Sunday, 6 October 2013

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza umuhimu wa Jimbo la Kiembe samaki kurejea katika Hisotia yake ya kuwa na wanamichezo mahiri wa soka

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza umuhimu wa Jimbo la Kiembe samaki kurejea katika Hisotia yake ya kuwa na wanamichezo mahiri wa soka wakati akikabidhi Jezi na Mipira kwa timu zilizoshiriki kombe la Dr. Sheni ndani ya Jimbo hilo hivi karibuni.
Balozi Seif akimkabidhi Jezi  na Mipira Katibu wa CCM Jimbo la Kiemba Samaki Suleiman Haroub kwa ajili ya Timu 8 zilizoshiriki Dr. Sheni Cup Jimboni humo hivi karibuni ili kutekeleza ahadi aliwapa wanamichezo hao wakati akiyafunga mashindano hayo.


Uongozi wa Chama cha Mapinduzi kupitia Umoja wa Vijana wa Chama hicho wa Jimbo la Kiembe Samaki umepongezwa kwa utaratibu wake uliojipangia wa kuendesha na kuimarisha michezo hasa ule wa kandanda ndani ya Jimbo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akikabidhi Jezi na mipira kwa  timu za  soka nane zilizoshiriki Mashindano ya Kombe la Dr. Sheni    ambayo yalifanyika hivi karibuni katika Jimbo la Kiembe Samaki.
Balozi Seif ambae alikuwa akitekeleza ahadi aliyoitowa  wakati akiyafunga mashindano hayo kwa kuipatia seti moja ya jezi na Mipira Miwili kila timu shiriki  kati ya nane  zilizomenyana kwenye  mashindano hayo alisema Kiembe samaki inapaswa kurejea katika historia yake ya kutoa wachezaji wazuri.
Alisema eneo la Kiembe samaki limekuwa likitajikana kwa kuwa na wanasoka mahiri ambao wengi kati yao walifanikiwa kuchezea timu kubwa mashuhuri hapa Nchini ikiwemo ile ya Taifa ya Zanzibar  na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wanamichezo hao wa Jimbo la Kiembe samaki kwamba  Serikali itajitahidi kuona kero zinazowakabili wana michezo hao hasa lile tatizo la uwanja wao linatafutiwa ufumbuzi.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki Waride Bakari Jabu, Katibu wa CCM Jimbo hilo Suleiman Haroub alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa umahiri wake anaoendelea kuwa nao wa kuimarisha michezo hapa Nchini.
Naye Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Kiembe Samaki Ibrahim Mbarak Ramadhan alimueleza Balozi Seif kwamba licha ya jitihada zinazochukuliwa na uongozi wa Jimbo hilo wa kuimarisha michezo lakini bado suala la ubovu wa viwanja vya michezo limekuwa kero kubwa.
Ibrahim Mbarak alifahamisha kwamba ubovu wa uwanja wao ambao pia hutumika katika  sherehe za siku kuu za Iddi umekuwa ukiwanyima furaha ya kuendeleza kwa michezo yao katika kiwango kinachokubalika Kimichezo.
“ Tunatamani uwanja wetu wenye urefu unaokubalika kivipimo siku moja unahimili tumutiwa kwa mazoezi au mashindano nyakati za usiku kama vilivyo viwanja vyengine vya wenzetu  ambavyo viko nje ya Mji Mkuu “. Alitoa joto lake katibu huyo wa uvccm Jimbo la Kiembe samaki.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klirpsvik Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
























Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klirpsvik  Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar ambapo walipata wasaa wa kubadilishana mawazo juu ya uhusiano wa mataifa yao mawili.

