Wednesday, 18 September 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maendeleo ya uzalishaji wa umeme kupitia miundo mbinu iliyopo hivi sasa kwenye kituo kikuu cha umeme Mtoni.

  Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO} Thabit Salum Khamis akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  mfumo mpya wa huduma za umeme unaotumika katika kituo kikuu cha Umeme kilichopo Mtoni wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya huduma za umeme Nchini.

 Mhandisi  wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Mohd Juma Othman akimfafanulia  Balozi Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo tofauti Nchini.

 Mhandisi  wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Mohd Juma Othman akimfafanulia  Balozi Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo tofauti Nchini.

Mhandisi  wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Mohd Juma Othman akimfafanulia  Balozi Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo tofauti Nchini.

 Press Release

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji Nishati na Madini imeombwa kufikiria njia muwafaka ya kuyauza Majanareta yaliyopo katika kituo kikuu cha kupokelea Umeme Mtoni ili kuwepusha hasara endapo yataendelea kuwepo eneo hilo bila ya matumizi.
Majanareta hayo 30 yalikuwa yakitoa huduma za umeme wa dharura katika kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya nishati ya umeme kutokana na kinanzio chake ilichokuwa ikikitumia wakati huo kutokidhi mahitaji halisi ya huduma hiyo Nchini.
Mhandisi wa Maganareta katika Kituo Kikuu cha Umeme Mtoni Yussuf Reja alitoa ushauri huo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa huduma ya umeme Nchini kupitia miundo mbinu iliyopo katika kituo hicho.
Mhandisi Yussuf Reja alimueleza Balozi Seif kwamba Majanareta hayo yako katika kiwango  bora lakini tatizo kubwa liliopo ni huduma ya mafuta ambayo ni maalum { IDO } na yana  hitaji  gharama kubwa za uendeshaji.
Alisema Shirika la Umeme lilikuwa likipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 16,000,000/-  kwa saa wakati maganareta hayo yalipokuwa yakiwashwa kusaidia huduma za umeme katika kipindi cha mgao wa huduma hiyo muhimu.
Mhandisi Yussuf Reja alifahamisha kwamba shirika la umeme lilikuwa likizalisha umeme kupitia Maganareta hayo kwa  uniti moja yenye  thamani ya shilingi 500/-  ambayo ingelazimika kuwauzia wateja wake uniti moja kwa shilingi 700/- gharama ambayo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.
“ Ukweli uliowazi gharama ya kuyaendesha Maganareta hayo kupitia shirika la Umeme ni kubwa mno na inaweza kuleta maafa kwa shirika hilo endapo yataendelea kutumiwa “. Alitahadharisha Mhandisi Yussuf Reja.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Nd.Mustafa Aboud Jumbe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo tayari imeshapokea mapendekezo ya Shirika hilo kuhusiana na majanareta hayo ya Kituo cha Umeme Mtoni.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Ardhi  Mustafa Jumbe alisema Wizara hiyo inajipanga kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na baadaye kuyawasilisha Serikali kuu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi muwafaka.
Mapema Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Thabit Salum Khamis alisema mfumo mpya wa kisasa wa huduma za umeme kwenye kituo kikuu cha Umeme Mtoni uitwao { SCADA } umewawezesha watendaji wa shirika hilo kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Thabit Salum alimfahamisha Balozi Seif kwamba mfumo huo umepunguza kero kubwa ya kukatika katika kwa umeme kulikokuwa kukitoa usumbufu kwa wananchi walio wengi kwenye maeneo mbali mbali wakati inapotokea hitilafu.
Alieleza kwamba shirika la umeme limekuwa na vituo vikubwa vinavyosambaza umeme kutoka kituo kikuu cha Mtoni kwenda Welezo na Fumba ambavyo vimepangwa kusambaza huduma hiyo na kuacha mfumo wa zamani wa kutumia laini moja tuu.
Kaimu Meneja huyo wa Shirika la Umeme aliongeza kwamba matumizi zaidi ya  umeme huongezeka kutoka Mega walts 33.16 nyakati za asubuhi hadi kufikia  Mega Walts 48.1 kipindi cha  jioni lakini huduma hiyo kuongezeka zaidi katika kipindi cha siku kuu na kufikia hadi Mega Walts 52.
Uwezo wa laini mpya ya umeme uliopo Zanzibar hivi sasa imefikia Mega Walts mia moja  ambapo shirika limekuwa na hakiba ya umeme kwa zaidi ya asilimia 50% mbali ya ile laini ya zamani yenye uwezo wa mega walts 40 kutokana na kuchakaa kwake.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwatanabahisha watendaji wa shirika la umeme kwamba huduma ya umeme hivi sasa imekuwa nyenzo  muhimu ya kiuchumi kwa vile inasaidia kipato cha mwananchi.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa watendaji wa shirika la umeme kufanya kazi zao katika mazingira ya ushindani mfano wa kuwepo  mashirika mengine yanayotoa huduma hizo hapa nchini kwa lengo la kupata ufanisi sambamba na kutoa huduma bora kwa wateja wake.
“ Watendaji lazima mfanye kazi kama mko katika ushindani wa kibiashara  na mashirika mengine licha ya kwamba mpo peke yenu. Kila mkiamka lazima mfikirie mtaongeza vipi wateja wengine wapya “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya athari na hatari ya kutumia mafundi wa mitaani katika kuungiwa huduma hiyo jambo ambalo mara nyingi huleta hasara kutokana na hitilafu zinazojitokeza baadaye.

Monday, 16 September 2013

Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi la Kijiji cha Kiomba Mvua

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Tawi Jipya la CCM la Kiomba Mvua akiongozana na Mwenyekiti wa Tawi hilo Bibi Zawadi Ali Suleiman.

 Mjumbe wa Kamati Kuu yaHalmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif  akikabidhi vifaa kwa ajili ya uendelezaji wa  ujenzi wa Tawi la CCM Kiomba Mvua kwa Mwenyekiti wa Tawi hilo Zawadi Ali Suleiman wakati alipofanya ziafa fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo.

 Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif  Ali iddi akimkabidhi mchango wa fedha Mwakilishi wa Kikundi cha Polisi Jamii cha Kijiji cha Kitope Nd. Bakari Khamis Simai pamoja na ahadi ya fulana kwa ajili ya kikundi chao cha ulinzi.
























Balozi Seif akimkabidhi mchango wa fedha mwakilishi wa Kikundi cha Polisi Jamii cha Kijiji cha Mbaleni Nd. Haji Shaali pamoja na ahadi ya fulana ili kuimarisha ulinzi katika kijiji hicho.

 Press Release:-
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema Viongozi na Wanachama wa CCM wanapaswa  kuendelea kufanya vikao vyao kwa mujibu wa Kanuni na Taratibu za Chama hicho ili kuwa na uhalali kamili wa maamuzi wanayoyatoa kuhusu chama chao.
Kauli hiyo aliitoa wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi  la Kijiji cha Kiomba Mvua na baadaye kukabidhi  vifaa mbali mbali vya uendelezaji ujenzi wa Tawi hilo.
Vifaa alivyokabidhi  Balozi Seif ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope ni pamoja na Mabati, saruji, mchanga kokoto, nondo, mbao pamoja miti kwa ajili ya ukamilishaji wa Tawi jipya la Kijiji hicho.
Hafla hiyo ilikwenda sambamba na Vikundi vya Polisi jamii vya Kijiji cha Kitope na Mbaleni kukabidhiwa Fedha taslimu na ahadi za fulana kwa ajili ya kuimarisha kazi za za ulinzi, mchango na vifaa vyote hivyo vikigharimu jumla ya Shilingi Milioni 4,000,000/-
Balozi Seif alisema maamuzi ya chama kwa mujibu wa kanuni za CCM hutakiwa kufanyika ndani ya vikao halali vya Viongozi na wanachama wenyewe jambo ambalo husaidia kuepusha minong’ono na hata majungu miongoni mwa wanachama wa chama hicho.
Alitahadharisha kwamba maamuzi ya chama hayatolewi bara barani na ndio maana Katiba ya CCM ikasisitiza kujengwa Ofisi bora za chama hicho   na zenye kwenda na wakati  zinazolingana na hadhi ya chama ili wana chama hao wapate fursa nzuri ya kutoa maamuzi kwenye ofisi zao.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliwapongeza wana CCM wa Tawi hilo kwa uamuzi wao wa kujenga Tawi Jipya na la Kisasa likiwa pia na sehemu ya miradi ya  kiuchumi.
“ Chama cha Mapinduzi katika ngazi zake zote lazima kiwe na miradi ya kiuchumi itakayosaidia utekelezaji wa kazi  za chama hicho katika ngazi husika ili kujilinda na utegemezi kutoka ngazi za juu za chama  “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba uwamuzi wao huo ni sahihi na unakwenda sambamba na lengo la Chama ndani ya Jimbo la Kitope la kuwa na Ofisi mpya za kisasa zinazokwenda na wakati
Alieleza faraja yake kuona kwamba Jimbo la Kitope katika Matawi yake 20 hadi sasa tayari Ofisi 16 za chama cha Mapinduzi zimeshakamilika kujengwa majengo mapya ikibakisha Matawi manne tu.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
13/9/2013.

Tuesday, 10 September 2013

KUMBUKUMBU YA WALIOFAKI KWA MELI --ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema inaendelea na hatua mbali mbali za kujipanga katika sekta ya usafiri wa baharini ili kuepusha ajali ya meli kuzama isitokee tena  kama ilivyotokea ajali ya Mv.Skagit na MV.Spice islander.

Hayo wameelezwa na Waziri wa Fedha Zanzibar,Mhe.Omar Yussuf Mzee katika kikao cha kumbukumbu ya wahanga walifarika katika ajali hiyo kilichaandaliwa na waandishi wa habari wa maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA).

Alisema Serikali ilichukua juhudi za kuchunguza na kubaini makosa mengi,ambayo yamesababisha ajali ya meli hizo kuzama,hivyo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  imepanga mikati mengi ya kuzuia ajali kama hiyo isitokee tena nchini.

Alisema Serikali ilibaini baadhi ya meli zilifanyiwa maarifa ya kuongezwa ukubwa (Modefication) hivyo Serikali imezisimamisha meli hizo kuendelea kutoa huduma ya usafiri wa baharini.

Mzee alisema Serikali  ilibani kulikua na meli zilikuwa zinafanyakazi kinyume na usajili wake,baada ya kubeba mizigo ilikua na beba abiria,ikiwemo tatizo kuajiri wafanyakazi wasiokuwa na sifa ya utaalam wa kazi hizo.Pia alisema baadhi ya meli zilikua hazina vifaa vya kujihami(life Jacket).

Alisema kutokana msiba mkubwa uliotokea wa Meli hizo mbili kuzama Mv.Skagit na MV.Spice Ilander  Mhe.Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein ameagiza Serikali ichukua hatua ya ununuzi wa meli mpya ya abiria na mizingo.

Alisema katika maagizo ya Mhe.Rais Dkt Shein ameagiza ijengwe meli yenye ubora na yenye usalama ambapo  hatua  za ujenzi wa meli mpya ya abiria imeshaanza kujengwa nchini Korea ya Kusini.

Alielezea Meli hiyo mpya itakuwa na mashini mbili(Engine) ikiwemo na rada,chumba  ambacho kitaweza kufifadhi maiti wa wawili pamoja na chumba cha Daktari atakaekuwa yumo ndani ya meli kila itakapokuwa ipo safarini.

Aidha Mzee alisema Serikali haikukaa kimya imezitaka wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini vyote viwe na bima ilikua hai(LIVE).Pia alisema Serikali imeshatoa amri meli itakayopakia abiria zaidi  ya uwezo wake isiondoke kinyume na agizo hilo captain na mkuu wa bandari wote watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa upande wa wajumbe wa Kikao akizunguza bibi mzuri aliiomba Serikali kuwafikiria jinsi ya kuwasaidia watu walioathirika kisaikolojia kutokana na ajali za meli hizo kuzama.
Alisema kuna watu wameathirika kisaikolojia kwa kupoteza watoto wane kwa wakati mmoja ,baadhi ya wanawake kupoteza mume na watoto.

