Jamii ya Kiislamu popote
pale Duniani inalazima kufanya jitihada za makusudi katika kuona inaendelea
kutumia utamaduni wa Kiislam katika muelekeo zaidi wa elimu, mawazo ya maendeleo, biashara, uchumi,
siasa, sayansi na utawala kwa lengo la kuuongezea nguvu ya ziada.
Hatua hiyo itawapa muono wa
kweli watu wengi wasiokuwa waumini wa Dini hiyo kuwaondolea shaka kwamba Uislam
si kundi la waumini ambao sera zao ni vurugu, ugaidi na uuwaji mawazo ambayo
hata baadhi ya Waislam wanachangia bila kuelewa.
Makamu wa
Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal
wakati akilifunga Kongamano la Kimataifa kuhusu Historia ya Ustaarabu wa
Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika ukumbi wa
Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Del Est Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema misikitini
mingi siku hizi imekuwa na hotuba za hamasa, jazba , uchochezi na
kugeuzwa kama majukwaa ya kisiasa badala ya kutolewa hotuba za ibada na
mafunzo ya Kiislam yanayohusu kumuabudu Mwenyezi Mungu na mafundisho yake ya
kupenda kufanya mazuri aliyoyaamrisha na kukataa mabaya aliyoyakataza.
Aliwataka wana jamii wa
Utamaduni wa kiislamu kutafakari kwa makini athari hii iliyojichomoza ambapo
isipozingatiwa na kupatiwa dawa maalum inaweza kumong’onyoa maadili na usaarabu
huo wa Kiislamu.
Alieleza kwamba ipo haja
kwa wakati huu kurejeshwa mfumo wa zamani wa kuifanya Misikiti kuwa ni chimbuko
la elimu ambapo ilikuwa mwalimu hukutwa amezunguukwa na vitabu mbali mbali akiendelea
kutoa elimu ambapo nyumba zao zikijaa baraza kwa kuwa ni sehemu ya
Madrassa.
Alifahamisha kwamba elimu
ya dini ilipewa umuhimu wa kipekee ambapo kila mtoto alijengewa mazingira ya
kupata taaluma ya dini kwanza ikifuatiwa na
ile ya elimu ya dunia
“ Hakukuwa na mtoto ambaye
hakuweza kupata elimu. Vyuo (Madrrassa) vilienea kila pembe. Vijijini ilikuwa
wazazi wakenda kulima mtoto mdogo anapelekwa chuoni kulelewa na wakubwa zake.
Kwa hiyo alianza kupata hisia za elimu akiwa tangu mdogo “.Alifafanua Makamu wa
Raiswa Serikali ya Jmuhuri ya muungano wa Tanzania.
Dr. Bilal alisema kwamba
Utamaduni wa Kiislam umepata nguvu kubwa kutokana na msingi wake wa kurithisha
vizazi kwa njia ya mashairi, maandiko na tungo tofauti, hivyo si kosa kueleweka
kuwa utamaduni huo umejengwa chini ya msingi wa elimu kwa vile chimbuko lake linatokana
na Qur’aan na Sira za Kiongozi wa Dini
ya Kiislamu Mtume Muhammad (SAW).
“ Mbali na athari
zilizojichomoza lakini bado utamaduni wa
Kiislam unabaki kuwa ni utamaduni wa Kiislam. Una miko yake, una sifa zake na
una matumizi yake. Utamaduni wa Kiislam unaweza kujisifu kuwa umeweza kusaidia
ukuaji wa tamaduni nyingi hasa za Ulaya “. Alifafanua Dr. Moh’d Gharib Bilal.
Makamu wa Rais wa Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza kwamba Ukuaji wa lugha ya
kiarabu kuwa ya Kimataifa ya sayansi na uendeshaji Serikali umesaidia kuufanya
Uislam uwe kiungo cha maendeleo chini ya msingi wa Quran inayowaagiza waumini
kutafuta elimu popote pale na muda wote wa umri wao.
Amewapongeza waliowaza
kufanya kongamano kama hili hapa Zanzibar na hasa wakati huu ambao Uislam
unapita katika mitihani mikubwa na kuelezea matumaini yake kutokana na ushiriki
mkubwa wa wajumbe utakaotoa maazimio mazuri yatakayosaidia kupeleka mbele
Uislam na ustaarabu wake.
Akisoma maazimio ya wana
kongamano hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kongamano hilo Dr. Juma Halifa
Juma alisema wana kongamano hilo wamependekeza kuendelezwa kwa makongamano hayo
kila mara.
Dr Juma alisema wana
kongamano hao walisisitiza umuhimu wa kuandikwa kwa Historia ya Uislamu wa
Afrika ya Mashariki na baadaye kuingizwa katika mitaala itakayozingatia mfumo wa
sasa wa Sayansi na Teknolojia.
Walisema umuhimu wa
kubadilishana utafiti kati ya waislamu wa Afrika na wenzao wa mabara mengine
Duniani unafaa kuzingatiwa vyema ili usaidie kuimarisha kasi ya utamaduni na
Dini ya Kiislamu popote duniani.
Wana kongamano hao
wamemshukuru Mfalme Qaboos Bin Said wa Oman kwa uamuzi wa Serikali yake kupitia
Taasisi zake kuandaa kongamo hilo lililotoa fura kwa wanafalsafa, wasomi na
waumini wa dini ya kiislam kupata kubadilishana mawazo.
Naye Mwenyekiti wa mamlaka ya kutunza nyaraka na kumbu kumbu ya Qasri
Nchini Oman Dr. Hamad Moh’d Al – Dhawian Bin Balqas alielezea faraja yake
kutokana na michango mikubwa ya washiriki wa Kongamano hilo hasa wale wenyeji
Zanzibar.
Dr. Hamad alisema utafiti
unaonyesha wazi kwamba Afrika Mashariki ni markaz ya kuleta mabadiliko ya
butamaduni wa ustaarabu wa Kiislamu hapa ulimwenguni.
Akimaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma Shamuhuna alisema Zanzibar imepata heshima
na bahati kubwa ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo jambo ambalo
litaijengea historia ndefu katika masuala ya utamaduni wa ustaarabu wa kiislamu
Duniani.
Jumla ya nyaraka 60
zilijadiliwa katika kongamano hilo lililosheheni wataalamu, wasomi, watafiti na
hata wanavyuoni wa dini ya Kiislamu kutoka pembe mbali mbali za Dunia.
Kongamano hilo la pili la
Kimataifa la ustaarabu wa Kiislamu likitanguliwa na lile llililofanyika Uganda
mwaka 2012 na limeshirikisha Mataifa kumi na saba mbali mbali Duniani likiwa na
lengo la kujitanga za Zanzibar katika Nyanja za Utafiti na Taaluma Kimataifa.
Serikali ya Oman kupitia
ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyara ya Nchi hiyo ndio iliyoandaa
kongamano hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar
4/9/2013.
No comments:
Post a Comment