Serikaliya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kujifunza kupitia Mataifa, Taasisi na Mshirika ya Kimataifa katika mpango wake iliyolenga wa kuelekea kwenye mradi mpya wa uzalishaji wa Mafuta.
Balozi wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn Klirpsvik alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Ingunn alisema hatua hiyo ya tahadhari inayofaa kuchukuliwa na Zanzibar inaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuingia katika mradi huo mpya wa Kiuchumi  kwenye muelekeo wa mafanikio makubwa.
Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Norway wakati wote iko tayari kutumia ujuzi  wake mkubwa katika masuala ya Mafuta kuisaidia Zanzibar kitaalamu ili ifanikiwe katika malengo iliyojipangia katika kuendesha mradi huo.
Alifahamisha kwamba Nch hiyo imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kuunga mkono harakati za kiuchumi na ustawi wa Jamii wa wananchi walio wengi Nchini.
“ Tumekuwa na ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu katik a pande zetu hizi mbili unaolenga kustawisha harakati za kijamii na uchumi kwa wananchi walio wengi “. Alisisitiza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn  Klirpsvik.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameishukuru Serikali ya Norway kwa juhudi zake za kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika maendeleo hasa uungaji mkono katika miradi ya miundo mbinu ya Kiuchumi.
Akizungumzia suala la amani ambalo linaonekana kuiteteresha pembe ya Bara la Afrika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Tanzania imelazimika kuchukuwa tahadhari ili kudhibiti wimbi hili linaloonekana kulikumba eneo hilo.
Balozi Seif alisema Serikali aya Tanzania  iko makini katika kufuatilia wageni wasio na mfumo sahihi wa kuishi ndani ya ardhi ya Tanzania na jitihada zinachukuliwa katika kuratibu wageni walioamua kuishi Nchini kupitia Sheria na taratibu zilizopo za Kitaifa na Kimataifa.
“ Tanzania imelazimika kuwa na tahadhari katika masuala  ya ulinzi wa amani ili kujaribu kuzuia au kudhibiti uasi ama ubabe unaoweza kufanywa na watu au vikundi vinavyopenda kuichezea amani “. Alisisitiza Balozi Seif.
Kuhusu suala la mchakato wa kuelea kwenye Katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Norway Nchini Tanzania Bibi Ingunn kwamba mabaraza ya Katiba ya Wilaya  yamekamilisha vyema mijadala yao.
Balozi Seif alisema hatua hiyo ndio iliyopelekea Bunge la Jamuhuri ya Muungano kujadili Marekebisho ya  sheria ya Katiba na kuipitisha ili kuundwa kwa Bunge la Katiba litakalojadili na  kuidhinsha i   kupigwa kwa kura ya maoni hapo baadaye ili kuamilisha mchakato mzima wa kupata katiba mpya.
Balozi Seif aliendelea kusisitiza kwamba Zanzibar imeshirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima wa kujadili katiba hiyo kuanzia msingi licha ya malalamiko na shutuma zinazoendelea kutolewa na upande wa upinzani kwamba Zanzibar haikushirikishwa.

Wednesday, 2 October 2013

Jamii Nchini inapaswa kuendelea kusaidia Jumuiya zinazojitolea katika mapambano dhidi ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi ili kuwapa faraja na matumaini zaidi watu ambao tayari wameshaathirika na maradhi hayo.

























Mkurugenzi wa Kampuni ya Malik Food inayojihusisha na Biashara ya Kuku { Maarufu Paja nono } Fikirini Hango akimkabidhi Mwenyekiti wa Zapha + Bibi Consolata John Boksi mbili za Mapaja ya Kuku kwa ajili ya kitoweyo cha watoto wanaoishi na vurusi vya Ukimwi.
Nyuma ya Mkurugenzi Fikirini ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Bibi Hasina Hamad pamoja na Mkurugenzi wa Zapha +.


Naibu Katibu wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Suleiman Haji Suleiman kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zapha + Bibi Hasina Hamad msaada wa vyakula.
Pembeni ya Bibi Hasina Hamad ni Mkuu wa Huduma Ofisi ya Faragha ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Kombo  Haji Kheir.
Msaada huo uliokabidhiwa hapo katika Kituo cha Jamii na Watoto cha Zapha + kiliopo Welezo umelenga kuwasaidia watoto yatima walioathirika na virusi vya ukimwi  ambao wazazi waowameshafariki Dunia.