Kikao hicho kimeandaliwa na Jumuia ya waandishi wa habri za maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)  ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuwakumbuka wahanga waliofariki katika ajali ya meli ya Mv.Skagit na Mv.Spice islander iliotokea Septemba 2011 na Julai 2012.
 




Monday, 9 September 2013








Hatimae Mabingwa wa Mashindano ya Ujirani mwema ya Dr. Sheni Cup yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Nungwi na kufadhiliwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali  Mohammed Sheni amepatikana katika mchezo wa Fainali ya mashindano hayo yaliyozikutanisha Timu za Soka za Kitamli ya Nungwi  dhidi ya wapinzani wao Timu ya Soka ya Mwendo Mdundo ya Kidoti.
Pambano hilo la Fainali lililoshuhudiwa na umati mkubwa wa wapenzi wa soka wa Jimbo la Nungwi na Vitongoji vyake limeiwezesha Wenyeji wa mashindano hayo Timu ya Kitamli ya Nungwi kuibuka na ushindi kwa kuilaza Mwendo Mdundo ya Kidoti Goli 1-0.
Timu ya Kitamli ilijipatia goli lake la pekee na la ushindi lililofungwa na mchezaji Haji Wa Haji katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo  ambapo mgeni rasmi katika pambano hilo la Fainali ya Dr. Sheni Cup alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mashindano hayo ya ujirani mwema  yaliyoanza kutimua vumbi Tarehe 24/8/2013 yamejumuisha Timu  Tisa kutoka katika vijiji tofauti vya Jimbo la Nungwi yakienda sambamba na yale ya mchezo wa Pete { Net Ball } kwa Wanawake yaliyojumuisha Timu Nne.
Akizungumza mara baada ya pambano hilo la Fainali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwahimiza Vijana hao kujitahidi kujifunza zaidi michezo ili wajijengee njia rahisi ya kupata ajira kupitia sekta ya michezo ambayo wakati huu imekuwa na thamani kubwa Duniani.
Balozi Seif alisema Ulimwengu hivi sasa umeshuhudia ongezeko kubwa la ajira kupitia Sekta ya michezo hasa Mchezo wa soka na Table Tennis ambayo imeonekana kutajirisha wanamichezo wengi wenye vipaji vikubwa vya michezo hiyo.
“ Tumeshuhudia wachezaji mbali mbali Duniani wakiwemo pia wale wanaotokea Bara letu la Afrika wakicheza mpira wa kulipwa katika timu mbali mbali za bara la Ulaya hasa ndani ya Uingereza. Huo ni Mfano halisi mmaopaswa kuutilia maanani ili na nyinyi siku moja mjikute mmetinga katika vilabu hivyo maarufu Duniani “. Alisisitiza Balozi Seif.
Mapema Mlezi wa Jimbo la Numngwi ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Haji Omar Kheir alisema mashindano hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM wa Jimbo hilo kwa  ushauri wa Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010.
Haji Omar alisema ilani hiyo imeeleza umuhimu wa uimarisha michezo katika maeneo mbali mbali nchini   lengo likiwa  kuwajengea afya njema pamoja na ajira wananchi wanaoshiriki michezo hiyo.
Katika kuunga mkono uendelevu wa mashindano hayo Waziri Haji Omar aliahidi kuchukuwa dhamana ya malipo kwa deni linalodaiwa Kamati ya mashindano hayo linalohusu malipo ya posho za waamuzi pamoja na baadhi ya vifaa vya mashindano hayo.
Katika fainali hiyo  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Kikombe kwa Mabingwa wa Mashindano hayo Timu ya Kitamli ya Nungwi, Jezi, Mpira pamoja na Shilingi laki 300,000/-.
Balozi Seif pia alimkabidhi mshindi wa pili Mwendo Mdundo ya Kidoti Jezi, Mpira na Shilingi Laki 150,000/- wakati mshindi wa Tatu Timu ya Mapinduzi ya Kidagoni ikakabidhiwa  Jezi, Mpira na Shilingi 75,000/-.
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akakabidhi shilingi 50,000/- kwa kila Timu bora , Mchezaji bora, mfungaji bora, Muamuzi bora, Mchezaji mdogo kuliko wote,kipa bora  pamoja na kocha bora kwenye mashindano hayo.
 Mashindano hayo yaliyopewa jina la Dr. Sheni Cup kwa mchezo wa Soka na Mwanamwema Sheni Cup kwa mchezo wa Pete { Net Ball } yamegharimu jumla ya shilingi milioni Sita Nukta Tano { 6,500,000/- }.
Wakati huo huo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi mchango wa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa ajili ya kusaidia ufufuaji wa michezo ya ndani { Indo games } hapa Nchini ambayo mingi inaonekana kufifia na mengije kufa kabisa kwa  kipindi kirefu sasa.
Akikabidhi mchango huo kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar  { BTMZ } Sharifa Khamis hapo Ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar ilikuwa ikisifika kimataifa kwa michezo ya ndani sifa ambayo hivi sasa imekufa kutokana na kufifia kwa michezo hiyo.
Alisema juhudi za pamoja zinahitajika kuchukuliwa katika kuona michezo hiyo inachipuka tena hapa Nchini kwa kuwapa nguvu za uwezeshaji na vifaa wachezaji wanaojihusisha na  michezo hiyo.
“ Vijana lazima waendeleze pia michezo ya ndani kama vile Table Tennis, Vinyoya, Beach Ball, Triatholon na riadha badala ya kuelekezaa  nguvu zao zaidi kwenye soka ili kurejesha sifa hiyo Kimataifa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akipokea mchango huo Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar             { BTMZ } Sharifa Khamis { Sherry } alisema msaada huo wa Balozi Seif ni hatua ya awali katika kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Taasisi za Michezo Nchini katika kufufua vuguvugu la michezo hapa Nchini.
Mwenyekiti Sharifa { Sherry } alisema katika kwenda samba mba na ufufuaji huo Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Soka Zanzibar        { ZFA } hivi karibuni  vinatarajiwa kufungua vuguvugu la michezo katika kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
 9/9/2013.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Wizara inayosimamia  sekta  ya kazi  ni  kuhakikisha kwamba inapambana na tatizo  la ajira linaloonekana kuathiri nguvu kubwa ya Vijana hapa Nchini.
Kauli hiyo aliitoa wakati  akizindua rasmi  Chuo cha Ushoni cha ujasiri amali  kilichoanzishwa na  Jumuiya ya Vijana ya Kibweni { Kibweni Yourth Organization } kiliopo katika Mtaa wa Kwa Botoro Kibweni ndani ya Jimbo la Bububu.
Balozi Seif alisema hatua hiyo ya Serikali inakwenda samba mba na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 inayoelezea umuhimu wa kuundwa  kwa vikundi vya  ujasiri amali ambavyo hutoa fursa kubwa ya ajira miongoni mwa wananchi.
Alisema kazi za ujasiri amali zimekuwa zikisaidia kupunguza umaskini  na Serikali itajitahidi kuhakikisha inavijengea nguvu vikundi hivyo vya Jamii ili viweze kutekeleza majumu iliyojipangia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya ya Vijana ya Kibweni kwa uamuzi wake wa kuanzisha Kikundi hicho ambacho ni mkombozi kwa wanajumuiya pamoja na vijana wa Jimbo hilo.
Hata hivyo Balozi Seif alihimiza viongozi na wana jumuiya hiyo kuwa wastahamilivu na kuvumiliana katika harakati zao za kila siku na hatua hiyo aliielezea kwamba itafanikiwa endapo utaratibu wa kufuata kanuni walizojiwekea utazingatiwa zaidi.
“ Nimefurahi kuona Vijana mmejikusanya kuanzisha mfumo wa ajira ambao Serikali kuu kadri ya hali itakavyoruhusu itazingatia na kutoa msaada unaostahiki ili kukiendeleza kikundi chenu “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alihimiza mpango wa kuendelea kupanda miti ulionzishwa na vijana hao wa Kibweni ili kukabiliana na upungufu wa maji uliyoikumba nchi kutokana na tabia za baadhi ya watu kukata miti ovyo.
Katika kuunga mkono juhudi za Vijana hao wa Kibweni za kuanzisha Chuo cha Ushoni cha ujasiri amali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Vyarahani vitano kama mchango wake wa kukipa nguvu Chuo hicho.
Balozi Seif pia aliahidi kuchangia Kompyuta moja na Mashine ya Kudarzi kwa chuo hicho hatua  ambayo imeungwa Mkono na Mwakilishi wa jimbo la Bububu Hussein Ibrahim Makungu aliyetoa mchango wa Shilingi Milioni 2,000,000/- taslim wakati Mbunge wa Jimbo hilo Masoud Sururu ambae ndie mlezi wa Jumuiya hiyo akaahidi kuchangia Vyarahani Vitano, Pasi na Vifaa vidogo vidogo.
Akisoma  Risala ya wanajumiya hiyo ya Vijana wa Kibweni  mmoja wa mwanachama wa Jumuiya hiyo Farida Juma Haji alisema Vijana wa Kibweni wameamua kuanzisha  jumuiya hiyo wakitambua kwamba Serikali Kuu haina fursa ya kutoa ajira kwa watu wote.
Alisema elimu ya ujasiri amali ambayo ni muhimu kwa taifa lolote Duniani ndio itakayowapa nafasi pekee ya kukabiliana na tatizo hilo la ajira na upande mwengine jumuiya imelenga kwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kupunguza Umaskini Zanzibar { Mkuza }.
Mapema akikikagua chuo hicho cha Ushoni cha ujasiri amali cha  Kibweni Mwalimu  wa chuo hicho Bibi Subira Haji Yahya alimueleza Balozi Seif kwamba lengo la kuanzishwa kwa chuo ni kuwajengea mazingira ya ajira vijana wa Shehia hiyo.
Bibi Subira alieleza kwamba mfumo huo wa mafunzo mbali ya kutengeneza kazi za ajira lakini pia utasaidia kupunguza wimbi la vitendo viovu wanavyojihusisha zaidi vijana ndani ya mitaa na kuleta kero na fadhaa kwa jamii.
Chuo cha ushoni cha ujasiri amali cha Kwa Botoro kilichoanzishwa na jumuiya ya Vijana wa Kibweni { Kibweni Yourth Organization – KYO } kimeanzishwa karibu miezi Tisa iliyopita kikiwa na wanafunzi 16 wa rika mbali mbali.
Wanafunzi wa chuo hicho hupata fursa ya kujifunza ushoni wa nguo tofauti wakianzi na zile za watoto wadogo kwa hatua ya ukataji na kufuatia ushoni utakaoambatana na kupatiwa vyeti wakati wanalizapo muda wao wa mafunzo.
Uongozi wa chuo hicho pia umeweka utaratibu wa kuwarahisishia wanafunzi wake muda wa mafunzo kulingana na harakati zao za maisha za kila siku ambapo pia hupata wasaa wa kujifunza lugha ya Kiingereza pamoja na upandaji miti katika maeneo ya vianzio vya maji vya Mwanyanya.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/9/2013.


