Sunday, 7 July 2013

Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Idara ya Biashara ya Jimbo Heilongjiang Nchini China Bwana Li Leyu amtembelea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa  katika Idara ya Biashara ya Jimbo Heilongjiang Nchini China Bwana Li Leyu Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Bwa Li Leyu akiuongoza Ujumbe wa Viongozi wane wa Idara hiyo upo Zanzibar kati a azma ya Idara yao kutaka kuwekeza Vitega Uchumi katika Viwanda vya mazao ya Baharini { Kamba na Samaki }.

Press Release:
Idara ya Biashara kupitia kitengo chake cha ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa katika Jimbo la Heilongjiang Nchini China inakusudia kuwekeza katika sekta ya Viwanda vitakavyozalisha  Mazao ya Baharini hatua ambayo imekuja kufuatia mazingira mazuri yaliyopo ya Bahari ya Hindi iliyovizunguuka Visiwa vya Zanzibar.
Mkuu wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kimataifa  katika Idara ya Biashara ya Jimbo hilo Bwana Li Leyu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Li Leyu aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Idara hiyo alisema kwamba mradi huo wa uwekezaji utakwenda sambamba na utoaji taaluma kwa wavuvi wadogo wadogo ukilenga kuwa na  uzalishaji wa kimataifa  kwa kushirikisha pande zote mbili.
“ Mradi wetu utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kutoa ajira zisizopunguwa mia tano kwa wavuvi wazalendo na ndio maana tukasisitiza zaidi suala la Taaluma kabla ya kuanza kwa mradi na hatimae uzalishaji. Tumekusudia Mradi wetu uwe wa mfano, bora na wa mwanzo katika mwambao wa Afrika Mashariki “. Alifafanua Bwana Li leyu.
Mkuu huyo wa Divisheni ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Nje katika Idara ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiag Nchini China Bwana Li alifahamisha kwamba wataalamu wa kufanya utafiti wa kuendesha mradi huo watafika Nchini mara baada ya kuridhiwa pamoja na kukamilika kwa taratibu zilizowekwa za uwekezaji Nchini.
Bwana Li Leyu alieleza kuwa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango kikubwa cha mazao ya Baharini ikiwemo samaki na Kamba mazao ambayo yana pato kubwa katika masoko ya kimataifa hasa eneo la Bara la Asia.
Alieleza  kwamba mradi huo mkubwa ulioelekezwa ndani ya kanda ya Afrika Mashariki ukiilenga zaidi Zanzibar unaweza kuwa tayari ndani ya kipichi cha kati ya miaka miwili hadi mitatu tokea utapoanza ujenzi wa Viwanda vyake.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliushukuru Uongozi wa Idara hiyo ya Biashara ya Jimbo la Heilongjiang Nchini China kwa mtazamo wake wa kuiona Zanzibar ndio mahali panapostahiki kuwekezwa mradi huo wa mazao ya Baharini.
Balozi Seif alisema huo ni mradi mzuri utakaoleta faraja kwa Serikali katika harakati zake za kuongeza ajira kwa wananchi na hasa lile kundi kubwa la vijana wanaomaliza masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Idara ya Baishara ya Jimbo la Heilongjiang kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar   itakuwa tayari kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuona mradi huo unasimama na kufanya kazi hapa Zanzibar.
“  Bidhaa za Kamba na Samaki tumekuwa tukizishuhudia ughali wake katika masoko ya Kimataifa. Sasa kuwepo kwa mradi huu hapa Nchini kutasaidia kuongeza pato la Taifa na kupunguza ukali wa maisha kwa wavuvi watakaobahatika kufanya kazi katika kiwanda hicho “. Alisisitiza Balozi Seif.
  
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi afanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli Mpya ya Daraja la Saba { Grand Hayert }


 Ramani halisi  itakavyokuwa Hoteli ya Daraja la Saba ya Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s inayojengwa katika eneo la ilipokuwa Starehe Club Pembezoni mwa Fukwe ya Forodha Mchanga.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ramani ya ujenzi wa Hoteli ya Daraja la Saba hapo Forodha Mchanga inayojengwa na Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s.


Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, makazi, Maji, Nishati na Madini Nd. Al - Khalil Mirza akimsisitiza Mwakilishi wa Kampuni ya ASB Holding’s Bwana Ali Al-Bwardy  kuzingatia kufuatwa kwa taratibu za hifadhi ya Mji Mkongwe kwenye ujenzi wa Hoteli yao iliyopo eneo la Forodha Mchanga mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.Pembeni yao ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Wafanyakazi wa Ujenzi wa Hoteli ya Daraja la Saba iliyopo maeneo ya Forodha Mchanga hawapo Pichani wakati alipofanya ziara fupi kukagua ujenzi huo.Pembeni yake ni Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa itayoendesha Hoteli hiyo ya ASB Holding’s Bwana Ali Al- Bwardy.


 Jengo la Hoteli ya Kimataifa ya Daraja la Saba la Kampuni ya ASB Holding’s linalojengwa na Kampuni ya Kimataifa ya CRJ ya China liliopo katika eneo la Forodha Mchnga.


Press Release:Hoteli Mpya ya Daraja la Saba { Grand Hayert } inayomilikiwa  na Kampuni   ya Kimataifa ya ASB Holding’s ambayo inajengwa katika eneo lililokuwa Starehe Club ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inatarajiwa kufunguliwa rasmi katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar za mwaka 2014.Ujenzi wa Hoteli hiyo unaofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya CRJ kutoka Nchini china unatazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ambapo zaidi ya ajira za wazalendo kati ya 60 na 100 zitatolewa wakati itakapoanza kazi zake rasmi.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli hiyo ili kupata sura halisi ya Ujenzi huo kufuatia kupokea malalamiko mengi kutoka kwa  baadhi ya watu na taasisi dhidi ya ujenzi huo kwa dhana ya kukiukwa kwa matakwa ya hifadhi ya Mji Mkongwe.Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Balozi Seif kwamba Jengo la Hoteli hiyo litakalokuwa na ghorofa tatu linazingatia kubakisha sura ile ile ya haiba ya nyumba zilizomo ndani ya Mji mkongwe.Nd. Sarboko alisema Uongozi wa Kampuni ya ASB utapaswa pia kuzingatia ujenzi wa ukuta maalum wa mita tatu kama yalivyo majengo mengine ya Mji mkongwe yaliyo pembezoni mwa bahari ili kusaidia kunusuru athari yoyote ya maji, Mazingira  au matukio ya dhoruba  yanapotokea wakati wowote.Alisema hatua zote hizo zinachukuliwa sambamba na matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Elimu sayansi na Utamaduni { UNECSO } juu ya hifadhi ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika makubaliano ya Hifadhi ya Kimataifa.Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s Bwana  Ali Al-Bwardy alifahamisha kwamba Uongozi wa Hoteli hiyo utazingatia matumizi bora na sahihi ya fukwe iliyopo pembezoni mwa Hoteli hiyo bila ya kuathiri matumizi ya Wananchi kwa utaratibu maalum utakaoandaliwa.Bwana Ali Al – Bwardy alisema uongozi wa Kampuni yake ya ASB  unaelewa kwamba eneo la fukwe ni la Serikali ambalo Jamii inafursa ya  kulitumia wakati wowote wanapolihitaji kwa shughuli zao za kila siku ikiwemo michezo au hata mapumziko.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake mara baada ya kuangalia harakati hizo za ujenzi alieleza kuridhika kwake na taratibu za ujenzi zinazochukuliwa na Kampuni hiyo ya ASB Holding’s.Balozi Seif alisema kwamba amechukuwa hatua hiyo ya kukagua ujenzi huo kufuatia malalamiko aliyokuwa akiyapokea kutoka kwa baadhi ya Watu na Taasisi tofauti yakiishutumu  Kampuni hiyo kukiuka taratibu za ujenzi ndani ya eneo la hifadhi ya Mji Mkongwe.“ Nimeridhika na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Kampuni yenu ya ASB Holding’s katika ujenzi huu wa Hoteli kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe. Sina shaka nao na mnaweza kuendelea na Ujenzi kama kawaida. Sasa kama kuna asiyeridhika mnaweza kumuelekeza kuja  kwangu “. Alisisitiza Balozi Seif.Ujenzi wa Hoteli hiyo  ya Daraja la Saba { Grand Hayert } iliyopo baina ya Tembo Hoteli  na Nyumba Iliyokuwa ikiandikisha Vizazi na Vifo ya Mambo Msiige itakapomalizika itakuwa na uwezo wa kulaza wageni wapatao 65 kwa wakati mmoja. 
 Othman Khamis Ame:Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar



ZIARA YA MHE RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI NCHINI CHINA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,katika ukumbi wa Mikutano wa World Hotel China,ambapo alifanya mazungumzo na kutiliana saini Makubaliano masuala ya Biashara.