  Press Release:-
Jamii Nchini inapaswa  kuendelea  kusaidia Jumuiya zinazojitolea katika mapambano  dhidi ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi ili kuwapa faraja na matumaini zaidi  watu ambao tayari wameshaathirika na maradhi hayo.
Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akikabidhi msaada wa vyakula  kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye mazingira magumu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao  wazazi wao tayari wameshafariki Dunia.
Balozi Seif alitoa msaada huo wa  Mchele, Mafuta na Sabuni uliowasilishwa na Naibu Katibu wake Nd. Suleiman Haji Suleiman  kwa Uongozi wa Kituo cha Jamii na Watoto cha Jumuiya ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar               { ZAPHA+ }  kiliopo Welezo.
Alisema msaada huo unatokana na ahadi aliyoitoa hivi karibuni ya kukubali kusaidia watoto wenye  mazingira magumu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao wazazi wao wameshafariki  Dunia kutokana na maradhi hayo.
Halkadhalika alieleza kwamba amepata msukumo wa kutoa msaada huo hasa ikizingatiwa kwamba siku kuu ya Iddi el Hajj inakaribia ili wapate kusherehekea vyema Siku Kuu hiyo kubwa ambayo waumini wa Dini ya Kiislamu hukusanyika Makka Nchini Saudi Arabia Kutekeleza Nguzo ya Tano ya Kiislamu kwa wale muumini mwenye uwezo.
Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Zapha+ Bibi Hasina Hamad amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa uungwana wake wa kutekeleza ahadi aliyowapa ndani ya kipindi kifupi kilichopita.
Bibi Hasina alisema msaada huo licha ya kwamba hautokidhi mahitaji ya watoto hao moja kwa moja lakini inafurahisha kuona utapunguza mzigo mkubwa uliokuwa ukiukabili Uongozi wa Jumuiya hiyo katika kuwahudumia watoto hao.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini wa Zapha+ amewaomba wananchi, wahisani na wafadhili tofauti ndani na nje ya Nchi kuendelea kuunga Mkono juhudi za Jumuiya  hiyo ili ifikie lengo la kuanzishwa kwake.
“ Tunaamini kwamba wapo watu, washirika, wahisani na hata taasisi tofauti ziwe za Kijamii na hata za ziserikali ambazo zitajitokeza kuwasaidia watoto wetu hawa tukitambua kwamba hili ni jukumu letu zote jamii “. Alifafanua Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya Zapha+ Bibib Hasina Hamad.
Wakati huo huo Kampuni ya Malik Food inayojihusisha na biashara ya Kuku             { maarufu  Paja nono }  imeitikia wito wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Zapha+  wa kusaidia watoto wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ambao wazazi wao wameshafariki Dunia.
Akikabidhi Boksi Mbili za Mapaja ya Kuku zenye uzito wa Kilo  20 zikiwa na thamani ya shilingi 80,000/- Mkurugenzi wa Kampuni ya Malik Food Bwana Fikirini Hango alisema uongozi wa kampuni hiyo umeamua kutoa msaada huo ili kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia Jamii zenye kuishi katika mazingira Magumu.
Mkurugenzi Fikirini alisema licha ya Kampuni hiyo ya kuendesha biashara hiyo ya Kuku walio katika kiwango kinachokubalika lakini pia hujipangia utaratibu wa kutoa misaada kwa wananchi kulingana na mazingira ya mahitaji ya Jamii.
Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi Zanzibar Zapha + Bibi Consolata John aliipongheza Kampuni ya Malik Food kwa jitihada zake za kusaidia jamii hasa watoto mayatima muda wowote ule wanapoombwa kufanya hivyo.
Bibi Consolata aliikumbusha Jamii hapa Nchini kuendelea kuelewa kwamba jukumu la ulezi wa watoto wenye mazingira magumu ambao wameathirika na virusi vya ukimwi si la Jumuiya ya Zapha + pekee bali ni la Jamii yote kwa ujumla.