Hasara ya zaidi ya Shilingi Bilioni Moja Nukta 2 imepatikana kufuatia kuungua kwa moto hoteli mbili za Kitalii za  White Sand na Sun Set Bungalows ziliopo katika Kijiji cha Kendwa Nungwi Wilaya ya Kaskazini “ A” Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi majira ya saa 11.00 za jioni.
Hoteli ya Sun Set Bungalows inakadiriwa kupata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 400,000,000/- wakati ile ya White Sand  iliyoungua zaidi kutokana na moto huo inakadiriwa hasara ya zaidi ya shilingi Milioni mia 800,000,000/-.
Moto huo ulisababishwa na hitilafu za umeme katika moja ya majengo ya Hoteli ya Sun Set Bungalows iliyoezekwa makuti na kutoa cheche za moto zilizosambaa kwa haraka katika baadhi ya  majengo mengine kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma katika eneo hilo.
Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi akitokea Bungeni Mjini Dodoma alifika eneo hilo la tokeo ili kuwafariji Wamiliki, Wafanyakazi wa Hoteli hizo pamoja na Wananachi wanaozizunguuka Hoteli hizo kutokana na maafa hayo makubwa kwa uchumi wa Taifa.
Akitoa ufafanuzi wa  mkasa halizi wa tukio hilo  Mmiliki wa Hoteli ya Sun Set Bungalows Abdullsamad Ahmed Said alimueleza Balozi Seif kwamba Moto huo umevikumba vyumba Vinane vya  kulala wageni, Stoo pamoja na jiko la kupikia.
Abdullsamad alisema Wageni wapatao sabini waliokuwemo kwenye vyumba vya Hoteli hiyo waliweza kuokolewa kwa ushirikiano kati ya Wafanyakazi wa Hoteli hiyo na Wananchi walioizunguuka Hoteli hiyo jambo ambalo lilileta faraja kwa Uongozi pamoja na wafanyakazi wake.
Mmiliki huyo wa Hoteli ya Sun Set Bungalows aliwashukuru wananchi hao, Viongozi wa Serikali Wilaya na Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Maafisa wa Kamisheni ya Utalii kwa msaada wao ulichangia kupunguza machungu ya janga hilo.
Balozi Seif Ali Iddi akikagua hali ya tukio  la moto huo ambao pia uliathiri Hoteli nyengine ya jirani ya White Sand ambapo Mmoja miongoni mwa  Viongozi wa Hoteli hiyo Ramadhan Msanif  alimfahamisha Balozi Seif kwamba  wakati wakijiandaa kutoa msaada kwa wenzao jirani wa Sun Set cheche za moto huo pia zikaanza kuvamia Hoteli yao na kulazimika kukabiliana nalo.
Bwana Msanif  alisema licha ya juhudi walizochukua kukabiliana na moto huo lakini kasi kubwa ya upepo uliokuwa ukivuma wakati huo ulisababisha kuathiri  mapaa ya nyumba  10  za hoteli hiyo katika kipindi kifupi kwa vile zilikuwa na mapaa ya makuti.
Akizungumza na Viongozi, Wafanyakazi wa Hoateli hizo pamoja na Wananchi wa jirani na Hoteli hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alitoa wito kwa wananchi kuendelea kusaidia wawekezaji wakati yanapotokea majanga kwenye maeneo ya vitega uchumi.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inasisitiza na kutegemea sekta ya Utalii ambayo kwa sasa inasaidia kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kutoa ajira kwa wananachi wanaovizunguuka vitega uchumi hivyo.
Hata Hivyo Balozi Seif aliendelea kuwakumbusha wawekezaji vitega uchumi mbali mbali Nchini kujenga utamaduni wa kuiwekeza Bima Miradi yao ili wakati wanapopatwa na majanga au maafa Bima hizo ziweze kuwasaidia.
Alisema inasikitisha kuona ipo miradi ya kiwango kikubwa cha fedha inayoendelea kuwekezwa Nchini lakini wamiliki wengi wa miradi hiyo wanashinda kuikatia bima na hatiame inakufa kabisa pale inapokumbwa na majanga kama ya moto.
“ Wawekezaji na hata Wafanyabiasharawengi  bado wamekuwa wazito kuiwekea Bima miradi yao na kusahau kwa kuona ghali  mpango huo ambao kumbe huwa unawasaidia wakati wanapopatwa na majanga “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi waliopo jirani na Hoteli hizo kwa juhudi kubwa waliyochukuwa na kusababisha  kupungua  kwa hasara kubwa iliyokuwa izikumbe hoteli hizo.
Alisema juhudi hizo zilizowaongezea nguvu za uokozi wafanyakazi wa hoteli hizo zimesaidia kuokoa mali na vifaa vya hoteli pamoja na wageni waliokuwa wakipata huduma ndani ya Hoteli hizo.
“ Nafarajika kusikia kwamba harakati za uokozi wa mali na vifaa katika Hoteli hizi mbili za White Sand na Sun Set Bungalows za Kendwa hakukuwa na ripoti za udokozi wa mali kama zilivyotokea Kwenye Hoteli ya Paradise Beach Resort iliyopo  Marumbi wakati ilipowaka moto wiki moja na nusu iliyopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Hoteli hizo kufikiria kubadilika  katika mfumo wa ujenzi wa mapaa ya makuti ili kujilinda na  majanga yanayoweza kuepukwa licha ya kwamba mfumo huo hutoa ajira kwa wananchi wanaouza makuti yao.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia eneo lililopembezoni mwa Bara bara mbele ya Skuli ya Msingi na Sekondari ya Mto Pepo ambalo liko katika hali mbaya kimazingira.
Ziara hiyo ya ghafla ya Balozi Seif ilikuja kufutia baadhi ya wananchi kufanya Biashara katika eneo hilo linalotishia afya za Binaadamu kutokana na kutuwama kwa maji machafu yanayoweza kusababisha maradhi ya kuambukiza.
Katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuagiza Sheha wa Shehia ya Mto Pepo pamoja na Diwani wa Wadi ya eneo hilo kufika Ofisini kwake Vuga Jumatatu  ya Tarehe  9 Septemba  asubuhi kulijadili suala hilo.
Hali ya mazingira ya  eneo hilo mbali ya kutoa  sura mbaya kwa wapita njia na wageni lakini pia inaweza kusababisha mripuko wa maradhi  hasa kwa  wanafunzi wadogo wasiozingatia afya zao wa Skuli ya jirani na eneo hilo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
8/9/2013.