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mw3amamwema Shein,akiangalia kitabu wakati alipotembelea makumbusho ya kihistoria katika Mji wa Beijing  nchini China,katika ziara ya Kiserikali kwa mualiko wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,(kulia) Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake Zanzibar,Bibi Chen Qiman.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi wa Maendeleo Omar Yussuf Mzee,akibadilishana Hati ya saini ya Mikataba ya uhusiano wa biashara na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,baada ya kutilianan saini katika ukumbi wa mikutano wa China World Hotel.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiuliza suala kwa waongozaji na watoa maelezo katika sehemu za kihistoria zenye kumbukumbu nyingi,zinazopelekea wageni wa aina tofauti kutembelea katika mji huo wa Beinjing nchini China.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akipata maelezo wakati alipotembelea sehemu za Kihistoria zilizopo katika mji wa Beijing nchini China kiwa katika ziara ya kiserikali na ujumbe wake.

Pichani inaonekanwa  moja wapo ya Majengo yaliyokuwemo katika Eneo kubwa sana la kumbukumbu za Kihistoria katika Mji wa Beijing,ambapo wananchi wa China wakiwa na ukarimu wa aina yake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifuatana naMkewe mama mwamamwema Shein,katika viwanja vya Makumbusho ya Kihistoria nchini Nchini China pamoja na  ujumbe waliofuatana nao katika ziara ya kiserikali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akifuatana na ujumbe wake wakitembelea sehemu mbali mbali za  Kihistoria zilizopo katika makumbusho ya Mji wa  Beijing nchini China kiwa katika ziara ya kiserikali.

Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mw3amamwema Shein,akiangalia kitabu wakati alipotembelea makumbusho ya kihistoria katika Mji wa Beijing  nchini China,katika ziara ya Kiserikali kwa mualiko wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,(kulia) Balozi Mdogo wa China anayefanyia kazi zake Zanzibar,Bibi Chen Qiman.

.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa tatu kusoto) pamoja na ujumbe aliofuatana nao akiuliza suala kwa waongozaji na watoa maelezo katika sehemu za kihistoria zenye kumbukumbu nyingi,zinazotembelea na wageni mbali mbali  katika Mji huo wa Beinjing nchini China,akiwa katika ziara ya Kiserikali ya siku saba.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mashamba yote ya Mikarafuu na Minazi ya Serikali yaamua kuwa kuanzia sasa yatakuwa yakishughulikiwa na Wziara ya Kilimo na Mali Asili


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi SDeif Ali Iddi akikagua shamba la Minazi la Serikali la ekari 45 lililo chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi linakabidhiwa kwa Wizara ya Kilimo kwa vile lipo katika Ukanda wa Utafiti wa Kilimo hapo katika Kijiji cha Tumbe Mkoa Kaskazini Pemba.

Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asili  zisizorejesheka Pemba Nd. Said Juma Ali akielezea hatua zilizochukuliwa na Wizara ya kilimo katika kuotesha minazi kwenye eka 10 zilizomo ndani ya shamba la Serikali la ekari 45 liliopo katika Kijiji cha Tumbe Kaskazini Pemba.