Tuesday, 1 October 2013

 Mmoja kati ya Wakulima wa Kijiji cha Nguruweni Dole Mzee Kitwana Mustaha aliishukuru na Kuipongeza  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi kwa kukamilisha ahadi yake ya kuwapatia hati za umiliki wa mashamba  wakulima hao kwa ajili ya kilimo katika maeneo yaliyowahi kuleta mgogoro kwa muda mrefu.
 Baadhi ya wananchi na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni wakiwa katika mkutano maalum  uliotishwa  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kukabidhiwa hati za umiliki wa mashamba ya kilimo katika maeneo yao.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Nguruweni kabla ya kuwakabidhi hati za umiliki wa mashamba ya kilimo wakulima hao.
 Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Hati ya umiliki wa shamba Bibi Josephine Yohana kwenye hafla maalum ya kumaliza mgogoro wa mashamba katika kijiji hicho.
 Balozi Seif akimpatia Hati Bwana Mohd Ali Pili ya kumiliki eneo la kilimo katika Kijiji cha Nguruweni  ambako kuliibuka mgogoro uliosababishwa na kuinbgizwa watu wasiohusika na maeneo hayo kwa kilimo.
























Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatahadharisha Wakulima wa Viijiji vya Ndunduke, Nguruweni na Dole  kuhakikisha kwamba maeneo ya kilimo waliyokabidhiwa na Serikali kwa shughuli za Kilimo wanayatumia  kama yalivyopangwa na kukubalika na pande hizo mbili.
Wakulima hao wakaonywa kuwa  ye yote atakaeamua maeneo hayo kuyakata viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba au kuyauza kwa mtu mwengine aelewe kwamba Serikali italazimika kumnyang’anya mkulima huyo mara moja.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akikabidhi hati  za umiliki wa mashamba ya kilimo kwa ajili ya wakulima 40 kati ya 181 wa Kijiji cha Nguruweni waliokuwa wakiilalamikia Serikali kwa kipindi kirefu kuidhinishiwa  mashamba wanayoyatumia ili kuendeleza shughuli zao za Kilimo.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya watu wenye tabia ya kuomba mashamba au eka kwa kisingizio cha kuendeleza kilimo lakini badala yake hujenga  tamaa inayowaelekeza kuanza kukata viwanja na kuuzia watu wengine.
“ Nataka nitahadharishe kabisa kwamba Mkulima ye yote atakayediriki kutumia fursa aliyopewa na Serikali ya kuendeleza kilimo kwenye shamba alilokabidhiwa na akaamua kufanya vyengine afahamu kwamba Serikali haitasita kunyang’anya shamba hilo mara moja “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  aliwapongeza wakulima hao wa Nguruweni kwa ustahamilivu wao mkubwa waliouchukuwa kwa kipindi kirefu kufuatia mgogoro wa maeneo waliyokuwa wakitumia kwa shughuli za kilimo baadhi yake kupewa watu wengine.
Balozi Seif alisema ustahamilivu huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuendeleza amani na utulivu kwenye Vijijini hivyo vya Nguruweni, Ndunduke pamoja  na Dole ambayo imeleta faraja kwa Serikali Kuu kwa vile haikuathiri shughuli za kila siku za kijamii.
Aliwakumbusha wakulima hao kwamba hivi sasa ni muda muwafaka wa kuendeleza shughuli zao za kilimo kwa vile wameshakuwa na uhalali wa kufanya hivyo katika maeneo waliyopewa na Serikali.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikisisitiza na kuhimiza kilimo kwa vile sekta hiyo bado inaendelea kuwa muhimili Mkuu wa uchumi wa Taifa hili.