Jamii ya Kiislamu popote pale Duniani inalazima kufanya jitihada za makusudi katika kuona inaendelea kutumia utamaduni wa Kiislam katika muelekeo zaidi wa  elimu, mawazo ya maendeleo, biashara, uchumi, siasa, sayansi na utawala kwa lengo la kuuongezea nguvu ya ziada.  
Hatua hiyo itawapa muono wa kweli watu wengi wasiokuwa waumini wa Dini hiyo kuwaondolea shaka kwamba Uislam si kundi la waumini ambao sera zao ni vurugu, ugaidi na uuwaji mawazo ambayo hata baadhi ya Waislam wanachangia bila kuelewa. 
Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Moh’d Gharib Bilal wakati akilifunga Kongamano la Kimataifa kuhusu Historia ya Ustaarabu wa Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika ukumbi wa Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Del Est Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema misikitini mingi siku hizi imekuwa na hotuba za hamasa, jazba , uchochezi   na  kugeuzwa kama majukwaa ya kisiasa badala ya kutolewa hotuba za ibada na mafunzo ya Kiislam yanayohusu kumuabudu Mwenyezi Mungu na mafundisho yake ya kupenda kufanya mazuri aliyoyaamrisha na kukataa mabaya aliyoyakataza.
Aliwataka wana jamii wa Utamaduni wa kiislamu kutafakari kwa makini athari hii iliyojichomoza ambapo isipozingatiwa na kupatiwa dawa maalum inaweza kumong’onyoa maadili na usaarabu huo wa Kiislamu.
Alieleza kwamba ipo haja kwa wakati huu kurejeshwa mfumo wa zamani wa kuifanya Misikiti kuwa ni chimbuko la elimu ambapo ilikuwa mwalimu hukutwa amezunguukwa na vitabu mbali mbali akiendelea kutoa elimu ambapo nyumba zao zikijaa baraza kwa kuwa ni sehemu ya Madrassa. 
Alifahamisha kwamba elimu ya dini ilipewa umuhimu wa kipekee ambapo kila mtoto alijengewa mazingira ya kupata taaluma ya dini kwanza ikifuatiwa na  ile ya elimu ya dunia
“ Hakukuwa na mtoto ambaye hakuweza kupata elimu. Vyuo (Madrrassa) vilienea kila pembe. Vijijini ilikuwa wazazi wakenda kulima mtoto mdogo anapelekwa chuoni kulelewa na wakubwa zake. Kwa hiyo alianza kupata hisia za elimu akiwa tangu mdogo “.Alifafanua Makamu wa Raiswa Serikali ya Jmuhuri ya muungano wa Tanzania.
Dr. Bilal alisema kwamba Utamaduni wa Kiislam umepata nguvu kubwa kutokana na msingi wake wa kurithisha vizazi kwa njia ya mashairi, maandiko na tungo tofauti, hivyo si kosa kueleweka kuwa utamaduni huo umejengwa chini ya msingi wa elimu kwa vile chimbuko lake linatokana na  Qur’aan na Sira za Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad (SAW).
“ Mbali na athari zilizojichomoza lakini  bado utamaduni wa Kiislam unabaki kuwa ni utamaduni wa Kiislam. Una miko yake, una sifa zake na una matumizi yake. Utamaduni wa Kiislam unaweza kujisifu kuwa umeweza kusaidia ukuaji wa tamaduni nyingi hasa za Ulaya “. Alifafanua Dr. Moh’d Gharib Bilal.
Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alisisitiza kwamba Ukuaji wa lugha ya kiarabu kuwa ya Kimataifa ya sayansi na uendeshaji Serikali umesaidia kuufanya Uislam uwe kiungo cha maendeleo chini ya msingi wa Quran inayowaagiza waumini kutafuta elimu popote pale na muda wote wa umri wao.
Amewapongeza waliowaza kufanya kongamano kama hili hapa Zanzibar na hasa wakati huu ambao Uislam unapita katika mitihani mikubwa na kuelezea matumaini yake kutokana na ushiriki mkubwa wa wajumbe utakaotoa maazimio mazuri yatakayosaidia kupeleka mbele Uislam na ustaarabu wake.
 