Sheha wa Shehia ya Micheweni Mjini Bwana Dawa Juma Mshindo akielezea changamoto wanazopambana nazo Masheha Kisiwani Pemba mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliokutana nao katika Ukumbi wa Chuo cha Amali Kiliopo Vitongoji Chake chake Pemba.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa uwamuzi kwamba Mashamba yote ya Mikarafuu na Minazi ya Serikali yaliyokuwa chini ya Usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia sasa yatakuwa yakishughulikiwa na Wziara ya Kilimo na Mali Asili.
Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa uamuzi huo wa Serikali wakati akizungumza na Masheha wote  wa Mikoa Miwili ya Pemba hapo katika ukumbi wa Chuo cha Amali Vitongoji Chake Chake Pemba.Balozi Seif alisema wakati suala la Ardhi litaendelea kubakia Wizara ya Ardhi amewaomba Masheha ambao maeneo yao yamo Mashamba ya Serikali  ya Mikarafuu na Minazi na hadi sasa hayajahakikiwa watoe Taarifa kwa Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo Pemba au Kiongozi yeyote atakayewekwa kwenye zoni.Alisema udhibiti wa mapato yanayotokana na mazao yaliyomo kwenye baadhi ya mashamba ya Serikali yalikuwa yakileta mgongano kutokana na Mashamba hayo kushughulikiwa na Wizara mbili tofauti.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza Masheha wa shehia mbali mbali Kisiwani Pemba kwa juhudi zao za kusaidia uhakiki wa mashamba ya Serikali yaliyomo kwenye shehia zao.Akizungumzia suala la udhibiti wa ukataji onyo wa Misitu Balozi Seif aliwakumbusha Masheha hao kuhakikisha kwamba wimbi la ukataji ovyo wa Miti unadhibitiwa.“ Kijani ya Pemba tunataka ibakie kama kawaida na hili litafanikiwa iwapo wana jamii pamoja na masheha watashirikiana katika udhibiti wa ukataji ovyo wa misitu  “.  Alisisitiza Balozi Seif.Wakielezea changamoto zinazowakabili baadhi ya Masheha hao walisema mazingira duni wakati wanapostaafu utumishi wao pamoja na mfumko wa hujuma wanazofanyiwa masheha limekuwa tatizo kubwa linalopunguza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.Masheha hao waliiomba Serikali Kuu kujenga mazingira yatakayowawezesha kupatiwa mikopo ya vyombo vya usafiri ili kurahisisha kazi zao masuala ambayo Balozi Seif aliahidi kwamba Serikali itayazingatia na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.“  Ninazichukuwa changamoto zenu zote zinazowakabili ambazo ni za msingi kabisa na sisi kama Serikali tutazizingatia na kuona namna gani tunazipatia ufumbuzi unaofaa. Tunaelewa kwamba nyinyi masheha ni sehemu ya Serikali “. Balozi Seif alikuwa akijibu baadhi ya changamoto za masheha hao.Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikagua shamba la Mikarafuu liliopo  Kijiji cha Kinyasini Mtambwe la Ekari Tisa lambalo lilikuwa  chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi na kupongeza hatua iliyofikiwa ya usafishaji wa shamba hilo lililokuwa katika hali mbaya.Pia aliangalia shamba la Mikarafuu la Daya Mtambwe linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo lenye Ekari zaidi ya 37 ambalo limeathirika kutokana na maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ambapo jumla ya miti 290 ya mikarafuu ililazimika kukatwa kutokana na ujenzi huo.Baadaye Balozi Seif alikagua shamba la Minazi la Tumbe ambapo Uongozi wa Wizara ya Ardhi unalikabidhi shamba hilo la ekari 45 kwa Wizara ya Kilimo kwa vile liko katika eneo la Ukanda wa Utafiti wa Kilimo.Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asili  zisizorejesheka Pemba Nd. Said Juma Ali alimueleza Balozi Seif kwamba Ekari kumi tayari zimeshaoteshwa minazi mipya ya asili { East Africa }.Nd. Ali alisema kituo cha Utafiti wa Kilimo Pemba kinaendelea na harakati za kurejesha minazi ya asili kwa kuotesha mbegu zitakazouzwa kwa wakulima katika maeneo mbali mbali ili kuziba pengo la minazi mipya ambayo uzalishaji wake huchukuwa kipindi kifupi.Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisisitiza kwamba zao la nazi bado linabaki kuwa na tija katika pato la taifa na mkulima binafsi.Balozi Seif aliwagiza watendaji  wa Sekta ya Kilimo kupanga utaratibu maalum utakaowasaidia wakulima Taaluma itakayowapa njia na fursa ya kuendeleza kilimo hicho kwa ufanisi mkubwa.“ Mnazi ni miongoni mwa mti uliobarikiwa kuwa na sifa na vitu vyake kutumika katika mambo mbali mbali tukitolea mfano Kifuu, usumba, makosi, nazi, makuti, madafu pamoja na kigogo chake kwa ajili ya utengenezaji wa mapambo ya samani “. Alifafanua Balozi Seif.Naye kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu Hemed Salum alisema Mashamba mengi ya Mikarafuu na Minazi ambayo yalikuwa chini ya Usimamizi wa Wizara hiyo ni yale ambayo waliopewa na Serikali wamefariki dunia au kuhama Nchini.Ndugu Hemedi alifahamisha kwamba mashamba hayo ni miongoni mwa zile eka tatu tatu zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
 Othman Khamis Ame.Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

