishi    ni  Othman Khamis    
 VUGA  NEWSROOM - OMPR - ZNZ



Thursday, 2 May 2013

              MAADHIMISHO YA MEI MOSI  ZANZIBAR


Mhe Makamo wa  Pili wa Rais wa    Zanzibar  Balozi   Seif Ali Iddi akihutubia katika maadhimisho  ya  Mei Mosi yaliofanyika  katika kiwanja  cha Amman


Mwakilishi wa shirila la bandari Zanzibar baada ya shirika hilo kuteuliwa kuwa shirika bora katika mashirika ya umma mwaka huu.


Mwakilishi wa Hospilai ya Al Rahma akipokea zawadi baada ya kuchaguliwa kuwa taasisi binafsi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani hapo uwanja wa amani mjini Zanzibar.





















Msanii wa kizazi kipya Iddi Thabit (IT) akiimba wimbi maalum katika  sherehe   hizo.
Picha no Hassana Issa wa  - (Vuga  Newsroom)  - OMPR – ZNZ.




Press Release:-
Ukosefu wa uaminifu pamoja na kutofanya kazi kwa bidii miongoni mwa    Wafanyakazi ndio hali inayowafanya  baadhi ya wawekezaji kutoka nje ya Nchi kuwaajiri wageni na kusababisha hali ya mazingira ya ajira kwa Wazanzibari kutokuwa  nzuri.
Hivyo umuhimu wa wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii  na maarifa utaendelea kuhitajika ili kukuza tija kazini sambamba na kurejesha imani kwa taasisi zinazotoa ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Sheni wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi zilizofanyika katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema kumekuwa na minong’ono kwa baadhi ya taasisi  na makampuni yanayotowa ajira hasa yale yaliyomo ndani ya sekta ya Utalii dhidi ya baadhi ya Wanzibari na matokeo yake fursa hiyo huchukuliwa na wafanyakazi kutoka nchi jirani.
Alisema pamoja na kwamba Serikali ilijiwekea lengo la kupunguza tatizo la ukosefu  wa ajira kutoka asilimia 7% mwaka 2007 hadi asilimia 4% mwaka 2010 lakini bado changa moto hilo linaendelea kuliumiza kichwa Taifa.
Balozi Seif  aliwataka Vijana kubadilika kwa kujenga utamaduni wa kujiajiri wenyewe kupitia vyama vya ushirika vya uzalishaji mali pamoja na kuunda saccos ili kujipatia tija  itakayotoa unafuu.
“ Uzoefu unaonyesha kuwa Vijana wetu wengi wamekosa utamaduni wa kufanya kazi katika sekta binafsi. Matokeo yake vijana wetu huacha kazi badala ya kipindi kifupi cha kuajiriwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana wa je ya nchi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wafanyakazi wote nchini kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha maslahi yao ikiwemo mishahara, maposho, mazingira mazuri ya kufanyia kazi na maslahi mengine kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.
Alisisitiza kwamba kamwe Serikali Kuu haitaweza wala kuthubutu hata siku moja kuwatelekeza wafanyakazi waliomo ndani ya Taasisi zake kwa vile muda wote inatambua kilio cha wafanyakazi wake kikubwa kiliwa suala la maslahi bora.
Alisema suala la kulindwa na kupewa kwa maslahi wafanyakazi wa sekta ya umma kulingana na kazi wanazozifanya litapewa msukumo wa hali ya kipekee ili kujenga mazingira ya upendo na kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo Balozi Seif aliwakumbusha wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kazini huku wakizingatia kwamba hakuna haki isiyokuwa na wajibu,akimaanisha kwamba haki na wajibu ni watoto pacha.
Akizungumzia suala la migogoro makazini Balozi Seif alisema  kuwepo kwa kitengo cha usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya mambo ya kazi ni hatua muhimu katika kupunguza migogoro ya kazi na mrundikano wa kesi mahakamani.
Alifahamisha kwamba kitengo hicho kimesaidia kuimarisha uhusiano mwema kazini kati ya waajiri na waajiriwa wakati inapotokea hitilafu ambapo hupata wasaa wa kujadiliana pamoja na hatimae kufikia usuluhishi unaofaa.
Akitoa salamu wa Shirika la Kazi Duniani { ILO } Naibu Mkurugenzi  wa Shirika hilo kwa Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda  Bibi Hopolang Phororo  alisema ukosefu wa ajira kwa vijana, changamoto nyingi wanazozipata katika kutafuta kazi zenye staha ni masuala muhimu ya kuzingatia kwani yanaweza kuleta hatari na kuacha makovu ya kudumu katika Jamii.
Bibi Hopolang Phororo alisema Mataifa wanachama yanatakiwa kushughulikia kwa umahiri kipaumbele cha maendeleo ya kimataifa ambacho ni uzalishaji wa ajira hasa kwa vijana zisizolazimishwa wala kubaguliwa.
Bibi Hopolang aliihakikishia Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwamba Shirika la Kazi Ulimwenguni litaendelea kuunga mkono harakati za Taifa hili katika kuimarisha viwango vya ajira Nchini Tanzania.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar {ZANEMA} Ndugu Salahi Salim Salahi aliikumbusha Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kutafuta mbinu za kujenga uwezo wa vijana wa kuwa na taaluma itakayoweza kujiuza wenyewe.
Nd. Salahi alisema waajiri wengi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la kuwapata waajiriwa hasa kundi kubwa la vijana wenye uwezo kamili wa kuwajibika taaluma.
Mkurugenzi huyo wa Jumuiya ya waajiri Zanzibar alishauri kupitiwa upya kwa mitaala iliyopo hapa nchini ili itengeneze mazingira yatakayotowa fursa kwa vijana anapomaliza masomo yao kuwa na uwezo kamili wa kuingia katika soko la ajira hasa lile na afrika Mashariki.
Mapema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama huru vya Wafanyakazi Zanzibar     { ZATUC } Maalim Khamis Mwinyi  Mohd amesifu hatua kubwa zilizofikiwa na Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuunda kanuni za ajira pamoja na utatuzi wa matatizo ya wafanyakazi.
Maalim Khamis alisema kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyotekelezwa na Serikali kuu ambayo yalikuwa  kilio cha muda mrefu miongoni mwa wafanyakazi walio wengi hapa Nchini.
Maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi Duniani { Mei Mosi } yametanguliwa na maandamano ya wafanyakazi kutoka taasisi za Umma, sekta binafsi pamoja na vijana wa mapiki piki wakiongozwa na Bendi ya Chipukizi.
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa zawadi ya fedha taslim kwa wafanyakazi bora wa taasisi za umma na zile binafsi pamoja na vyetu maalum kwa Taasisi bora.
Ujumbe wa mwaka huu wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duiani mei mosi unasema Katiba Mpya izingatie  Haki, Maslahi na usawa kwa wafanyakazi Nchini.


Othman Khamis Ame
(Vuga  Newsroom)
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/5/2013.