Akisoma maazimio ya wana kongamano hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kongamano hilo Dr. Juma Halifa Juma alisema wana kongamano hilo wamependekeza kuendelezwa kwa makongamano hayo kila mara.
Dr Juma alisema wana kongamano hao walisisitiza umuhimu wa kuandikwa kwa Historia ya Uislamu wa Afrika ya Mashariki na baadaye kuingizwa katika mitaala itakayozingatia mfumo wa sasa wa Sayansi na Teknolojia.
Walisema umuhimu wa kubadilishana utafiti kati ya waislamu wa Afrika na wenzao wa mabara mengine Duniani unafaa kuzingatiwa vyema ili usaidie kuimarisha kasi ya utamaduni na Dini ya Kiislamu popote duniani.
Wana kongamano hao wamemshukuru Mfalme Qaboos Bin Said wa Oman kwa uamuzi wa Serikali yake kupitia Taasisi zake kuandaa kongamo hilo lililotoa fura kwa wanafalsafa, wasomi na waumini wa dini ya kiislam kupata kubadilishana mawazo.
Naye Mwenyekiti wa mamlaka  ya kutunza nyaraka na kumbu kumbu ya Qasri Nchini Oman Dr. Hamad Moh’d Al – Dhawian Bin Balqas alielezea faraja yake kutokana na michango mikubwa ya washiriki wa Kongamano hilo hasa wale wenyeji Zanzibar.
Dr. Hamad alisema utafiti unaonyesha wazi kwamba Afrika Mashariki ni markaz ya kuleta mabadiliko ya butamaduni wa ustaarabu wa Kiislamu hapa ulimwenguni.
 Akimaribisha Mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Juma Shamuhuna alisema Zanzibar imepata heshima na bahati kubwa ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo jambo ambalo litaijengea historia ndefu katika masuala ya utamaduni wa ustaarabu wa kiislamu Duniani.
Jumla ya nyaraka 60 zilijadiliwa katika kongamano hilo lililosheheni wataalamu, wasomi, watafiti na hata wanavyuoni wa dini ya Kiislamu kutoka pembe mbali mbali za Dunia.
Kongamano hilo la pili la Kimataifa la ustaarabu wa Kiislamu likitanguliwa na lile llililofanyika Uganda mwaka 2012 na limeshirikisha Mataifa kumi na saba mbali mbali Duniani likiwa na lengo la kujitanga za Zanzibar katika Nyanja za Utafiti na Taaluma Kimataifa.
Serikali ya Oman kupitia ushirikiano wa mamlaka ya kumbu kumbu na nyara ya Nchi hiyo ndio iliyoandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }.
 