ZIARA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI NCHINI CHINA




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Rais wa China Xi jinping alipofika Ikulu ya Mjini Beijing Nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Serikali wa Jamhuri hiyo.[Picha na Ramadhan Othman,China.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiwatambulisha Viongozi katika ujumbe aliofuatana nao kwa Rais wa Jamhuri ya watu wa China Xi jinping, walipofika Ikulu ya Mjini Beijing Nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Serikali wa Jamhuri hiyo.[Picha na Ramadhan Othman,China.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiwatambulisha Viongozi katika ujumbe aliofuatana nao kwa Rais wa Jamhuri ya watu wa China Xi jinping, walipofika Ikulu ya Mjini Beijing Nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Serikali wa Jamhuri hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(wa nne kushoto)akiwa na ujumbe wake katika mazungumzo na Rais wa China Xi Jinping,(wane kulia) katika Ikulu ya Mjini Beijing Nchini China leo, .[Picha na Ramadhan Othman,China.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Makamo wa Rais wa China Li Yuanchao,katika makaazi yake Mjini Beijing nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Kiserikali wa Nchi hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Makamo wa Rais wa China Li Yuanchao,katika makaazi yake Mjini Beijing nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Kiserikali wa Nchi hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza  la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akiwa katika  mazungumzo na  Makamo wa Rais wa China Li Yuanchao,katika makaazi yake Mjini Beijing nchini China akiwa katika ziara ya mualiko wa Kiserikali wa Nchi hiyo.

MKE WA RAIS WA ZANZIBAR MAMA MWANAMWEMA SHEIN
AKISALIMIANA NA MKE WA MAKAMO WA RAIS WA CHINA MAMA LI
YUANCHAO,ALIPOWASILI KATIKA MAKAAZI YA MAKAMO WA RAIS MJINI BEIJING
NCHINI CHINA KATIKA ZIARA YA KISERIKALI.

MKE WA RAIS WA MAMA MWANAMWEMA SHEIN AKISALIMIANA NA
MAKAMO WA RAIS WA CHINA  LI YUANCHAO,ALIPOWASILI KATIKA MAKAAZI YA
MAKAMO WA RAIS MJINI BEIJING NCHINI CHINA KATIKA ZIARA YA
KISERIKALI,KATIKATI NI RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA
MAPINDUZI DK.ALI MOHAMED SHEIN.

MKE WA MAKAMO WA RAIS WA CHINA MAMA LI
YUANCHAO,AKISALIMIANA NA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA
MAPINDUZI DK.ALI MOAHAMED SHEIN, KATIKA MAKAAZI YA MAKAMO WA RAIS
MJINI BEIJING NCHINI CHINA AKIWA KATIKA ZIARA YA KISERIKALI,





Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kumgharamia mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiongezea taaluma ya fani yoyote ya Udaktari Bingwa


 Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Dr. Salhia Muhsin Ali akitoa maelezo mbele ya Kikao cha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Wanafunzi wanaosoma mafunzo ya Udaktari katika Chuo cha Afya waliopo Wawi Kisiwani Pemba.





Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wanafunzi  12 wa Chuo cha Afya wanaosomea fani ya Udaktari waliopo Kisiwani Pemba.

Rais wa Wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba Ali Omar Khalifa akitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa chuo cha afya waliopo Kisiwani Pemba.

Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa Chuo cha Afya waliopo Pemba Dr. Maria Makdalema akielezea furaha yake kutokana na umahiri wa wanafunzi wake mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipowatembelea kwenye makazi yao Wawi Pemba.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwalimu Mkuu wa Wanafunzi wa chuo cha Afya waliopo Kisiwani Pemba Dr. Maria Makdalema.Pembeni yao ni Afisa Mdhamini Wizara ya AfYA Pemba Mkasha Hija Mkasha na Mkurugenzi  Idara ya Tiba Zanzibar Dr. Salhia Muhsin Ali.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
 Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kumgharamia mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiongezea taaluma ya fani yoyote ya Udaktari Bingwa kwa lengo la kuiondoshea Zanzibar uhaba wa Madaktari.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wakufunzi pamoja na Wanafunzi wa chuo cha afya wanaosomea fani ya Udaktari chini ya Wataalamu wa Cuba hapo Wawi chake chake Pemba.Balozi Seif alisema uwamuzi huo wa serikali umelenga kukidhi ule Mpango wake uliojipangia wa kuimarisha huduma za Afya katika kila umbali wa Kilomita Tano katika Visiwa vya Zanzibar.Alisema Serikali katika kukabiliana na upungufu wa Madaktari bingwa wa fani tofauti imetowa fursa hiyo ili Daktari mwenyewe awe huru kuamua kuongeza ujuzi zaidi katika Nchi na fani aiwezayo huku akilenga kuja kuisaidia Jamii yake mara amalizapo mafunzo hayo.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wanafunzi hao kwa ushiriki wao wa mafunzo hayo ya miaka saba na kuelezea matumaini yake kwamba wamalizapo mafunzo hayo ni kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya Udaktari.
“ Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kuwa na Madaktari 50 kwa mpigo jambo ambalo ni mafanikio makubwa  kwa Serikali “. Alionyesha furaha yake Balozi Seif.“ Historia ya kuanzishwa kwa darasa la Madaktari Zanzibar limetokana na ziara ya Dr. Sheni  Nchini Cuba wakati akiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya  Muungano wa Tanzania katika miaka ya 2008 “. Alisisitiza Balozi Seif.Alifahamisha kwamba wazo hili lililotolewa na Cuba lilikuwa na nia ya kusaidia gharama za usomeshaji ambazo ni kubwa pamoja na udhibiti wa wanafunzi hao ambao wakisoma nje ya nchi wanakuwa na mawazo ya kuikimbia nchini.
Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar ameahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaangalia na kuimarisha mazingira ya walimu pamoja na wanafunzi hao ili waweze kufanikisha lengo lililokusudiwa chuoni hapo.Alisema haipendezi kuona wataalamu hao wamekubali kujitolea kusaidia wananchi wa Tanzania na Zanzi bar kwa ujumla na mazingira yao hasa makazi yanakuwa hayako katika hali ya kuridhisha.Wakitoa baadhi ya changamoto zinazowakabili Wanafunzi hao wa Udaktari walisema upungufu wa vifaa limekuwa tatizo sugu linalorejesha nyuma mafunzo yao ya kila siku.Waliiomba Serikali kupitia Wizara ya afya kuyafanyia kazi matatizo hayo likiwemo pia tatizo la  mtandao wa Internet kwa wakufunzi wao sambamba na usafiri wanakwenda na kurudi kwenye mazoezi hasa wakati wa usiku.
Wanafunzi hao wa Udaktari wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake huo wa kuanzisha mafunzo hayo hapa Nchini ambao utapunguza gharama kubwa.Naye kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Darasa hilo Dr. Maria Makdalema kutoka Nchini Cuba ameelezea furaha yake kutokana na umahiri mkubwa walionao wanafunzi wake.Hata hivyo Dr. Maria alisema `ukosefu wa vifaa vya mazoezi unawapa mazingira magumu wanafunzi hao katika kujipatia mazoezi ya vitendo ambayo ni muhimu katika mafunzo yao.Mapema Mkurugenzi Idara ya Tiba ambae ndie anayeratibu mafunzo hayo Dr. Salhia Muhsin Ali alisema mafunzo hayo ya Udaktari yamejumuisha wanafunzi 50 ambao 38 kati yao wapo Unguja na 12 Kisiwani Pemba.Dr. Salhia alieleza kwamba wanafuzi 38 wa Unguja hivi sasa wako katika hatua ya mwisho kumaliza mafunzo yao ya miaka saba wakati wale 12 wa Pemba wanaingia mwaka wa nne wakiwa katika mkupuo wa tatu.Katika Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alichangia shilingi Laki Tano kusaidia ununuzi wa Vifaa muhimu vidogo vidogo na kuahidi Serikali Kuu kuyafanyia kazi yale matatizo mengine makubwa likiwemo lile la upatikanaji wa Projector.
 Othman Khamis Ame.Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.


Balozi Seif akagua baadhi ya Mashamba ya Serikali ya Miti ya Mikarafuu Mkoa wa Kusini Pemba.