“ Serikali imekuwa ikihimiza na kusisitiza umuhimu wa kilimo. Lakini Mkulima hawezi kuendeleza kilimo bila ya kuwa eneo la kilimo, sasa kwenu nyinyi hili suala  linaonekana kuondoka “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati Maalum aliyoiunda kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi kwa kushirikiana vyema na watendaji wa Wizara za Kilimo na Ardhi na kuutatua mgogoro huo wa muda mrefu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Ali Juma alisema Taasisi za Kilimo na Ardhi zililazimika kufanya uhakiki wa kina ili kuwatambua wakulima halali waliokuwa wakistahiki kupatiwa hati hizo.
Nd. Ali alisema uhakiki huo ulioshirikisha pia Masheha wa Vijiji vilivyohusika na mgogoro huo vya Nguruweni Ndunduke na Dole umeibua wakulima wapatao 181 ambapo  wakulima 40 kati ya hao wamethibitika kupatiwa hati hizo kwa awamu ya kwanza.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili alieleza kwamba kazi ya uhakiki sambamba na uchambuzi kwa wakulima wa Kijiji cha Dole imeshaanza rasmi na inatarajiwa kukamilika katika kipindi kifupi kijacho.
Akitoa shukrani zake Mwenyekiti wa Kamati  Maalum iliyounda  na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozib Seif kushughulikia mgogoro huo wa mashamba ya vijiji vya Nguruweni, Ndunduke na Dole Mh. Abdulla Mwinyi  alisema Wakulima wa Vijiji hivyo  wanapaswa kupongezwa kwa umahiri wao wa ustahamilivu kufuatia mgogoro huo wa mashamba kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Mh. Abdulla Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi amewaomba wale wakulima ambao bado mgogoro wao haujapatiwa ufumbuzi waendelee kuwa na subra kwa vile Serikali kupitia Uongozi wa Kamati hiyo unajitahidi katika kukamilisha mchakato huo.
Akitoa shukrani kwa Niaba ya Wakulima hao Mmoja wa Wazee wa Vijiji hivyo Mzee Kitwana  Mustafa alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ujasiri na uungwana wake aliouchukuwa wa kutimiza ahadi aliyowapa  mwaka jana wa kumalizika kwa kadia hiyo.
Mzee Kitwana alisema wakulima wa Vijiji hivyo wamefarajika na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwatatulia kero lililokuwa likiwasumbua kwa miaka mingi iliyopita.
“ Ile furaha yetu tuliyonayo leo kama tumengeruhusiwa basi tunatamani tukubebe na matope yetu Mzee wetu kwa jinsi ulivyotujali na kututhamini  kwa katambua kwamba tulikuwa tukisumbuka kweli kweli “ Alionyesha furaha yake Mzee Kitwana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwahi kutoa  ahadi kwa wakulima hao wa Nguruweni, Ndunduke na Dole  kwamba Serikali  itayagawa maeneo  yote ambayo kamati aliyoiunda tarehe 14 Disemba Mwaka 2012 Chini ya Mwenyekiti wake Mh. Abdulla Mwinyi  kufanya uhakiki wa mashamba yote yaliyoleta mgogoro.
Wakulima hao waliwahi kutoa shutuma kali kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif dhidi ya watendaji na Maafisa  wanaosimamia Ardhi, Kilimo wakiwemo pia Viongozi wa ngazi ya kati wa Serikali kwa vitendo vyao vya kuingiza wakulima waliokuwa hawahusiki na mashamba hayo.
Watendaji hao walituhumiwa na wakulima hao kuvuruga  jukumu  walilopewa la kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya kwanza waliokubalika kupatiwa hati za umiliki huo chini ya aliyekuwa waziri Kiongozi wa mwisho wa SMZ  Mh. Shamsi Vuai Nahodha.
 Serikali ililazimika kuzuia utolewaji wa hati hizo kufuatia hitilafu zilizojichomoza za kupandikizwa baadhi ya watu wasiohusika jambo ambalo lilisababisha mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima hao na watendaji waliopewa jukumu la kusimamia suala hilo.

 Othman Khamis  Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/10/2013.