 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/9/2013.
 


Uhusiano wa  kubadilishana nyaraka za Kihistoria kati  ya Oman na Zanzibar  unaweza kuwasaidia wananchi  wa pande  mbili  pamoja na watafiti wa masuala ya Kihistoria kuelewa kwa kina maingiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya  Wazanzibar na Waoman ambayo yanafanana  Kisilka na Kiutamaduni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Viongozi sita wa Serikali ya Oman ulioongozwa na Waziri wa Habari wa Nchi hiyo Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu tokea karne ya 18 ambao umethibitishwa na wataalamu pamoja na watafiti wa mambo ya Kihistoria kutoka vyuo vikuu tofauti Duniani.
Alielezea haja kwa Viongozi na Wananchi wa Oman na Zanzibar kuendelea kushikamana na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya maendeleo yatakayosaidia ustawi wa vizazi vya sehemu zote mbili rafiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Serikali ya Oman  kupitia ushirikiano wa mamlaka  ya kumbu kumbu na nyaraka ya Oman na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } kwa kuandaa Kongamano la Kimataifa la Ustaarabu wa Kiiislamu kwa Nchi za Mashariki mwa Bara la Afrika.
Balozi Seif alisema  uamuzi huo wa kufanywa kwa kongamano hilo  hapa Zanzibar umekuja wakati muwafaka kwa wataalamu wa mambo ya Kale kubainisha kwamba  Historia ya Uislamu imeanzia hapa Zanzibar.
“ Nimefurahi kusikia kwamba Historia ya Uislamu imeanza Zanzibar. Inaonyesha watafiti wameliona hili kutokana na asilimia kubwa ya wakaazi wa Visiwa vya zanzibar  kuwa  waumini wa Dini ya Kiislamu sambamba na Utamaduni wake “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri tafiti za Wataalamu wa masuala ya Historia ambazo zitaibuka katika Kongamano hilo  zielekezwe zaidi kunufaisha wananchi  na waislamu wa ukanda wote wa Afrika Mashariki.
“ Tafiti hizi za Wataalamu wetu wa Kihistoria itapendeza kama zitaendelea kubakishwa katika maktaba zetu ili zisaidie wananchi, waislamu na hata wasomi wetu wa vyuo vikuu vya ukanda wetu wa Afrika Mashariki “. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi.
Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa Serikali ya Oman Waziri wa Habari wa Nchi hiyo   Dr. Abdulmumin Mansour Bin Said Al- Hasani alisema ipo haja ya kuendelea kuhifadhiwa kwa Historia iliyopo ya Zanzibar na Oman kwa faida ya vizazi vijavyo.
Dr. Abdulmumin alieleza kwamba upeo wa tabia za watu wa oman na Zanzibar unaolingana ndio unaochangia na kushawishi wageni na watalii wa mataifa mbali mbali  duniani  kupendelea kuzitembelea nchi hizi zinazofanana kiutamaduni.
Waziri huyo wa Habari wa Oman alifahamisha kwamba Kongamano  hilo la ustarabu wa Kiislamu linalofanyika hapa Zanzibar  mbali ya utafiti uliopatikana lakini pia litafungua uhusiano katika Nyanja nyengine za maendeleo kwa nchi shiriki.
Dr. Abdulmumin alielezea faraja yake kutokana na umuhimu wa udugu uliopo  kati ya watu wa Oman na Zanzibar ambao umepelekea waoman wengi  kujitokeza kushiriki kwenye kongamano hilo.
Alifahamisha kwamba ipo ishara ya kuendelea kwa ziara za mara kwa mara kati ya watu wa pande hizo mbili.
Kongamano hilo la siku tatu linalofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya La Gemma Della East Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kushirikisha Mataifa yapatayo 17 lina lengo la kuitangaza Zanzibar katika Nyanja za utafiti na Taaluma Kimataifa.
Hilo ni kongamano la Pili la Kimataifa la Ustarabu wa Kiislamu  kufanyika likitanguliuwa na lile la mwaka 2012 lililofanyika Nchini Uganda na kutolewa uamuzi wa kongomano linalofuata kufanyika hapa Zanzibar kutokana na  Historia yake  iliyopo  sambamba na uhusiano  wa karibu iliyonayo na Mataifa ya Kiarabu.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/9/2013.

Mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Jamuhuri ya Uturuki katika kusaidia Sekta ya Afya Zanzibar umesaidia kuipunguzia mzigo mkubwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwahudumia Wananchi wake hasa wale wanaohitaji kusafirisha  kwa ajili ya matibabu zaidi ya kitaalamu nje ya Nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiwashukuru Madaktari 45 na Maprofesa watano wa Jamuhuri ya Uturuki waliokuwepo Nchini kutoa huduma mbali mbali za afya ikiwemo upasuaji alipozungumza nao katika ukumbi mdogo wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ziara za kila mwaka kwa timu za madaktari wa Uturuki wanaokuja kujitolea Zanzibar katika sekta ya afya zimeleta faraja na upendo baina ya watu wa Uturuki na Zanzibar hali ambayo alieleza kwamba inapaswa kuimarishwa na kuenziwa zaidi.
Alifahamisha kwamba mpango wa Madaktari hao kupitia taasisi zao za misaada za kutoa msaada wa vyandarua 8,000 pamoja na usomeshwaji wa wazanzibari wapatao 86 tokea kuanza kwa mpango huo mwaka 2007 umetoa picha halisi kwa taasisi hizo jinsi zilivyokubali kujitolea kusaidia huduma za Kibinaadamu hapa Nchini.
“ Tunafurahi kuona kwamba msaada wenu huu wa vyandarua umekuja wakati muwafaka kwa vile Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar iko katika mpango wa  kumaliza kabisa maradhi ya malaria Nchini ambayo hivi sasa yamepunguwa kwa hatua kubwa sana “. Alieleza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Uturuki kupitia Taasisi zake za Misaada ya maendeleo ya vyuo Vikuu kwa jitihada zake inazochukuwa za kusaidia huduma za kijamii kwa mataifa rafiki ikiwemo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“ Wapo wataalamu wetu wengi wa fani ya afya waliowahi kupata mafunzo yao ya juu nchini Uturuki  hatua ambayo kwa kiasi kikubwa inaendelea kuipunguzia mzigo  kubwa Serikali  kwa kumsafirisha mgonjwa nje ya Zanzibar kwa matibabu ambao wengi kati yao hivi sasa wanayapata hapa hapa Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.
Naye Kiongozi wa Madaktari hao kutoka  Chuo Kikuu cha Fatih kinachoshughulikia masuala ya matibabu na utafiti kutoka Jamuhuri ya Uturuki  Profesa Mkuu wa Upasuaji  Omer Faruk Akinci alisema tatizo kubwa la Jamii linaloleta fadhaa na hatimae kutumbuka kwa maradhi tofauti ni msongamano wa mawazo yasiyokwisha.
Profesa Omer Faruk alisema kitu pekee kitakachoisaidia  jamii popote pale katika kupunguza wimbi hilo la mawazo ni kwa wana jamii wenyewe kuelekeza nguvu zao zaidi katika kujipatia  taaluma ambayo ndio mkombozi wa yote.
Wakitoa salamu katika kikao hicho wadhamini wa Madaktari hao wa Uturuki  Profesa Seif Ali Tekalan kutoka Chuo Kikuu cha Fatih na Profesa MuratTuncer wa Chuo Kikuu cha Hacettepe Nchini humo walisema vyuo vyao hivi sasa vina jumla ya wafanuzi 25 wanaosomea fani  tofauti  kutoka Tanzania   Bara pamoja na Zanzibar.
Walisema wakati Taasisi zao zimejikita zaidi katika kuimarisha sekta ya elimu kuanzia skuli hadi vyuo vikuu zimelenga  kuongeza zaidi idadi ya viwango vya wanafunzi  wanaotoka Tanzania.
Wametoa mwaliko kwa wanafunzi wa Tanzania kushiriki katika mashindano yatakayoandaliwa na vyuo vikuu hivyo hapo baadae katika masuala ya elimu yakijikita zaidi  kwenyea masuala  ya Utamaduni.
Mapema Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Juma Duni Haji alisema ushirikiano uliopo kati ya wananchi wa Mataifa ya Jamuhuri ya Uturuki na Zanzibar ni dalili nzuri ya uhusiano mwema kati ya pande hizo mbili.
Waziri Juma Duni Haji alishauri dalili hiyo nzuri ya uhusiano inapaswa kuendelea kuenziwa na kuimarishwa kwa ustawi wa vizazi vijavyo vya pande zote mbili rafiki.
Madaktari hao  wa Jamuhuri ya Uturuki  walipata fursa ya kutoa huduma mbali mbali za afya katika hospitali za Mnazi Mmoja, Nungwi, Kitope, Kivunge, Makunduchi kwa unguja na  Chake chake wete, Mkoani na Vitongoji kwa Pemba.
Serikali ya Jamuhuri ya Uturuki kupitia Taasisi zake za vyuo vikuu vya mambo ya Afya imekuwa ikitoa msaada wa kiafya kwa kuwashirikisha madaktari wake wanaojitolea kuja kufanya kazi hapa Zanzibar kwenye mpango wake maalum ulioasisiwa tokea mwaka 2007.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
2/9/2013.





Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Meja Khatibu Shaaban Mshindo aliyefariki Dunia akiwa katika shughuli za ulinzi wa amani katika kikosi  cha umoja wa Mataifa kwenye jimbo la Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo amezikwa kwa heshima zote za Kijeshi.
Meja Shaaban ambaye alijeruhiwa vibaya kwa bomu katika eneo lake la kazi na kusababisha kuvuja damu nyingi na hatimae kusababisha kifo chake akiwa njiani kupelekwa Hospitali alizikwa kijiji kwao Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa Kaskazini Unguja.
Makamanda na wapiganaji wa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania , askari wengine wa vikosi vya ulinzi, wananchi , ndugu wa marehemu walishiriki kwenye mazishi hayo wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed.
Marehemu Meja Khatib Shaaban Mshindo alizaliwa Tarehe 29 Septemba 1972 katika Mtaa wa Rahaleo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi na baadaye kupata elimu yake ya msingi na kuhitimu mwaka 1986.
Alijiunga na Skuli ya Sekondari uchama na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 1990 ambapo baadaye akajiunga na kidato cha tano na sita katika skuli ya sekondari ya Alharamain na kumaliza mwaka 1993.
Meja Khatib Shaaban Mshindo alijiunga na Jeshi la wananchi wa Tanzania             { JWTZ } Tarehe 1 machi 1995 na kutunukiwa heshima ya kamisheni tarehe 17 mei 1997.
Katika utumishi wake Meja Khatib Shaaban Mshindo alibahatika kuhudhuria mafunzo ya afisa mwanafunzi chuoni Monduli, kozi ya uongozi wa platuni, uongozi wa kombania pamoja na mafunzo ya operesheni Nchini Canada mwaka 2008.
Kamanda Khatib kutokana na ukakamavu wake alipandishwa vyeo kuanzia nafasi ya Luteni mwaka 1998, kepteni mwaka 2004 na kufikia cheo cha meja mwaka 2010 wadhifa aliokuwa nao hadi kufariki kwake.
Marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo aliwahi kushika madaraka ya Kamanda wa Kikosi mwaka 1997, Mkufunzi kuanzia mwaka 2000  hadi mwaka 2006 pamoja na kuwa kamanda wa kombania Mkoani Kibaha.
Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua na kuthamini mchango wa Meja Khatibu Shaaban Mshindo alimtunuku nishani ya Miaka 40 ya JWTZ.
Umoja wa Mataifa katika mazishi hayo uliwakilishwa na Kamanda wa Vikosi vya Umoja huo Mjini Goma Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Meja D.B Samujeli .
Kamanda Khatibu Shaaban Mshindo aliyelitumikia jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kipindi cha miaka 18 miezi saba na siku 28 ameacha kizuka mmoja na watoto watatu.
Mwenyezi Muungu alilaze roho ya marehemu Meja Khatibu Shaaban Mshindo mahali peMa peponi. Amin.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/9/2013.