 Balozi Seif akagua baadhi ya Mashamba ya Serikali ya Miti ya Mikarafuu  Mkoa wa Kusini Pemba.  Shamba la Mikarafuu la Serikali lililo chini ya uangalizi wa Mkulima Ali Othman Ali wa Kijiji cha Minazini Wilaya ya Mkoani ambalo liko katika hali nzuri ya kupendeza baada ya kuhuishwa kwake.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza Umuhimu wa Mashamba ya Mikarafuu kulimwa kwa Kitaalamu ili kukidhi mahitaji halisi ya soko la Kimataifa.


 Mkamu Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifurahia mazingira bora ya baadhi ya mashamba ya Serikali ambayo yamekuwa yakihuishwa na baadhi ya wakulima katika maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Pemba.

Press Release:-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa wakulima wa mashamba ya Mikarafuu kukubali kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa Kilimo hicho ili kujenga nguvu za uzalishaji wa uhakika wa zao Karafuu Nchini.Balozi Seif alitoa sisitizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua baadhi ya Mashamba ya Serikali ya Miti ya Mikarafuu ambayo yako chini ya usimamizi wa baadhi ya wakulima ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba.Alisema bado ipo dhana kwa baadhi ya wakulima wa Mikarafuu kujilimbikizia miti mingi ya zao hilo wakiwa na mawazo na fikra za kupata uzalishaji mkubwa zaidi jambo ambalo ni ndodo Kitaalamu.Balozi Seif ambae amekuwa na utaratibu wa kutembelea mara kwa mara mashamba ya Mikarafuu hasa Kisiwani Pemba alieleza kwa kuwa Serikali Kuu inaendelea na Mikakati ya kuimarisha zao hilo Wananchi pamoja na Wakulima wa Kilimo hicho wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.“ Hivi sasa tunapaswa kuwa makini katika uzalishaji wa zao la Karafuu kitaalamu kwani wakati wa kuvuna karafuu mpeta umepitwa na wakati kulingana na mazingira yaliyopo ya soko la Dunia “ Alisisitiza Balozi Seif.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wakulima Abdulla Masoud Abdulla wa Kijiji cha Shungi na Mkulima Ali Othman Ali wa Kijiji cha Minazini kwa uamuzi wao wa kujikubalisha kuyahuisha mashamba ya Mikarafuu ya Serikali yaliyomo katika maeneo yao.Balozi Seif alisema juhudi hizo zimeleta faraja kwa Serikali na kuwaahidi kwamba wao ndio wanaostahiki kupewa upendeleo wa kukodishwa wakati unapofikia msimu wa zao la karafuu.Naye Mkulima Ali Othman Ali wa Kijiji cha Minazini alimueleza Balozi Seif kwamba shamba hilo la Serikalio lilikuwa pori tupu kwa muda mrefu na kulazimika kuliomba kulihuisha kutoka kwa Taasisi husika ili kulirejesha katika hali yake.Mkulima Ali Othman alifahamisha kwamba alilazimika kutumia nguvu za ziada katika kulihuisha shamba hilo lenye ukubwa unaokadiriwa kufikia ukubwa wa Eka moja.Alisema hatua hiyo hivi sasa imempa faraja kwa vile tayari mazao ya Mihogo na Migomba aliyoiotesha ndani ya miti ya Mikarafuu iliyomo ndani ya shamba hilo imeanza kumpatia faida cha chakula sambamba na fedha za kujikimu kwa mambo mengine ya maisha.Naye Mkulima Abdulla Masoud Abdulla wa Kijiji cha Shungi amemuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuzingatia ushauri wa wataalamu katika harakati za kuendesha kilimo hicho.Mkulima Masoud alieleza kuwa ufinyu wa taaluma ya kilimo hicho ndio uliokuwa ukiwapa  ukaidi na kupelekea kuleta mgongano kati yao na wataalamu wa kilimo hicho.Mapema Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Hemed Salum alisema kasi ya wakulima wa Mikarafuu kujitokeza kufyekea mashamba yanayomilikiwa na Serikali hivi sasa imeongezeka zaidi.Nd. Hemed alisema hatua hiyo imeleta faraja kwa Watendaji wa Taasisi yake kupata muda wa kuendelea na majukumu yao ya kawaida badala ya kushughulikia zaidi mashamba hayo.
 Othman khamis Ame:Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar